Oct 07, 2022 02:36 UTC
  • Ijumaa tarehe 7 Oktoba, 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 1444 Hijria sawa na Oktoba 7 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1489 iliyopita alifariki dunia babu yake Mtume Muhammad (saw), Bwana Abdul Muttalib katika mji wa Makka. Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa wakuu wa kabila la Kuraish kabla ya kudhihiri Uislamu na alikuwa hodari mno katika fasihi ya lugha ya Kiarabu. Bwana Abdul Muttalib alikuwa msimamizi na mshika ufunguo wa nyumba tukufu ya al-Kaaba. Vilevile babu huyo wa Mtume alikuwa akitayarisha chakula na maji kwa ajili ya watu wanaozuru nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kazi hiyo aliirithi kutoka kwa baba yake. Aliheshimu mno mikataba na ahadi zake na kwa sababu hiyo alikuwa na ushawishi mkubwa baina ya watu. Miongoni mwa watoto wa mtukufu huyo ni Abdullah, baba yake Mtume wetu Muhammad (saw) na Abu Twalib, baba yake Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Tarehe 10 Rabiul Awwal miaka 1472 iliyopita, yaani miaka 28 kabla ya Hijra, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwailid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu. Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw), Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenzi wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw). Aidha Bibi Khadija (as) aliishi pamoja na Mtume kipindi cha miaka 25 na daima alikuwa mke mwema na mwenye kujitolea kwa mumewe Mtume Muhammad (saw) mbora wa walimwengu. Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya Bibi Khadija mtoharifu.

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kufuatia kushadidi harakati za kupigania katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kufanikisha kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alazimika kutekeleza jambo hilo.

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan.

Sohrab Sepehri

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti lilivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita yaani tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. 

 

Tags