Aug 18, 2022 02:43 UTC
  • Alkhamisi, Agosti 18, 2022

Leo ni Alkhamisi mwezi 20 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria sawa na Agosti 18 mwaka 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1369 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.

Eneo la Ajnadeen huko Palestina

 

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasser Deen Shah Qajar na kufanikiwa kutoa athari zenye thamani kubwa za uchoraji.

Muhammad Ghaffari maarufu kwa jina la Kamal al-Mulk

 

Katika siku kama hii ya miaka 43 iliyopiya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuvunjwa mzingiro na kukombolewa eneo la mpakani la Paveh huko Magharibi mwa Iran. Eneo hilo lilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na baadhi ya makundi yaliyokuwa yakipiga vita Mapinduzi ya Kiislamu. Makundi hayo yalikuwa yakisaidiwa na madola ya kigeni na yalianzisha machafuko katika maeneo mbalimbali ya Iran baada tu ya ushindi wa Mapindzi ya Kiislamu hapa nchini. Baada ya amri hiyo ya Imam Khomeini wananchi na wanajeshi waliharakia kwenda eneo la Paveh na kulikomboa kikamilivu.

 Dk Chamran na wanamapambano wenzake walikuwa na nafasi kubwa katika ukombozi wa Paveh

 

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbali mbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran.

Azimio namba 598

 

Tags