Apr 19, 2018 20:31 UTC
  • Imam Husain (AS) Nyota ya Fadhila (Kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Husain AS)

Tarehe 3 Shaaban ni siku ambayo mji wa Madina ulishuhudia kuzaliwa mtoto mwingine katika nyumba ya Bibi Fatimatuz Zahra SA binti mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Huyo alikuwa ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia hiyo ambayo Mtume Muhammad SAW alikuwa siku zote akiwaita watu wa familia hiyo kuwa ni Ahlul Bayt wake na daima akiwaombea dua za kheri na amani. Katika Qur'ani Tukufu pia kuna aya inayotaja ubora, utukufu na usafi wa watu wa nyumba hiyo.

 Katika sehemu moja ya aya ya 33 ya Suratul Ahzab tunasoma: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Ahlul Bayt (Watu wa Nyumba ya Mtume), na kukusafisheni baarabara. Mama wa kitoto hicho kichanga alikuwa ni Faatimah, binti wa Bwana Mtume ambaye alikuwa na sifa za ukamilifu wa kibinaadamu alijipamba kwa sifa bora kabisa za kimaadili kiasi kwamba anahesabiwa kuwa ni mwanamke bora zaidi duniani.

Mwenyezi Mungu anataja fadhila za Bibi Faatimah katika Suratu al Kauthar wakati maadui wa Bwana Mtume walipokuwa wakimfanyia tashtiti kuwa amekatikiwa na kizazi, Mwenyezi Mungu akamliwaza Mtume Wake akimwambia kuwa hao wanaofanya chagizo hizo wao ndio waliokatikiwa na kizazi kwani kizazi cha Bwana Mtume kingelineemeka na kuenea kote dunia kupitia kwa Bibi Fatimatuz Zahra SA. 

Mtume Muhammad SAW amesema: Hasan na Husain ni Maimamu, wawe wamekaa au wamesimama

 

Baba wa kitoto hicho ni Ali mwanamme wa kwanza kuwa Muislamu. Imam Ali AS alijulikana vilivyo kwa ushujaa wake na kutotetereka kwake katika kuilinda na kuitetea dini tukufu ya Kiislamu.Baada ya kuzaliwa, kichanga hicho kilipelekwa katika "mahdhar" tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Imam Ali AS akamuomba Bwana Mtume kwa heshima zote amchagulie jina mtoto huyo, naye Bwana Mtume hakuajizi ila alimchagulia jina mara moja akamwita Husain.

Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwenu nyinyi nyote kwa mnasaba huo adhimu.Mapenzi ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa Imam Husain AS yalikuwa makubwa kiasi kwamba hayakufichika kwa mtu yeyote yule. Binti ash Shatwi, msomi wa kike wa Misri anasema kuhusu mapenzi makubwa aliyokuwa nayo Bwana Mtume kwa mjukuu wake Imam Husain kwamba: "Majina na Hasan na Husain kwa Bwana Mtume yalikuwa mithili ya wimbo mzuri na sauti ya kutuliza na kuburudisha moyo, na Bwana Mtume alikuwa hachoki kukariri mara kwa mara majina hayo. Alikuwa akiwaita Hasan na Husain kuwa ni wanawe. Mwenyezi Mungu alimpa Zahra neema kubwa sana ya kuendeleza kizazi cha Bwana Mtume na alimpa heshima hiyo pia Ali ambaye kupitia kwake, kizazi cha Mtume kimeendelea hadi leo hii." Mwisho wa kunukuu.

Haram ya Imam Husain AS mjini Karbala Iraq

 

Mapenzi ya Bwana Mtume kwa kitoto hicho hayakutokana tu na uhusiano wake wa kidamu na nasaba. Kwani kwa mujibu wa nasi ni kwamba Bwana Mtume alikuwa hafanyi chochote kwa mapenzi ya nafsi, bali yote yalikuwa ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mapenzi ya Bwana Mtume kwa Hasan na Husain yalitokana na nafasi ya aina yake waliyokuwa nayo watukufu hao mbele ya Mola Muumba. Moyo wa Bwana Mtume ulijaa mapenzi kwa wajuu zake hao kiasi kwamba amenukuliwa akisema: Yeyote anayewapenda wajukuu zake hao ni sawa na kwamba amempenda yeye na yeyote anayewafanyia uadui ni kana kwamba amemfanyia yeye uadui.Imam Husain AS alikuwa bado kijana mdogo wakati kilipojiri kisa cha Mubahala. Mtume Muhammad SAW aliwachukua Hasan na Husain kwa jina la wanawe katika kisa hicho ambapo Wakristo wa Najiran walipoona watu aliofuatana nao Bwana Mtume yaani Bibi Faatimah, Ali na watoto wao wawili, waliogopa mno na hawakuthubutu kuendelea na upinzani wao. Kisa cha Mubahala ni maarufu kwa wanaofuatilia matukio ya Kiislamu.Lakini miaka ya furaha haikurefuka kwani ilikuwa ni takriban baada ya miaka sita ya tangu kuzaliwa Imam Husain AS ndipo alipofariki dunia Bwana Mtume SAW. Bwana Mtume ameusia sana juu ya umuhimu wa kuwapenda na kushikamana na Ahlul Bayt wake.

