Aug 19, 2022 02:38 UTC
  • Ijumaa, Agosti 19, 2022

Leo ni Ijumaa mwezi 21 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria sawa na tarehe 19 Agosti 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 718 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Muharram 726 Hijria, alifariki dunia faqihi na msomi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu, Hassan bin Yussuf bin Mutahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli. Allamah Hilli alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khaja Nasiruddin Tusi na anatajwa kama miongoni mwa wasomi wa kipekee wa zama zake. Aliandika zaidi ya vitabu mia moja katika taaluma mbalimbali za Kiislamu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni Tadhkiratul Fuqahaa' ambacho kinaelezea mitazamo mbalimbali za madhehebu ya Kiislamu, tafsiri ya Qurani Tukufu ya 'Nahjul Imaan' na 'Muntahaal Matwalib'.

Hassan bin Yussuf bin Mutahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli

 

Miaka 360 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Blaise Pascal, mwandishi, mwanahesabati na mvumbuzi wa calculator au kikokotoo wa Kifaransa. Alizaliwa Juni mwaka 1623 na tangu utotoni Pascal alivutiwa mno na somo la hisabati. Vilevile urafiki uliokuwepo kati ya baba yake Pascal na msomi mmoja maarufu wa zama hizo ulisaidia mno katika kuchanua kipawa na kugunduliwa uwezo wa kijana huyo katika taaluma ya hisabati. Mwishoni mwa umri wake Blaise Pascal alijielekeza mno katika masuala ya dini na kuandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. 

Blaise Pascal

 

Siku kama hii ya leo miaka 203 iliyopita aliaga dunia mvumbuzi na mhandisi wa Kiingereza James Watt. Msomi huyo alipendelea na kuvutiwa mno na utafiti kuhusu masuala ya kisayansi. Katika utafiti wake Watt alifanikiwa kuvumbua nishati ya mvuke na kuzusha mapinduzi makubwa katika sekta ya viwanda hususan usafirishaji wa nchi kavu na baharini.

James Watt

 

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, kulifanyika mapinduzi ya Kimarekani dhidi ya serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq nchini Iran na baadaye kidogo Shah Reza Pahlavi akatwaa tena madaraka ya nchi. Mapinduzi hayo ambayo yalipangwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA kwa ushirikiano wa Uingereza, yaliiondoa madarakani serikali ya Musaddiq kupitia njia ya kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya wanaharakati wa kisiasa na wananchi na kueneza anga ya ghasia na machafuko nchini. Vilevile yalimrejesha Iran Shah Pahlavi ambaye siku tatu kabla alikuwa amekimbilia nchini Italia. Kabla ya tukio hilo la kusikitisha, wananchi Waislamu wa Iran walikuwa wamefanikiwa kukata mkono wa Uingereza hapa nchini na kutaifisha sekta ya mafuta iliyokuwa ikidhibitiwa na wakoloni hao.

Dakta Muhammad Musaddiq

 

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 28 Mordad 1357, Hijria Shamsia, vibaraka wa utawala wa Shah walifanya maafa ya kutisha ya kuchoma moto jumba la sinema la Rex katika mji wa Abadan kusini mwa Iran. Katika tukio hilo la kinyama la kuchomwa moto Jumba la Sinema la Rex, watu wasio na hatia 377 wakiwemo watoto na wanawake walipoteza maisha yao. Jinai hiyo ilifanywa na maajenti shirika hatari la ujasusi la Savak na vibaraka wa utawala wa Shah. Watu karibu 700 waliokuwa wakitazama sinema katika jumba hilo walifungiwa ndani baada ya moto kuzuka na mamia miongoni mwao wakateketea. Tukio hilo lilizusha hasira kubwa baina ya wananchi. Utawala wa Shah ulifanya maafa hayo na kisha kuwatuhumu wanamapinduzi kuwa ndio waliotekeleza shambulizi hilo la kutisha kwa shabaha ya kuchafua sura la harakati za Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wananchi. Hata hivyo njama hizo za Shah zilifeli. 

Jumba la sinema la Rex lililochomwa moto na vibaraka wa Shah huko Abadan

 

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita alifariki dunia Dakta Azar Andami mwanafizikia, mhakiki na mtaalamu mahiri wa bakteria wa Kiirani. Alizaliwa katika eneo la Rasht katika mkoa wa Gilan huko kaskazini mwa Iran. Alikuwa na kipaji kikubwa cha masomo. Azar Andami alihitimu masomo ya PhD katika Chuo Kikuu cha Tehran. 

Dakta Azar Andami

 

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Urusi ya zamani wakiongozwa na Gennady Ivanovich Yanayev walifanya mapinduzi dhidi ya rais wa mwisho wa Muungano wa Sovieti, Mikhail Gorbachev. Wanajeshi hao walitaka kukomeshwa marekebisho ya Gorbachev na kuzuia mpango wa kugawanywa Urusi ya zamani. Wakati wa mapinduzi hayo Mikhail Gorbachev alikuwa katika Peninsula ya Crimea huko kaskazni mwa Bahari Nyeusi. Hata hivyo Boris Yeltsin ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Federesheni ya Urusi na ambaye alikuwa akiungwa mkono na Magharibi, alizima mapinduzi hayo kwa msaada wa wananchi na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini. Kushindwa kwa mapinduzi hayo kulizidisha uwezo na satua ya Boris Yeltsin na kuharakisha mwenendo wa kusambaratika Urusi ya zamani hapo mwaka 1991.

Gennady Ivanovich Yanayev

 

Tags