Feb 02, 2020 07:47 UTC
  • Fatimatu Zahra katika Suratu Dahr (Insan)

Wanahistoria na wapokezi wa hadithi wameandika kuwa, siku moja Hassan na Hussein wajukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) walipatwa na maradhi wakiwa watoto wadogo.

 وَ یُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلىَ‏ حُبِّهِ مِسْکِینًا وَ یَتِیمًا وَ أَسِیرًا ، إِنمَّا نُطْعِمُکمُ‏ لِوَجْهِ اللَّهِ لَا نُرِیدُ مِنکمُ‏ جَزَاءً وَ لَا شُکُورًا

Mtume (saw) alikwenda nyumbani kwa binti yake, Fatima na mume wake, Ali bin Abi Twalib kwa ajili ya kuwajulia hali wajukuu wake. Baada ya kuwatembelea na kuwaona wajukuu wake alimwambia baba yao, Ali bin Abi Twalib kwamba: Kama ungeweka nadhiri kwa ajili ya kupata shifaa kuna matumaini kwamba, Mwenyezi Mungu SW atawaponya na kuwapa shifaa haraka. 

Imam Ali (as) alisema: Yaa Rasullah! Ninaweka nadhiri ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu ili awape shifaa na kuwaponya. Bibi Fatima (as) na hadimu wake, Fidha pia waliweka nadhiri ya kufunga siku tatu pamoja na Imam Ali (as). Baada ya siku kadhaa maua hayo mawili yenye harufu nzuri ya Mtume (saw), yaani wajukuu wake Hassan na Hussein, walipona na kupata shifaa, na wazazi wao wawili pamoja na hadimu wao, Fidha wakaamua kutekeleza nadhiri yao ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu SW. Siku hiyo, Bibi Fatima alisaga shayiri kwa ajili ya kutayarisha mkate na chakula cha futari. Aliugawa unga huo katika sehemu tatu zitakazotumiwa kupika mkate wa familia kwa ajili ya futari ya siku tatu za swaumu ya kutimiza nadhiri yao.

Siku ya kwanza familia ya Imam Ali na Fatima ilipoketi kwenye kitanga cha chakula kwa ajili ya futari, alibisha hodi mtu maskini na kuomba chakula. Bibi Fatima alimpa chakula chao cha futari. Siku ya pili pia hali ilikuwa hivyo hivyo. Wakati familia ya Bibi Fatima ilipokuwa ikijitayarisha kwa ajili ya futari, aligonga mlango yatima na kuomba chakula. Bibi Fatima alimpa mkate uliotayarishwa kwa ajili ya furari, na familia yake ikafuturu kwa maji. Hali hiyo ilijikariri katika siiku ya tatu ambapo hohehahe alibisha mlango wa nyumba ya Bibi Fatima (as). Alikuwa mateka aliyezongwa na njaa akaamua kwenda nyumbani kwa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatima (as) kuomba chakula. Usiku huo pia Ahlubaiti wa Mtume (saw) walitoa chakula chao cha futari na kumpa mhitaji na wakafuturu kwa maji. Wakati huu ndipo iliporetemshwa Suratu Dahr ikipongeza na kubakisha hai tukio hilo la kujisabilia kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Aya ya 8 mpaka 9 za sura hii zinasema: 

Na huwalisha chakula, licha ya kukipenda, masikini, na yatima, na wafungwa. Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya kupata radhi (wajihi wa) za Mwenyezi Mungu. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani. 

Ukarimu, kujitolea na kutoa kila ukipendacho kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa sifa nzuri na aali ambazo walijipamba nazo mawalii wa Mwenyezi Mungu SW hususan Ahlibaiti wa Mtume (saw). Sifa hii ilidhihirika kikamilifu zaidi katika watu wa nyumba ya Bibi Fatima ya Ali bin Abi Twalib (as) na inaambatana na watufuku hao mara zote majina yao yanapotajwa.

Wanahistoria wanasimulia kwamba: Siku moja Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa ameketi msikitini akizungukwa na masahaba zake. Mzee mmoja aliyekuwa na nguo chakavu na hali ya kusikitisha aliingia msikitini hapo huku akiwa taabani kutokana na uzee na udhaifu wa mwili. Mtume alimwendea na kumjulia hali. Mzee huyo alisema: "Mimi ni masikini dhaifulhali, nina njaa ninaomba chakula, sina mavazi naomba nguo, na ni fukara naomba kutatuliwa shida zangu." Mtume alimwambia: "Kwa sasa sina chochote lakini mwelekezaji katika kheri na mema ni sawa na mtenda wema." Baada ya hapo Mtume alimuelekeza kwenye nyumba ya Bibi Fatimatu Zahra (as).

