Feb 10, 2020 08:42 UTC
  • Kilele cha maadhimisho ya miaka 41 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Assalamu Alaykum mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Nakukaribisha kutegea sikio mfululizo huu wa vipindi maalumu tulivyokuandalia kwa mnasaba wa kuadhimisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Kipindi chetu cha leo kinakujia sambamba na kuwadia kilele cha maadhimisho ya miaka 41 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, hivyo mbali na kutoa mkono wa pongezi kwa maadhimisho ya siku Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi mnamo Bahman 22, 1357, nakuomba uendelee kuwa nami kuanzia awali hadi tamati ya mazungumzo yetu kusikiliza niliyokuandalia kwa mnasaba huo. 

Tarehe 11 Februari mwaka 1979, ni siku muhimu na ya mabadiliko makubwa katika kalenda ya historia ya matukio ya dunia. Siku hiyo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yaliyoongozwa na Imam Khomeini, alimu wa dini mpambanaji na mwanajihadi, yalipata ushindi. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamesajiliwa kwenye kalenda ya matukio muhimu na makubwa ya dunia, kwa sababu taathira za mapinduzi hayo hazikukomea katika kuanguka utawala dhalimu tu na wa kidikteta wa kifalme. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran uliliathiri eneo lote la Asia Magharibi na ulimwengu kwa ujumla. Na ndiyo maana Mapinduzi ya Kiislamu yanajadiliwa na kuwekwa kwenye orodha ya mapinduzi makubwa yaliyojiri duniani. Athari za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika upeo wa kimataifa zilikuwa na umuhimu mkubwa sawa na wa kuangushwa utawala wa kiimla wa ufalme uliodumu kwa miaka 2500 ndani ya Iran. Kwa hakika kama ambavyo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ilikuwa harakati ya kisiasa na kijamii ya kupambana na udikteta, ilikuwa na ingali pia ni harakati ya kupiga vita ukoloni; na ni kwa sababu hiyo, baada ya kupita miaka 41 ingali inaendelea kufanya hivyo kwa kupambana na madola ya kibeberu na yanayoonyesha ubabe. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi wakati kila tukio la kisiasa na kimapinduzi lililojiri duniani katika zama hizo lilikuwa tegemezi kwa harakati mbili za Demokrasia ya Kiliberali na Umaksi. Lakini harakati ya Imam Khomeini, ambayo tangu ilipoanza mwaka 1963 haikuwa tegemezi kwa fikra za Mashariki wala Magharibi, iliweza kupata ushindi katika kupambana na madola ya kibeberu kwa kutegemea mafundisho matukufu ya Uislamu.

Ikumbukwe kuwa katikati ya muongo wa 1970 katika enzi za mfumo wa kambi mbili kuu duniani za Mashariki na Magharibi, Iran ya utawala wa Pahlavi wa Pili, yaani Mohammad Reza Shah ilionekana kama kisiwa cha amani na uthabiti. Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani Magharibi hadi kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi hizo, uliofanyika tarehe 4 hadi 7 Januari 1979 katika kisiwa cha Guadeloupe, zilikuwa zingali na matarajio kuwa utawala wa kifalme nchini Iran hautaanguka. Januari mwaka 1978, mwaka mmoja kabla ya kuangushwa utawala wa Kipahlavi, wakati rais wa wakati huo wa Marekani Jimmy Carter alipotembelea Iran, alimsifu Shah akisema ni kipenzi cha wananchi na akaitaja Iran kuwa ni kisiwa cha amani na uthabiti. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza wakati huo David Owen, yeye alitoa taarifa maalumu akitangaza waziwazi msimamo wa nchi yake wa kuuunga mkono utawala wa Mohammad Reza Pahlavi katika kuamiliana na harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran. Wote hao walihalalisha uungaji mkono wao huo kwa kisingizio cha kukabiliana na Wakomunisti. Hata hivyo mwenendo wa mabadiliko ya kijamii yaliyojiri kuanzia Januari 1978 hadi Februari 11, 1979 ulionyesha ni jinsi gani waungaji mkono wa utawala wa kiimla wa Shah walivyokuwa na uono mdogo na uelewa finyu kuhusu masuala ya Iran.

Uungaji mkono wa madola ya Magharibi yanayojigamba kuwa watetezi wa uhuru na demokrasia kwa utawala wa kidikteta wa Shah, ulichangia sana kumtia mori na kumhamasisha mtawala huyo ashadidishe ukandamizaji dhidi ya maandamano ya upinzani ya wananchi. Gholamreza Nejati, mmoja wa waandishi watajika wa historia ya zama hizi ya Iran ameandika yafuatayo kuhusiana na nukta hiyo: "Hotuba ya kusifia aliyotoa Jimmy Carter usiku wa tarehe mosi Januari 1978 katika kasri la Niyavaran, vilimpa nguvu Mohammad Reza Shah na kumfanya azidi kujiamini. Uungaji mkono usio na masharti wa Marekani ulimfanya adhani kwamba ataweza kuendeleza sera ya mbinyo na ukandamizaji na kuwatupa nje ya ulingo viongozi wa upinzani, hasa Ayatullah Khomeini ambaye alikuwa angali anaendeleza harakati dhidi ya utawala kutokea Najaf." Katika kuuhakiki kiukosoaji uungaji mkono wa Jimmy Carter kwa utawala wa kifalme wa Iran, Gholamreza Nejati anasema: "Hotuba aliyotoa rais wa Marekani Januari 1978 ya kumpamba na kumsifu Shah, ambaye mikono yake ilikuwa imetapakaa damu za maelfu ya Wairani... inadhihirisha ukweli kwamba kaulimbiu za 'haki za binadamu, uhuru na demokrasia' ni nyenzo za mashinikizo tu dhidi ya jamii zenye misimamo huru na zinazopinga ubeberu wa Marekani; na hasa ilipofika hadi ya Carter kusema: "hakuna kiongozi yeyote duniani ninayempa heshima kubwa zaidi na niliye na uhusiano naye wa kirafiki zaidi kuliko Shah."

