Jul 03, 2019 07:39 UTC
  • Mwisho wa Apartheid Afrika Kusini na kuendelea kwake maeneo mengine ya dunia

Jumapili ya terehe 30 ilikuwa siku ya kumbukumbu ya tukio muhimu sana katika historia ya Afrka na dunia nzima. Ilikuwa siku ya kufutwa mfumo usio wa kibinadamu wa Apartheid huko Afrika Kusini mwaka 1991.

Siku hiyo mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid ambao ni miongoni mwa sura za ukatilii na unyama wa kutisha na ubaguzi wa kizazi uliotawala Afrika Kusini kwa miaka mingi kwa maslahi ya wazungu waliowachache dhidi ya wazalendo weusi, ulifutwa rasmi. 

Apartheid ni neno ambalo katika lugha ya Afrikaans ya Waafrika Kusini ina maana ya kutenganisha, kwa maana ya mfumo wa ubaguzi wa rangi wa kutenganisha watu kwa misingi ya rangi na mbari zao, na ubaguzi wa kisiasa, kiuchumi, kijamii, kidini na kadhalika ambao aghlabu hufanywa na kundi linalotawala dhidi ya kaumu au kundi jingine la watu. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa, Apartheid ina maana ya kutenganisha watu wa rangi na mbari makhsusi, kuwalazimisha kuishi maeneo makhsusi na kuwanyima haki zao zote za kisiasa, kijamii na kibinadamu. Kwa ufupi tunaweza kusema, Apartheid ni hali inayoshabihiana sana na utumwa dhidi ya watu wanaotofautiana kimbari na kundi linalotawala au lenye nguvu. 

Siasa za ubaguzi wa rangi za wazungu dhidi ya wazalendo waliowengi zilianza kutekelezwa katika karne ya 17 na kuenea zaidi katika eneo hilo la kusini mwa bara la Afrika. Siasa hizo zilirasimishwa mwaka 1948 kwa jina la Apartheid baada ya chama cha The National Party (NP) kushika madaraka. Tangu mwaka 1953 siasa hizo zilishika kasi zaidi na kwa mujibu wake, wazungu wachache waliokuwa wakiunda asilimia 20 ya jamii huko Afrika Kusini walitambuliwa kuwa ni kizazi bora ambacho kilitawala na kuwa juu ya wazalendo weusi. Ndoa baina ya watu weupe na wazalendo weusi zilipigwa marufuku, na watu weusi walizuiwa kufanya harakati za kisiasa na kulazimishwa kufanya kazi mbaya na duni katika jamii.

Sheria zilizopasishwa na wazungu katika kipindi hicho ziliwatambua watu weupe kuwa ni raia wa daraja la juu ambao walipaswa kupewa haki na fursa zote za kijamii, kisaisa, kiuchumi, kielimu na kiutamaduni. Suala hili kwa hakika lilikuwa na maana ya kujenga ukuta na mtengano katika jamii ya Afrika Kusini ambayo katika upande mmoja ilikuwa na wazungu na watu weupe, na upande wa pili kuliwepo wazalendo weusi. Kila kitu kilitofautiana baina ya pande hizo mbili. Vyuo na shule za watu weupe zilitenganishwa na zile za watu weusi. Shule za wazungu zilitengewa bajeti kubwa na kupewa suhula zote bora zinazowezekana. Shule na vyuo hivyo vilishindana kwa ubora na vyuo bora zaidi duniani, ilhali shule na vyuo vya wazalendo weusi vilitengewa bajeti ndogo kupita kiasi na kwa msingi huo shule hizo zilikuwa taabani na katika hali ya kusikitisha. 

Ili kukabiliana na mfumo huu wa ubaguzi, tarehe 30 Novemba mwaka 1973 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 3068 la makubaliano ya kimataifa ya kuzuia ubaguzi wa Apartheid na kuutambua kuwa ni uhalifu. Azimio hilo liliutambua ubaguzi wa Apartheid kuwa ni uhalifu wa kimataifa na kuwatambua kuwa ni wahalifu wale wote wanaoshajiisha, kushirikiana au kula njama ya kutekeleza mfumo huo wa kikatili. 

Baada ya hatua hiyo walimwengu walitilia maanani zaidi na kufuatilia kwa makini mfumo wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini. Japokuwa Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi za Magharibi zilikuwa na uhusiano wa karibu sana na utawala wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini lakini nchi nyingi duniani zilikataka kabisa uhusiano na utawala huo na kupinga sera na siasa zake. Upinzani huo na mashinikizo ya walimwengu sambamba na mapambano ya wazalendo wa Afrika Kusini wakiongozwa na shujaa Nelson Mandela, hatimaye vilipelekea kufutwa mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini humo tarehe 30 Juni mwaka 1991. Disemba mwaka 1993 Bunge la Afrika Kusini lilipasisha katiba mpya iliyotambua haki sawa baina ya watu weupe na wazalendo weusi na katika uchaguzi wa kwanza uliowashirikisha watu weusi Aprili mwaka 1994, Mzee Nelson Mandela aliyefungwa jela miaka 27, alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini.