Mzee huyo alielekea kwenye nyumba ya Bibi Fatima al Zahra iliyokuwa karibu mno na Msikiti wa Mtume (saw) na akamweleza matatizo yake. Bibi Fatima pia alisema: "Sisi pia kwa sasa hatuna chochote hapa nyumbani." Kisha alifungua mkufu aliokuwa amepewa zawadi na binti wa Hamza bin Abdul Muttalib (ra) na akampa mzee huyo maskini kisha akasema: "Uza mkufu huu na inshallah utapata muradi wako."

Mzee fukara alichukua mkufu na akaelekea kwenye msikiti wa Mtume. Mtume (saw) alikuwa bado ameketi na masahaba zake. Mzee fukara alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Bibi Fatima kanipa mkufu huu ili niuuze na kutumia mapato yake katika kukidhi haja na matatizo yangu." Mtume alilia baada ya kusikia maneno hayo. Sahaba Ammar bin Yasir alisema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Unaniruhusu ninunue mkufu huu?" Mtume alisema: "Namuomba Mwenyezi Mungu asimuadhibu mtu yeyote atakayenunua mkufu huu."

Ammar alimuuliza mzee Mwarabu: "Mkufu huo unauuza kiasi gani?" Alisema: "Ninauuza kwa thamani ya chakula cha mkate na nyama kitakachonishibisha, vazi litakalositiri mwili, na dinari moja itakayokuwa masurufu ya kunifikisha nyumbani kwangu." Sahaba mwema wa Mtume, Ammar bin Yasir alisema: "Ninanunua mkufu huu kwa dinari 20 za dhahabu, chakula, nguo na mnyama wa kupanda." Kisha Ammar alimchukua fukara huyo nyumbani kwake na akampa chakula, nguo, mnyama wa kusafiria na dinari 20 za dhahabu. Aliuchukua mkufu huo akautia uturi na akaufunga kwenye kitambaa. Alimwambia hadimu na mtumishi wake: "Mpelekee Mtume wa Mwenyezi Mungu mkufu huu na wewe pia nimekutoa zawadi kwa mtukufu huyo."

Mtume Muhammad (saw) pia aliurejesha mkufu na hadimu yule aliyeachiwa huru na Ammar kwa Bibi Fatima (as). Hadimu alikwenda kwa Bibi Fatima na kumpa mkufu. Bibi Fatima al Zahra alimwambia hadimu yule: "Nimekuachia huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu." Mtumishi huyo alicheka. Bibi Fatima aliuliza sababu na siri ya kicheko hicho. Alijibu: "Ewe Binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Baraka za mkufu huu ndizo zinazonifanya nicheke. Umemshibisha mwenye njaa, ukamvisha mtu asiyekuwa na nguo, umemtajirisha fukara, ukampa kipando mtu ambaye hakuwa nacho na kumuachia huru mtumwa, kisha ukarejea kwa mwenyewe." 

Tunakamilisha kipindi chetu leo kwa hadithi kadhaa zilizopokewa na wanazuonii wa Kiislamu.

Imam Ahmad bin Hanban ambaye ni kiongozi wa madhehebu ya Hanbal amenukuu hadithi kutoka kwa Sahaba Anas bin Malik ambaye alikuwa hadimu na mtumishi wa Mtume Muhammad (saw) akisema: Sijawahi kumuona mtu yeyote aliyefanana zaidi na Mtume (saw) kuliko Hassan bin Ali na Fatima. 

Vilevile Abu Daud katika kitabu cha Sunan, al Hakim al Nishaburi katika Musnadul Hakim, Tirmidhi na hata Bukhari wamenukuu kutoka kwa mke wa Mtume (saw), Bibi Aisha akisema kwamba: "Sijawahi kuona mtu anayefanana na Mtume (saw) katika kusema na kuzungumza kuliko Fatima. Kila alipokuwa anakuja kuonana na baba yake, Mtume alikuwa akisimama mahala alipokuwa ameketi (ili kuonyesha upendo na heshima yake kwa Fatima), akimshika mkono wake na kuubusu na kumkalisha mahala pake. Na mara zote Mtume alipokuwa anakwenda nyumbani kwake, Fatima naye alikuwa akifanya vivyo hivyo." 

Tags

Maoni