Jul 27, 2022 03:23 UTC
  • Jumatano tarehe 27 Julai 2022

Leo ni Jumatano tarehe 27 Dhulhija 1443 Hijria sawa na Julai 27 mwaka 2022.

Katika siku kama hii ya leo tarehe 27 Dhulhija miaka 752 iliyopita alifariki dunia Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kirani. Saadi Shirazi alizaliwa karibu mwaka 606 Hijria Qamariya katika familia ya kielimu kwenye mji wa Shiraz ulioko kusini mwa Iran na baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa wa Shiraz, akiwa kijana, Saadi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq. Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na maeneo mengine ya dunia. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi. Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi Shirazi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan.

Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi

Miaka 250 iliyopita, katika siku kama ya leo ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya katika karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja ya nchi zilizo huru za mashariki mwa Ulaya, iligawanywa baina ya nchi tatu za Urusi, Austria na Prusssia kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa. Ni muhimu kuashiria hapap kwamba hadi sasa Poland imeshawahi kugawanywa mara nne kati ya nchi tofauti.

Bendera ya Poland

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 5 Mordad mwaka 1358 Hijria Shamsiya, iliswaliwa rasmi Swala ya kwanza ya Ijumaa katika mji wa Tehran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Tehran ikiongozwa na marehemu Ayatullah Talaqani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu, kufuatia agizo la Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Swala ya Ijumaa haikuwa ikifanyika kutokana na kuweko anga ya udhibiti na ukandamizaji wa serikali ya Shah.

Ayatullah Talaqani

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran aliaga dunia huko Cairo, Misri. Aliingia madarakani baada ya baba yake yaani Rezakhan kuondolewa kwenye uongozi na kubaidishwa na Waingereza. Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad Reza Pahlavi alikuwa na uhusiano mkubwa na Uingereza na ndio maana akafanya jitihada za kulinda maslahi haramu ya nchi hiyo nchini Iran. Hata hivyo baada ya harakati za wananchi na kushinda harakati ya kuitaifisha sekta ya mafuta, maslahi ya Waingereza nchini Iran yalifikia tamati. Shah aliwakandamiza wananchi wa Iran kwa ngumi ya chuma na alikuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Suala hilo lilizidisha kasi ya harakati za Mapinduzi ya Kiislamu zilizoongozwa na hayati Imam Khomeini na mwaka 1357 Mapinduzi ya Kiislamu yalihitimisha utawala dhalimu wa Shah ambaye alikimbilia nje ya nchi na kufia Misri katika siku kama hii ya leo.

Muhammad Reza Pahlavi

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, ilianza operesheni kubwa ya kijeshi iliyopewa jina la "Mirsad" huko magharibi mwa Iran kwa lengo la kuwasambaratisha vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin. Kundi la Munafiqin ambalo lilikuwa limekusanya magaidi katika mpaka wa Iran na Iraq wakiwa na silaha nzito kutoka kwa utawala wa zamani wa Baghdad lilianza kuishambulia ardhi ya Iran siku mbili kabla ya kuanza operesheni hiyo. Kiongozi wa Munafiqin alidhani kuwa magaidi hao wangeweza kuvuka barabara kuu za Iran bila ya kizuizi na tabu yoyote na kufika haraka mjini Tehran. Hata hivyo wanajeshi wa Iran wakishirikiana na wananchi waliojitolea katika operesheni hiyo ya Mirsad waliwazingira vibaraka hao wa Munafiqin huko magharibi mwa nchi na kuwasambaratisha magaidi hao walio na uhusiano mkubwa na nchi za kigeni.

Operesheni ya Mirsad

 

Tags