Nov 20, 2018 12:11 UTC
  • Wiki ya Umoja: Uislamu unaoshajiisha Umoja; dharura ya leo ya ulimwengu wa Kiislamu

Tuko katika siku tukufu za Wiki ya Umoja wa Kiislamu, ambayo ni wiki ya kuadhimishwa uzawa na maulidi ya Mtume Mtukufu Muhammad (saw).

Ahlu Suna wal Jamaa wanategemea baadhi ya riwaya katika kuamini kwamba Mtume Mtukufu (saw) alizaliwa tarehe 12 Rabiul Awwal nao Waislamu wa madhehebu ya Shia wana riwaya nyingine nyingi zinazowafanya waamini kuwa mtukufu huyo (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal. Kipindi cha kati ya tarehe hizo mbili kilitangazwa na Imam Khomeini (MA) kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ili kuleta umoja na mfungamano kati ya Waislamu bila kujali madhehebu zao. Kwa kutilia maanani hali ambayo inawakabili Waislamu ulimwenguni na hujuma inayotekelezwa dhidi ya Uislamu na Waislamu katika pembe tofauti za dunia, tunaweza kusema kuwa suala la kuwepo umoja kati ya Waislamu ni suala muhimu sana kwa ajili ya kuwawezesha kukabiliana na fitina za maadui wao. Ni wazi kuwa madhara ambayo yamewapata Waislamu katika miongo kadhaa iliyopita yametokana na kuwepo migawanyiko na hitilafu miongoni mwao. Nara ya Waingereza inayosema 'tawanya (gawa) utawale' ni moja ya stratejia muhimu ambazo zimekuwa zikitumiwa na maadui wa Uislamu na Waislamu kwa madhara ya umma wa Kiislamu. Mtazamo wa harakaharaka kuhusu hatua laini na zisizo laini, vikiwemo vyombo vya propaganda na silaha, ambazo zimekuwa zikitumiwa na maadui katika kipindi hiki unathibitisha wazi kwamba hakuna jambo ambalo limelengwa na maadui hao wa Uislamu kama mshikamano na umoja wa Uislamu. Njama za kuushughulisha ulimwengu wa Kiislamu na migawanyiko, machafuko, ghasia na vita vya kikabila na kimadhehebu sambamba na kuenezwa propaganda za kuufanya Uislamu na hasa Ushia ukiongozwa na Iran uogopewe na kuchukiwa duniani, zote hizo ni hatua hatari ambazo zimekuwa zikitekelezwa na maadui kwa lengo la kuuharibia Jina Uislamu na kuvuruga umoja wa Waislamu. Hivi sasa Waislamu wanakabiliwa na changamoto na machungu makubwa katika pembe tofauti za dunia ambapo Yemen, Bahrain, Nigeria, Myanmar, Kashmir, Afghanistan, Iraq, Syria na Palestina ni sehemu ndogo tu ya machungu wanayoyapitia Waislamu. Kama umoja ungekuwepo miongoni mwa Waislamu huenda hali hiyo ya kusikitisha isingeshuhudiwa katika baadhi ya nchi za Kiislamu. Kwa msingi huo ni wazi kuwa Waislamu wanapasa kuzingatia vyema mafundisho ya kitabu chao kitakatifu cha mbinguni, yaani Qur'ani Tukufu na Suna za Mtume wao Mtukufu ambayo yanawahimiza kuwa na umoja baina yao.


Kudhihiri na kuenezwa  fikra za ukufurishaji na ugaidi kama vile wa Daesh katika nchi za Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni bila shaka ni njama zinazofanywa na maadui wa Uislamu kwa lengo la kuzuia kupatika umoja miongoni mwa Waislamu na kuchafua sura nzuri ya Uislamu unaohimiza uadilifu, amani, upendo na kuwepo maadili mema miongoni mwa wanadamu. Ni wazi kuwa iwapo umoja na mshikamano utadumishwa miongoni mwa Waislamu, bila shaka maadui wa Uislamu hawatapata fursa wala mwanya wa kupenya na kueneza fitina na mifarakano kati yao. Kuna Aya nyingi mno za Qur'ani ambazo zinahimiza na kusisitiza umoja na maelewano kati ya Waislamu. Mhimili wa umoja kwa mtazamo wa Qur'ani ni Tauhidi na kisha dini ya Uislamu katika hatua inayofuata. Qur'ani ilimtuma Mtume Mtukufu (saw) kwenda kwa Watu wa Kitabu (Wakristo) na kuwataka wazingatie na kufuata Tauhidi na sio kitu kingine chochocte. Aya ya 64 ya Surat Aal Imran inasema: Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu pia anasema katika Aya ya 103 ya Sura hiyohiyo ya Aal Imran: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane.

Ni wazi kuwa umoja na mshikamano wa Waislamu huwapa nguvu kubwa ya kuweza kukabiliana na njama za maadui. Nguvu hiyo ni mfano wa nguvu kubwa ambayo huletwa na mkusanyiko wa matone madogomadogo ya mvua ambayo hata kama mwanzoni huwa si kitu, lakini hukusanyika pamoja na kuweza kuunda nguvu kubwa. Mito na mabwawa makubwa tunayoyashuhudia hii leo katika pembe tofauti za dunia na ambayo hutumika kuzalisha nguvu za umeme zinazotumika kuendeshea mitambo na mashine tofauti viwandani, kwa hakika ni natija ya mkusanyiko wa matone hayo madogomadogo ya mvua. Iwapo matone kama hayo yanaweza kubuni nguvu hii kubwa na ya ajabu bila shaka umoja na mshikamano wa Waislamu unaweza kusababisha nguvu maradufu ya hiyo inayosababishwa na matone ya mvua, na hivyo kusukuma mbele malengo ya maendeleo na ya kibinadamu na wakati huohuo kuzuia kufikiwa malengo yasiyo ya kibinadamu yanayofuatiliwa na madola ya kibeberu na kikoloni. Ni wazi kuwa kuthibiti hali hiyo kutachangia pakubwa ustawi, nguvu na utukufu wa mwanadamu.