Miaka 25 kabla ya kupinduliwa Mohammad Reza Shah, Marekani iliandaa mapinduzi ya kijeshi mnamo mwaka 1953 dhidi ya serikali halali ya Dakta Mohammad Mosaddeq na kumrejesha Shah nchini Iran; na kwa muda wa miaka 25 ikauunga mkono kwa kila hali utawala wake wa kifalme dhidi ya harakati za upinzani wa wananchi. Kuanzishwa shirika la intelijensia na usalama, lililojulikana kama SAVAK, ambalo lilikuwa moja ya mashirika katili, ya kuogofya na ya kutisha ya ujasusi duniani, kwa ajili ya kukandamiza na kuzima upinzani wa aina yoyote dhidi ya utawala wa Shah, kulifanyika katika kipindi hicho. Kwa sababu hiyo, Imam Khomeini alianzisha harakati yake ya kukabiliana na Shah sambamba na kupambana na dola la kikoloni la Marekani na utawala bandia wa Israel. Na sababu ni kuwa, utawala wa Mohammad Reza Pahlavi ulikuwa na mafungamano ya kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiintelijensia na utawala haramu wa Kizayuni. Ukweli ni kwamba mapambano na kusimama kidete wananchi wa Iran katika kukabiliana na uadui wa Marekani na Uzayuni dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa muda wote wa miaka 40 iliyopita, chimbuko lake limeanzia kwenye historia ya mapambano ya wananchi kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa kipindi cha miaka 41 iliyopita, sera kuu ya Marekani kuhusiana na Iran ni ya kuung'oa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini. Katika muda wote wa miongo minne ya umri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Marekani haijasita kuwafanyia kila aina ya uadui wananchi wa Iran. Kuashiria moja tu miongoni mwa hatua kubwa zaidi za kiuadui ilikuwa ni kumchochea dikteta wa Iraq Saddam Hussein, aivamie kijeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mwaka 1980, ikiwa imepita miezi 19 tu tangu Mapinduzi ya Kiislamu yapate ushindi. Na hatua ya karibuni zaidi ya Marekani ni ya kuiwekea vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi kuwahi kushuhudiwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata hivyo wananchi wa Iran wamehitari kuwa ngangari na kusimama imara kuzikabili hatua za kiuadui za Marekani; na kwa kufanya hivyo wameweza kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kijeshi.

Muqawama wa wananchi wa Iran wa kuukabili utumiaji mabavu wa Marekani na Wazayuni haukomei ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kupitia mhimili wa kambi ya muqawama, leo hii Iran inazichachafya sera za kibeberu za Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo la Asia Magharibi. Miaka 40 nyuma, wananchi wa Iran waliwatimua washauri elfu 40 wa Marekani waliokuweko hapa nchini. Hivi sasa matakwa ya wananchi wa eneo hili ni kuondoka Marekani katika nchi zao na kufungwa vituo vyake vya kijeshi. Tarehe 11 Februari ambayo ni ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, inasadifiana na Arubaini ya siku walipouliwa kigaidi Abu Mahdi Al-Muhandis, kamanda wa Al Hashdu-Shaabi ya Iraq na Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds na jemadari mkuu wa muqawama na mapambano dhidi ya ugaidi na vuguvugu la ukufurishaji. Trump aliwaita kamanda Soleiamni na Al Muhandis magaidi, lakini wakati mataifa ya Iran na Iraq yalipowaaga na kuwasindikiza mashahidi hao na wanamuqawama wenzao kwa umati mkubwa wa watu nadra kuwahi kushuhudiwa, yaliidhihirishia dunia ni nani hasa gaidi na nani hasa wanaoendesha mapambano ya kweli dhidi ya magaidi. Si hayo tu, lakini wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipotoa jibu kwa jinai hiyo iliyofanywa na Marekani kwa kuishambulia kwa makombora kambi ya utawala huo wa kigaidi ya Ainul-Assad nchini Iraq, ilithibitisha kuwa taifa kubwa la Iran haliyumbishwi wala halitetereshwi na makeke ya Marekani.  Hii ni kwa sababu tangu baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, hakuna nchi yoyote duniani iliyothubutu kushambulia kituo chochote cha kijeshi cha Marekani kikiwa na mamia ya askari wa nchi hiyo ndani yake. Kwa kujitokeza na kushiriki kwa wingi katika maandamano ya mwaka huu ya kuadhimisha miaka 41 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wa Iran wanawathibitishia walimwengu kwa mra nyingine kuwa, wangali wameshikamana barabara na malengo matukufu ya jemadari wa mapinduzi hayo, Imam Khomeini chini ya uongozi wa Ayatullah Khamenei. Na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na juhudi za vijana wake hodari na wenye moyo wa uchapaji kazi, taifa la Iran litapiga hatua za maendeleo katika nyuga zote, licha ya mbinyo wa kiuchumi liliowekewa na utawala wa kibeberu wa Marekani na litaendelea kuwa kigezo na mfano wa kuigwa na jamii zote zenye fikra huru duniani.../    

 

 

Tags

Maoni