Feb 02, 2019 13:15 UTC
  • Alfajiri Kumi na Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Tarehe 12 Bahman sawa na tarehe Mosi Februari, inasadifiana na mwanzo wa sherehe za kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Siku hiyo kiongozi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamuو Imam Ruhullah Khomeini alirejea nchini baada ya kuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15. Baada ya Shah Muhammad Reza Pahlavi dikteta wa zamani wa Iran kutoroka nchi hapo tarehe 16 Januari mwaka 1979, Imam Khomeini aliamua kurejea nchini lakini waziri mkuu wa mwisho wa serikali kibaraka ya Shah, Shapour Bakhtiyar alifunga viwanja vyote vya ndege akitaka kuzuia ndege iliyokuwa imembeba Imam kutua hapa nchini. Katika miezi mitatu ya mwishoni mwa utawala wake, Shah Muhammad Reza Pahlavi alibadili mawaziri wakuu mara tatu wenye mielezo tofauti ili asaa akaweza kulinda utawala wake wa kifalme lakini mipango yote hiyo haikuweza kuzuia harakati ya mwamko wa wananchi ya kuuondoa madarakani utawala huo kibaraka. Baada ya kuunda serikali yake, Bakhtiyar alifuatilia malengo matatu makuu. Kukomesha migomo na maandamano, kurejesha nidhamu na utulivu na kufanya mapatano na Imam Khomeini. Bakhtiyar alishindwa kukomesha maandamano na migomo ya wananchi na kama si msaada wa Jenerali Robert Huyser wa Marekani na kuingiza nchini fedha zilizochapishwa nje ya nchi na jenerali huyo basi asingeweza hata kulipa mishahara ya wafanyakazi wa umma.

Shapour Bakhtiyar

Miongoni mwa matukio muhimu ya serikali ya siku 37 ya Shapour Bakhtiyar ni kufungwa viwanja vya ndege nchini na kumzuia Imam Ruhullah Khomeini kurejea nchini akitokea uhamishoni. Hata hivyo maandamano ya mamilioni ya wakazi wa Tehran na miji mingine yalimlazimisha Bakhtiyar kufungua viwanja vya ndege na hatimaye tukio la kihistoria la kurejea nchini Imam Khomeini. Baada ya kurejea nchini na kupokewa na mamilioni ya watu, Imam Khomeini alielekea moja kwa moja katika makaburi ya mashahidi waliouliwa na utawala wa Shah katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu na kutoa hotuba muhimu na ya kihamasa. Alisema katika hotuba hiyo kwamba ataainisha serikali mpya kwa msaada wa wananchi wa Iran.

Kurejea nchini Imam Khomeini ni miongoni mwa matukio muhimu sana ya historia ya sasa ya Iran. Tukio hilo lililotimia baada ya miaka mingi ya mapambano na kupigania haki na uadilifu, lilieneza harufu ya uturi ya uhuru na kujitawala tena katika maneo yote hapa nchini. 

Kuhusu mchango na nafasi ya Imam Khomeini katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei anasema: Kila panapotajwa jina la Imam Khomeini basi jina la Mapinduzi ya Kiislamu pia lipo hapo. Mambo hayo mawili pia yatasajiliwa na kujadiliwa daima katika historia ya Uislamu na dunia kwa ujumla na Imam  Ruhullah Khomeini atazungumziwa na kuendelea kuenziwa kama mwasisi wa mapinduzi hayo.   

Imam Khomeini akihutubia hadhara katika makaburi ya Behesht Zahraa

Hapana shaka kuwa, tukio hilo la kihistoria lisingeweza kutokea bila ya muono wa mbali, istiqama, kusimama kidete, kujitolea na uwezo mkubwa wa kiuongozi na azma kubwa ya mwanazuoni huyo wa kidini. Ni wasomi na wanafikra wachache sana duniani ambao waliwezi hata kudhania kuwa, harakati changa ya Imam Khomeini katika kipindi hicho kilichokuwa na mazingira makhsusi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ingeweza kufanya mapinduzi makubwa ya yasiyo na kifani katika dunia ya sasa. Harakati hiyo ya Imam ilidhihirisha mambo mawili makuu ambayo ni shakhsia adhimu ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na fikra za mfumo aali aliohuisha. Kimsingi katika harakati na mapinduzi yote ya dunia, uongozi huwa moja ya nguzo tatu muhimu za ushindi sambamba na aidiolojia na wananchi. Katika upande wa uongozi wa harakati za Mapinduzi, shakhsia ya Imam  Khomeini ilikuwa ya aina yake, na alisifika kuwa na hima kubwa, malengo aali, imani ya kupigiwa mfano, irada na azma imara na madhubuti, subira, kumtegemea sana Mwenyezi Mungu, kuwa makini na macho wakati wote, takwa na uchamungu, kusema ukweli na kuwa muwazi, usafi wa roho, kutazama mbali, kutumia hekima na busara na kadhalika, vitu ambavyo vilimfanya kiongozi mwenye haiba kubwa na mwenye mvuto makhsusi baina ya wananchi.  

