Feb 04, 2020 04:44 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kufuata kigezo cha Qur'ani katika kupambana na Uistikbari

Assalamu Alaykum mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Nakukaribisha kutegea sikio mfululizo mwengine wa vipindi maalumu tulivyokuandalia kwa mnasaba wa kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambapo leo tutazungumzia namna mapinduzi hayo yanavyofuata kigezo cha mafundisho ya Qur'ani kwa ajili ya kupambana na Uistikbari duniani. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Nuru ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuangaza, huku ikiwa imepita miongo minne tangu kuchomoza kwake na wakati mapinduzi hayo yakizidi kupiga hatua mbele kuelekea kwenye kilele cha ushindi. Mapinduzi ambayo yameleta mabadiliko makubwa kabisa na ya kina zaidi, ya thamani na fikra katika zama hizi; na jemadari wake mkuu, Imam Khomeini (ma) ameutangaza Uislamu halisi wa asili katika nyuga za kijamii na katika medani ya kupambana na Uistikbari. Leo hii kupambana na Uistikbari na mfumo wa kibeberu limekuwa suala lililoenea katika mataifa yanayotetea uhuru wa kujiamulia mambo yao; na Iran inatambulika kama mbeba bendera wa harakati hiyo. Ni jambo la heshima kwa Iran ya Kiislamu kuona kwamba kadiri umri wa mapinduzi unavyorefuka, ndivyo njama za madola ya kibeberu zinavyozidi kudhihirika huku thamani za kimapinduzi zikiendelea kung’ara na kuwaangazia watu. Hapana shaka kuwa, mapinduzi haya ni chemchemi ya mwamko wa fikra za Kiislamu na yamepata mafanikio mengi katika nyanja tofauti kuanzia ndani, kieneo na kimataifa. Moja ya mafanikio ya mapinduzi hayo ni kuimarika kambi ya muqawama wa Kiislamu katika kukabiliana na Uistikbari wa dunia, mwongozo na dira ya mapambano hayo ikiwa imebainishwa katika mafunzo na mafundisho ya Uislamu. 

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika aya ya 34 ya Suratul-Baqarah:

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِکَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِیسَ أَبَىٰ وَاسْتَکْبَرَ وَکَانَ مِنَ الْکَافِرِینَ

Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akatakabari na akawa katika makafiri.  

Uistikbari ni msamiati wa Qur’ani na wa tendo lililonasibishwa na shetani Iblisi, wakati alipoasi na kukaidi kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu baada ya kuamrishwa amsujudie Adam (as). Kwa mujibu wa aya hiyo ya 34 ya Suratul-Baqarah, shetani Iblisi ni kiumbe wa kwanza aliyetakabari na kujiona bora kuliko mwanadamu; na muhimu zaidi ya hilo alikataa kutii amri ya Mwenyezi Mungu na hivyo kulaaniwa na kuwekwa mbali na rehma za Mola.

Imam Khomeini (ma) jemadari wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitangaza Marekani kuwa ni “Uistikbari wa Dunia” na “Shetani Mkubwa” na chanzo cha masaibu yanayolisibu kila taifa linaloifuata na kuiridhia. Dunia nzima imethibitikiwa kwamba, kufanya urafiki na Marekani hakuna hatima nyingine isipokuwa nakama na idhilali; na kila nchi, zikiwemo hata marafiki wa Marekani hazina imani na nchi hiyo, kwani hulka ya kiistikbari, utumiaji mabavu, unyonyaji, dhulma, kushupalia vita na kutokuwa na muamana iliyonayo Marekani haibadiliki abadani. Ni kwa sababu hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei ameitaja Marekani kuwa ni mfano halisi na wa kila hali wa Uistikbari.

Mtu muistikbari na dola la kiistikbari ni lile linalopenda kuingilia masuala yote ya watu na ya mataifa mengine kwa ajili ya kulinda manaufaa na maslahi yake, lakini lenyewe linajihisi liko huru kufanya litakavyo wala haliwajibiki kwa yeyote. Uistikbari unapoingia katika nchi yoyote ile hutumia kila njia ili kuinakamisha nchi hiyo; yaani hufanya kila uwezalo kuhodhi kila milki ya nchi hiyo kwa manufaa yake.

Lakini mkabala na kambi hiyo dhalimu na kinyonyaji, kuna kambi inayoamua kupambana na Uistikbari, ambayo haikubali katu kupigishwa magoti na kuburuzwa. Kuupiga vita Uistikbari, maana yake ni taifa kutokubali uingiliaji na utezaji nguvu wa mtu muistikbari au dola la kiistikbari; na taifa la Iran linajitangaza kuwa ni mpiga vita Uistikbari, kwa sababu halijawahi katu kuridhia uburuzaji na utumiaji mabavu wa utawala wa Marekani.

Katika aya ya 43 ya Suratu-Faat'ir, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: 

اسْتِکْبَارًا فِی الْأَرْضِ وَمَکْرَ السَّیِّئِ ۚ وَلَا یَحِیقُ الْمَکْرُ السَّیِّئُ إِلَّا بِأَهْلِهِ ۚ فَهَلْ یَنظُرُونَ إِلَّا سُنَّتَ الْأَوَّلِینَ ۚ فَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَبْدِیلًا ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّتِ اللَّـهِ تَحْوِیلًا

Kwa kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya. Hebu hawangojei yalio wasibu watu wa kale? Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.

