Aug 17, 2022 02:30 UTC
  • Jumatano, Agosti 17, 2022

Leo ni Jumatano mwezi 19 Mfunguo Nne Mharram 1444 Hijria sawa na Agosti 17 mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein AS na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya Bani Umayyah. Msafara huo hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib AS ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala. Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad SAW huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah wakitanguliwa na kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein AS. 

Msafara wa mateka wa Karbala

 

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, wananchi wa Indonesia walianzisha mapambano ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mholanzi. Mapambano hayo yaliyoongozwa na Ahmad Sukarno yaliendelea kwa miaka minne huko Indonesia. Baada ya kushadidi mapambano hayo ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Indonesia, Umoja wa Mataifa uliiamuru serikali ya Uholanzi kuuasisi utawala kwa jina la " Umoja wa Indonesia na Uholanzi". Jamhuri ya Indonesia ilivunja umoja huo mwaka 1956 na kutangaza uhuru wa nchi hiyo na Sukarno akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo.

Ahmad Sukarno

 

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gabon iliyoko magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Atlantiki, ilipata uhuru wake. Wareno walifika huko Gabon kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15 Miladia. Hata hivyo nafasi ya kijiografia ya Gabon ilizuia kugunduliwa nchi hiyo hadi karne ya 19. Katikati ya karne ya 19 Wafaransa waliwasili Gabon na kuidhinishwa kuitawala nchi hiyo katika mkutano uliofanyika huko Berlin Ujerumani. Hatimaye mwaka 1960 Gabon ilipata uhuru. Kijiografia nchi ya Gabon inapakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, Cameroon na Equatorial Guinea.

Bendera ya Gabon

 

Miaka 35 iliyopita katika siku kama ya leo, Rudolf Hess makamu wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa jela nchini Uingereza. Hess ambaye alizaliwa mwaka 1894, alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Kinazi na miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya Hitler. Rudolf Hess alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya jinai za kivita ya Nuremberg nchini Ujerumani baada ya nchi hiyo kushindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Hess alijiua akiwa jela mwaka 1987.

Rudolf Hess pembeni mwa Adolf Hitler

 

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, kundi la kwanza mateka wa Kiirani waliokuwa wakishikiliwa katika magereza za kutisha za Saddam Hussein liliwasili katika ardhi ya Iran. Kuachiwa huru mateka hao ilikuwa hatua muhimu ya kutekelezwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya Iran na Iraq. Saddam Hussein ambaye wakati huo alikuwa chini ya mashinikizo kutokana na kuivamia Kuwait alikubali kuwaachia huru mateka hao wa Iran na kurejea katika mipaka inayokubalika kimataifa ya nchi mbili baada ya kukubali mkataba wa mpaka wa Algeria. 

Mateka wa Iran waliokuwa wanashikiliwa na Saddam Hussein

 

Na miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliondoka kikamilifu katika eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina baada ya miaka 38 ya kukalia mabavu eneo hilo na kutenda jinai. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, eneo la Ukanda wa Gaza limegeuka na kuwa nembo ya muqawama na kusimama kidete katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Wazayuni wakiwa na lengo la kushinda muqawama wa Kiislamu, wamelishambulia eneo la Gaza mara kadhaa ambapo shambulio la mwisho lilikuwa la Ijumaa ya tarehe 5 Agosti mwaka 2022 vita ambavyo vimedumu kwa muda wa siku 3. 

Wanajeshi wa utawala katili wa Israel

 

Tags