Akieleza wasifu wa hayati Imam Ruhullah Khomeini katika moja ya hotuba zake, Kiongozi wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei anasema: "Kiongozi kipenzi, azizi na Imam wetu Mwenyezi Mungu amrehemu aling'aa sana duniani na katika zama hizi na hata za kabla yake hatujashuhudia shakhsia mkubwa mithili yake. Baada ya Manabii na Mawalii wa Mwenyezi Mungu, hatujawahi kuona shakhsia adhimu iliyokusanya sifa na vipawa vingi kama Imam Khomeini. Mimi naamini kuwa, siri kubwa ya mafanikio ya Imam ni ikhlasi yake, kuelekea na kushikamana kikamilifu na Allah SW."

Sifa nyingine ya Imam Khomeini ni fikra zake wakati wa mapambano hadi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Malengo na fikra zake zilitokana na asili ya itikadi ya Tauhidi na kumwamini Mwenyezi Mungu mmoja na kupigania uadilifu. Mafundisho ya dini yalitawala kila kitu kwake yeye na alihuisha thamani na maadili ya Kiislamu vilivyokuwa vimepuuzwa na kutupiliwa mbali katika jamii ya Iran. Imam Ruhullah Khomeini aliunganisha pamoja Uislamu na Uirani na dini na siasa na akaanzisha Jamhuri ya Kiislamu isiyotegemea madola mawili makubwa wakati huo ya Mashariki na Magharibi. Alipambana na ubeberu kwa himaya na msaada wa watu waliokuwa wakidhulumiwa na kuvitaja uhuru, kujitawala, kujiamini na kujitosheleza katika pande zote kuwa ni tunu na zawadi kubwa za dini tukufu ya Uislamu kwa wanadamu wenye fikra huru. 

Mbinu na mitazamo ya kisiasa ya Imam Khomeini ilitokana na maarifa yake makubwa ya kidini. Uongozi wake ulikuwa na sifa za kipekee suala ambalo liliwavutia hata wapinzani wake. Alisifika sana kupenda kushauriana na wataalamu, kusikiliza mitazamo ya maoni ya wenye ujuzi wa jambo fulani, kuwa na kifua kipana na uvumulivu katika kukabiliana na wapinzani wake na kuwapa nafasi na fursa watu wote wenye uwezo na sifa zinazohitajika, kutetea haki na uadilifu na kuwalinda na kuwatetea wanaodhulumwia bila ya kujali dini, kaumu na rangi zao.

Imam Ruhullah Khomeini

Kutokana na sifa hizo wanadharia wengi dunia walimsifu sana Imam Ruhullah Khomeini na kumtaja kuwa mwanafalsafa na mwanafikra mkubwa wa zama hizi. Inatupasa kusema hapa kuwa hata wapinzani wa Mapinduzi ya Kiislamu wanakiri kwamba, nguvu ya harakati ya Imam na sifa makhsusi za kiongozi wake vilikuwa na taathira kubwa katika ushindi wa harakati hiyo.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu maadui walifanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, yanafeli na kugonga mwamba. Njama hizo zote zilifanyika kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali na utawala mchanga wa Kiislamu. Hata hivyo umoja na mshikamano uliokuwa umejengwa na mhandisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran uliimarisha zaidi misingi ya utawala huo na kuufanya imara kama jabali na sasa Mapinduzi hayo yanatimiza miaka 40 baada ya kuvuka milima na mabonde na tufani za aina mbalimbali na njama za maadui wa Uislamu na ubinadamu.    

Tags

Maoni