Amma baada ya kufariki dunia Mtume na kupita miaka mingi hadi Waislamu walipomshikilia Imam Ali AS achukue uongozi wa dola ya Kiislamu, miaka yote hiyo Imam Husain na kaka yake Imam Hasan walikuwa bega kwa bega na baba yao Imam Ali na walishiriki vilivyo katika masuala yote ya kisiasa, kijeshi na mengineyo mengi.Hata baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ali AS, Imam Husain alikuwa bega kwa bega na kaka yake Imam Hasan katika njia ya kutangaza na kupigania dini ya Mwenyezi Mungu. Ushujaa wa Imam Husain na kujitolea kwake katika njia ya Mwenyezi Mungu uliendelea hadi kwenye hamasa ya kihistoria ya ushindi wa damu dhidi ya upanga katika jangwa la Karbala.

 

Ni jambo lisilo na shaka kwamba Bwana Mtume na Ahlul Bayt wake ni viumbe bora kabisa. Sira, mwenenendo na maisha ya Imam Husain AS yalijaa mapenzi kwa watu. Sifa ya mtukufu huyo ya kuwa pamoja na watu wakati wote kwa shida na raha na miongoni mwa sifa za kipekee za Imam Husain ilikuwa ni usamehevu. Kusamehe na kujitolea ni miongoni mwa sifa tukufu za waja wema.

Ni vyema hapa tukikusimulieni kisa kifupi kilichotokea zama za Imam Husain AS. Bwana mmoja kutoka Sham aliyejulikana kwa jina la Isam alitembelea mji mtukufu wa Madina. Kwa bahati alionana na mtu ambaye sura yake ilijipambanua na ya watu wengine alipouliza huyo alikuwa ni nani aliambiwa na Husain bin Ali mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Mwenyeji huyo wa Sham ambaye alikuwa amejazwa chuki zisizo na kifani dhidi ya Imam Ali AS na wanawe, aliona hiyo ndiyo fursa nzuri ya kutoa hiqdi na chuki kubwa aliyokuwa nayo moyoni. Bila woga wala kusita, alimkabili Imam Husain AS kwa kila aina ya tusi, shutuma, fihi na uhasidi, alimradi alitoa kila uchukivu aliokuwa nao rohoni. Wakati wote huo Imam Husain alikuwa anamwangalia kwa macho mtule huyo wa watu. Alipomaliza kujifaragua kwa matusi, Isam alisubiri kijeuri kuona radiamali ya Imam Husain AS. Lakini tofauti na alivyotarajia, radiamali ya Imam haikuwa ya kughadhibika wala tone la kukasirika. Alimwangalia kwa jicho la kumhurumia Bwana yule wa Sham na kwa upole akamwambia, unaonekana wewe ni mgeni hapa, kama una shida niko tayari kukusaidia, kama huna pa kufikia milango ya nyumba yangu iko wazi kwa ajili yako. Bumbuwazi lilitanda kwenye uso wa Isam, soni zikafunika paji lake la uso, akatafuta pa kuweka uso wake akashindwa kutokana na haya na kufedheheka. Isam anaendelea kusimulia kisa hicho akisema: Wakati huo nilitamani ardhi ipasuke nididimie ndani lakini hilo halikuwa." Kwa muda huo mchache, Isam alibadilika na kuwa miongoni mwa wafuasi watiifu kabisa wa Watu wa Nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Imam Husain ana maneno mengi ya hekima na miongoni mwake ni haya yasemayo: Kuna neema tano kubwa ambazo mtu akiwa nazo hubarikiwa katika maisha yake; akili, dini, adabu, haya, wema na maadili bora. Kwa mara nyingine tunatoa mkono wa baraka kwa mnasaba huu mtukufu wa kukumbuka siku aliyozaliwa Imam Husain AS. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags

Maoni