Japokuwa mfumo wa ubaguzi wa Apartheid umehitimishwa huko Afrika Kusini kutokana na mapambano makubwa ya wazalendo chini ya uongozi wa shujaa Nelson Mandela, lakini dunia bado inashuhudia mfumo mpya wa Apartheid ambao miongoni mwa mifano yake hai ni sera na siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Utawala huo umeifanya nchi ya Palestina kuwa hamamu ya damu na unazidisha ubaguzi wa Apartheid kila uchao. Ushahidi unaonesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ulikuwa mshirika na muitifaki mkubwa sana wa utawala wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kisini, hivi sasa na kwa sura rasmi na isiyo rasmi, unatekeza siasa za Apartheid za kuwatenganisha watu kwa mujibu wa mbari, imani na itikadi zao katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina. Kwa mfano tu, Wapalestina hawaruhusiwi kuishi katika vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi huko katika Ukingo wa Magharibi (West Bank) na mamia ya vitongoji vya makazi makhsusi ya walowezi ya Kiyahudi yamejengwa katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina. Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Habari cha Palestina Oktoba mwaka 2016 ilisema kuwa, utawala ghasibu wa Israel umejenga vitongoji 505 vya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi na karibu vitongoji 93 katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) ambavyo vina jamii ya zaidi ya watu milioni moja. Vitongoji hivyo ni kwa ajili ya makazi ya Wayahudi tu. Sambamba na hayo Wapalestina wananyimwa haki ya kujenga nyumba katika maeneo hayo nawanapokarabati nyumba zao za zamani basi nyumba hizo hubolewa kwa kutumia visingizio vya aina mbalimbali.

Makazi ya walowezi wa Kiyahudi, Ukingo wa Magharibi

Mfano mwingine hai wa mfumo wa Apartheid katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ni kupasishwa sheria ya "Kaumu ya Mayahudi" mwaka jana wa 2018 katika Bunge la Israel. Sheria hiyo ina vifungu 15 na kifungu chake cha kwanza kinajenga uhusiano baina ya Mayahudi wanaoishi katika jiografia ya Palestina na wale wa maeneo mengine ya dunia na kuwatambua kuwa ni taifa moja. Sheria hiyo pia inajaribu kujenga mfungamano wa kiutamaduni na kihistoria baina ya Wayahudi na ardhi ya Palestina ilhali Israel ni dola bandia la vamizi ambalo maazimio ya Shirika la Elimu, Sayandi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) yanasema hakuna uhusiano wowote wa kihistoria, kiutamaduni wala kidini baina ya Mayahudi ardhi ya Palestina.   

Ukuta wa kibaguzi unaotenganisha baina ya makazi ya Wapalestina na walowezi wa Kiyahudi, Ukingo wa Magharibi

Siasa za kibaguzi za Israel zinaendelea kukosolewa sana kote duniani licha ya kukingiwa kifua na madola makubwa ya Magharibi hususan Marekani. Mjukuu wa Mzee Nelson Mandela, Zwelivelile "Mandla" Mandela anasema: Utawala wa Kizayuni wa Israel ni mbaya zaidi kuliko utawala wa ubaguzi wa Apartheid uliokuwa ukitawala Afrika Kusini. Mandla Mandela anasema katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la Guardian la Uingereza kwamba: "Imepita miaka mingi sasa tangu nchi yangu (Afrika Kusini) ilipopata uhuru na kujikomboa kutoka kwenye makucha ya utawala wa wabaguzi waliowachache, lakini hadi sasa dunia haijasalimika na jinai za Apartheid." Zwelivelile Mandela anaendelea kusema kuwa: Kuna mfanano wa kutisha sana baina ya sheria na siasa za kibaguzi za Israel mkabala wa Wapalestina na muundo wa Apartheid huko Afrika Afrika. Anaongeza kuwa: Uamuzi wa hivi karibuni wa Tel Aviv wa kuvunja kijiji cha Khan al Ahmar na kuwafukua wakazi wake ni mfano wa jinai za utawala wa Apartheid wa Israel. Mandla Mandela anasema: Mauaji yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya waandamanaji wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza ni mfano wa mauaji ya Sharpeville yaliyofanywa na polisi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini mwaka 1960 dhidi ya wazalendo weusi wakazi wa eneo hilo.

Zwelivelile "Mandla" Mandela

Ukweli ni kuwa, ingawa dunia ya leo inapinga mifumo ya kisiasa ya kibaguzi na tawala zenye muundo wa Apartheid, lakini swali muhimu linalojitokeza ni kuwa, kwa nini Israel inayoungwa mkono na kusaidiwa na Marekani, inaendeleza siasa hizo za kibaguzi? Je, jamii ya kimataifa haitaki kukabiliana na ubaguzi huo kama ilivyokuwa katika miongo iliyopita?

Tukio la kukomeshwa mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid huko Afrika Kusini tarehe 30 Juni mwaka 1991 huko Afrika Kusini linawahamasisha walimwengu kufanya jitihada zaidi za kuhakikisha mifumo yote ya ubaguzi wa Apartheid mambo leo inafutwa na kutokomezwa kabisa duniani bila la upendeleo wa aina yoyote.                 

Tags

Maoni