Katika aya hii, Mwenyezi Mungu Mtukufu amezitaja sababu mbili kuwa ndizo zinazowafanya waliopotoka wajiweke mbali na haki: Kwanza ni kuhitari kufuata njia ya Uistikbari na kutokuwa tayari kamwe kusalimu amri mbele ya haki. Na pili ni kufanya mambo yao kwa kutumia hila chafu na mbaya.

Ili kukabiliana na hulka ya kufurutu mpaka na ya uasi uliyonayo Uistikbari, kuna njia moja tu inayoweza kudhibiti na kuzuia kupindukia kwake mipaka; nayo ni mwamko na irada ya mataifa. Wakati taifa linapoamka, likatambua haki zake, likamjua adui yake, likalielewa lengo lake na hivyo likaamua kusimama imara na kukabiliana naye, kambi ya Uistikbari na Marekani hazitakuwa na uwezo tena wa kufanya lolote, licha ya silaha na zana zote za kijeshi zilizonazo. Na hii ndio nukta ya msingi ambayo Mapinduzi ya Kiislamu yaliiwekea msisitizo tangu awali, na yakauasisi Mfumo wa Kiislamu juu ya msingi huo imara na madhubuti. Katika aya ya 30 ya Suratu-Fussilat, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa ahadi ifuatayo watu wanaosimama imara kukabiliana na madhalimu na waistikbari kwa kutawakali na kumtegemea Yeye: 

إِنَّ الَّذِینَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَیْهِمُ الْمَلَائِکَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِی کُنتُمْ تُوعَدُونَ

Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa. 

Sababu ya mikwaruzano na misuguano inayozuka kati ya Waistikbari na Jamhuri ya Kiislamu ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu inataka Iran iwe ni nchi yenye izza, inayojitawala na kujichukulia maamuzi yake kwa uhuru; na kila inaloamua litokane na rai na matakwa ya watu wake, si ya Waistikbari na watumiaji mabavu. Katika aya ya nane ya Suratu-Saaf, Mwenyezi Mungu anasema: 

یُرِیدُونَ لِیُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَاللَّـهُ مُتِمُّ نُورِهِ وَلَوْ کَرِهَ الْکَافِرُونَ

Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia.

Kwa hiyo inapasa tuwe na imani juu ya ahadi ya Mwenyezi Mungu na kusimama imara, na kama inavyotuusia aya ya 139 ya Suratu-Aal Imran, kwamba tusilegee wala tusihuzunike, kwa sababu kama tutakuwa na imani ya kweli, sisi ndio tutaokuwa wa juu na tutashinda. Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa "Hizbullah" yaani kundi la Allah ndilo litakalokuwa na izza na ndilo litakaloshinda; na "Hizbu-shait'an", yaani kundi la shetani na majeshi yake daima litashindwa na kuharibikiwa. Aya ya 56 ya Suratul-Maidah inasema: 

وَمَن یَتَوَلَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَالَّذِینَ آمَنُوا فَإِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْغَالِبُونَ

Na atakaye fanya urafiki na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kushinda.

Imam Khomeini (ma) ameusia kwa kusema: "Pazeni sauti zenu kadiri muwezavyo dhidi ya Marekani". Leo hii Jamhuri ya Kiislamu inapaza sauti yake kwa uwazi kabisa dhidi ya dhulma, dhidi ya ubeberu, dhidi ya unyonyaji na dhidi ya Uistikbari bila kuchelea chochote, pasi na kumhofu adui wala kuogopa vitisho vyake; na hatua yake hiyo inayaathiri mataifa mengine. Kwa kufuata kigezo na muongozo wa mafunzo na mafundisho ya Qur'ani, taifa la Iran limekuwa kila mara likitilia mkazo ulazima wa kulinda izza na kujitawala kwa nchi na katu halijawahi kuridhia batili iwe juu ya haki. Ni kama ilivyoeleza Qur'ani Tukufu katika aya ya 81 ya Suratu-Israa ya kwamba: Haki ni yenye kushinda na batili ni yenye kutoweka tu. Siri ya Mitume na waumini kuwa na izza, heshima na utukufu ni kumuelekea na kumtegemea kwao Mwenyezi Mungu na kuomba izza na utukufu kwake Yeye tu.

Kupambana na Uistikbari ni jambo lisilo na mwisho na linaloendelea daima, kwa sababu maadamu batili ipo, haki itasimama kukabiliana nayo tu. Na kwa sababu hiyo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei anasema: "Kama hatutapambana na Uistikbari, hatuwi asilani wenye kuifuata Qur'ani." Jamii ya Iran, ambayo leo hii inatazamwa kama kigezo cha kuigwa na mataifa yanayotetea uhuru wa kujitawala bali na ulimwengu mzima, kutokana na kuwa mfano uliofanikiwa wa kupiga vita Uistikbari, inahitajia hivi sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma, kumtegemea zaidi Mwenyezi Mungu Mwenye hekima na kufuata mafunzo na mafundisho ya Qur'ani pamoja na miongozo ya hekima ya kiongozi wake na kupambana na kila aina ya Uistikbari na dhulma na kujibari na Waistikbari. Ni wazi kuwa, kulinda izza, nguvu na moyo wa kujiamini katika jamii ni mambo ya dharura na ya lazima kwa ajili ya kupambana na Uistikbari. Kwa kufanya hivyo, hatua anazopiga mtu zitakuwa imara na thabiti na kumwezesha kushuhudia kwa haraka zaidi ladha tamu ya ushindi dhidi ya dhulma na Uistikbari wa dunia. Mpenzi msikilizaji, kipindi hiki maalumu cha maadhimisho ya Alfajiri Kumi kimefikia tamati. Ahsante kwa kunisikiliza…/

 

 

Tags

Maoni