Bila shaka mchangiaji mkubwa zaidi wa umoja na mshikamano wa Waislamu katika zama zetu hizi ni Imam Khomeini (MA) mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Alikuwa akiamini kwamba umoja, ambalo ni lengo muhimu la Uislamu huleta nguvu, na utengano hudhoofisha misingi na nguzo za dini. Imam Khomeini (MA) aliwasilisha mikakati mbalimbali ya kuleta na kuimarisha umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu na yeye mwenyewe kuchukua hatua za kivitedo kufikia lengo hilo. Aliamini kwamba mojawapo ya njia na mikakati muhimu ya kuleta umoja miongoni mwa Waislamu ni kuasisiwa serikali ya Kiislamu. Siku moja tu baada ya kufikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Imam aliashiria wazi suala hilo kwa kusema: "Sisi na Waislamu wa Ahlu Suna ni wamoja. Sisi ni wamoja kwa sababu ni Waislamu na ndugu. Iwapo mtu atatamka neno ambalo litasababisha kudhihiri mfarakano kati yetu basi na aelewe kuwa atakuwa amefanya hivyo kutokana na ujahili wake au ni miongoni mwa watu wanaotaka kuleta hitilafu miongoni mwa Waislamu. Suala hapa sio la Ushia na Usuni; sisi sote ni ndugu." Miezi kadhaa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini, aliwatumia ujumbe wakazi wa eneo la Kurdistan magharibi mwa Iran ambao wengi ni wafuasi wa Ahlu Suna kwa kusema: "Vibaraka wa madola ya kigeni ambao wanayaona maslahi yao na ya mabwana zao yako yakiwa hatarini, wanaeneza hitilafu za Shia na Suni kwa ajili ya kuwachochea ndugu zetu wa Ahlu Suna na mauaji kati ya ndugu, na wanataka kutumia mbinu chafu kueneza hitilafu kati ya ndugu wamoja. Katika Jamhuri ya Kiislamu ndugu wa Kisuni na Kishia wako pamoja na wote wana haki sawa. Yeyote anayeeneza mambo kinyume na haya ni adui wa Uislamu na Iran na ndugu zetu wa Kikurdi wanapasa kuzima bila kusita propaganda hizi zisizo za Kiislamu."


Ayatullah Ali Khamenei ambaye alichukua usukani wa uongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya kuaga dunia Imam Khomeini (MA), pia amekuwa akisisitiza mara kwa mara juu ya udharura na umuhimu wa kuzingatiwa umoja na mshikamano wa Waislamu ulimwenguni, na sera za mfumo wa Kiislamu wa Iran zimekuwa zikiainishwa kwa mtazamo huo. Katika moja ya hotuba zake anazungumzia njama zinazofanywa na maadui wa Uislamu kwa madhumuni ya kuleta mifarakano na migawanyiko kati ya Waislamu kwa kusema: "Kuna watu bilioni moja duniani ambao wana imani moja kuhusu Mwenyezi Mungu, Mtume, Swala, Hija, Kaaba, Qur'ani na itikadi nyingine nyingi za kidini na wanahitilafiana katika masuala machache tu. Watu hawa hawapasi kupigana vita kuhusiana na hitilafu hizo ndogo na kuamua kushirikiana na watu wasiomwamini kabisa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) na ambao wanapinga moja kwa moja dini na mafundisho yanayofungamana nayo." Mshikamano wa umma wa Kiislamu katika mtazamo wa Ayatullah Khamenei ni kudiriki machungu ya pamoja, maadui wa pamoja na uwezo wa mapoja. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu analipa umuhimu mkubwa suala la umoja wa Kiislamu kwa kadiri kwamba katika jumbe na hotuba zake mbalimbali amekuwa akiwasihi wasomi, viongozi wa serikali, wanafikra, wanazuoni na Waislamu wa matabala mbalimbali kuzingatia kwa kina mafundisho ya Qur'ani na suna za Mtume Mtukufu (saw) katika miamala, maisha na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Umoja katika mtazamo wa Kiongozi Muadhamu una maana ya kutokuwepo mifarakano, mapigano, mivutano na ghasia katika jamii ya Kiislamu. Anaamini kwamba inatosha kwa wafuasi wa madhehebu mbili hizi muhimu za Uislamu za Shia na Suni kuhisi kuwa ndugu na lengo la umoja wa Kiislamu sio kuwafanya Mashia kuwa Masuni wala Masuni kuwa Mashia. Ulimwengu wa Kiislamu hii leo unahitajia umoja kuliko wakati mwingine wowote ule. Mifarakano na ukufurishaji ni balaa kubwa ambayo imewakumba Waislamu ambao wote wanamwamini Mwenyezi Mungu mmoja na Mtume wake (saw), wana Kitabu kimoja cha mbinguni na wanaswali wakiwa wameelekea upande mmoja wa Kibla. Maadui wa Uislamu hivi sasa wanapiga ngoma ya mifarakano na kuzua fitina miongoni mwa Waislamu kuliko wakati mwingine wowote na kuota ndoto ya kuzidhibiti nchi zote za Kiislamu. Katika kipindi kigumu kama hiki Mwenyezi Mungu anawasihi waja wake wema wote kuzingatia umoja na mshikamano baina yao. Kuitikia wito na nasaha hiyo ya Mwenyezi Mungu bila shaka kutawaletea Waislamu, saada, ufanisi, heshima na utukufu wa kudumu.

Tags

Maoni