Feb 12, 2020 12:02 UTC
  • Mgogoro wa virusi vya Corona Duniani

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika kipindi cha Makala ya Wiki ambacho leo kitatupia jicho mgogoro uliosababishwa na virusi vya Corona ambavyo vinaendelea kuua watu na kusambaa katika nchi mbalimbali duniani. Ni matarajio yangu kwamba ntakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Miongoni mwa changamoto kubwa zinazolikabili Shirika la Afya Duniani (WHO) na serikali ya China ambayo pia imezusha wasiwasi mkubwa sana katika nchi nyingine ni maambukizi ya virusi vya Corona na ongezeko la watu waliopatwa na virusi hivyo. Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na seriali ya China zinasema kuwa, tangu mwezi Septemba mwaka jana wakati virusi hivyo vilipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini humo zaidi ya watu 44 elfu wameambukizwa na zaidi ya 1,100 wameaga dunia kutokana na virusi vya Corona. 

Mbali na China, watu wengine zaidi ya 180 wameambukizwa virusi vya Corona katika nchi nyingine duniani. Shirika la Afya Duniani limetahadharisha kuwa, hatari ya kusambaa zaidi virusi hivyo ni kubwa na kwamba nchi  zote zinapaswa kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana navyo. Hapa linajitokeza swali kwamba, ni nini virusi vya Corona na vina hatari gani kwa wanadamu? Na je, ni zipi njia za kukabiliana navyo?

Virusi vya Corona ni sehemu ya familia kubwa ya virusi vinavyosababisha mafua ya kawaida hadi mafua makali sana kama ya SARS na MERS. Virusi vya Corona viligunduliwa mwaka 1960 na hadi sasa kumejulikana aina saba ya virusi hivyo. Aina ya hivi karibuni kabisa ni ile iliyogunduliwa Disemba mwaka jana wa 2019 na kuwambukiza watu wengi katika mji wa Wuhan nchini China. Wataalamu wanasema kuwa, japokuwa aghlabu virusi vya Corona vinaonekana zaidi baina ya wanyama, lakini aina 5 za virusi hivyo zinaathiri mfumo wa kupumua wa mwili wa mwanadamu. Dalili za ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona ni pamja na homa na matatizo ya kupumua kama kubanwa na pumzi, kuhema na kupumua kwa kasi kubwa, maumivu ya koo na kutokwa na mafua ya majimaji. Ingawa watu wa kwanza kupatwa na virusi hivyo ni wale waliokuwa wakifanya kazi katika soko la vyakula vya baharini lakini baada ya virusi hivyo kusambaa zaidi baina ya watu ambao hawakuwa na mawasiliano yoyote na wanyama, Shirika la Afya Duniani (WHO) limefikia natija kwamba, maambukizi ya virusi hivyo baina ya wanadamu pia yamefikia kiwango cha kupewa mazingatio. 

Utafiti mpya uliofanywa na wasomi na wataalamu umeonesha kuwa, kuna uwezekano kwamba virusi vya Corona vimehamia kwa wanadamu kutoka kwa wanyama. Matokeo ya uchunguzi huo ambayo yamechapishwa kwenye jarida la Journal of Medical Virology yanaonesha kuwa, virusi vipya vya Corona vilianza kuzagaa kutokana na nyoka. Wasomi hao wanasema mabadiliko yaliyotokea kwenye mojawapo ya proteini za virusi vipya vya Corona yamewezesha kuhama virusi hivyo kutoka kwa wanyana na kumpata mwanadamu. Inatupasa kusema hapa kuwa, hili si jambo jipya kwani katika kipindi cha miaka 50 iliyopita idadi kadhaa ya magonjwa ya kuambukiza yamehama kutoka kwa wanyama na kumpata mwanadamu baada ya kupitia awali kadhaa za kukamilika kwa magonjwa hayo. Virusi vya HIV (AIDS) katika muongo wa 1980, mambukizi ya virusi vya homa ya mafua ya ndege baina ya mwaka 2004 na 2007 na baadaye homa ya mafua ya nguruwe na kisha ugonjwa wa Ebola, na katika miaka ya karibuni virusi vya SARS, MERS na Corona ni baadhi ya magonjwa yaliyohamia kwa mwanadamu kutokana na wanyamapori.

Maambukizi ya kwanza ya kirusi cha Corona kinachofanana sana na ugonjwa wa homa ya mapafu (Pneumonia) yaliripotiwa tarehe 31 Disemba mwaka jana nchini China. Tangu wakati huo virusi hivyo vimesambaa zaidi na kuripotiwa katika nchi kadhaa ikiwemo Japan, Thailand, Marekani, Uingereza, Australia, Korea Kusini na Ufaransa. Takwimu zinaonesha kuwa, aghlabu ya wahanga wa maradhi yaliyosababishwa na kirusi hicho walikuwa na umri wa zaidi ya miaka 60. Hata hivyo vifo vya vijana kadhaa vilivyosababishwa na kirusi hicho akiwemo Daktari wa macho, Li Wenliang (34) aliyekuwa wa kwanza kutoa tahadhari kwa madaktari wenzake kuhusu mambukizi ya kirusi kinachoshabihiana na SARS, vimezusha wasiwasi mkubwa kuhusiana na virusi vya Corona. 

Daktari Li Wenliang (34) alikuwa wa kwanza kutoa tahadhari kwa madaktari wenzake kuhusu mambukizi ya kirusi kinachoshabihiana na SARS

Hivi sasa na licha ya kuwa, imethibitishwa kwamba virusi vya Corona vimewapata watu katika zaidi ya nchi 23 duniani lakini Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Magonjwa ya Kuambukiza cha Shirika la Afya Duniani, Dr. Sylvie Briand anasema: Kwa sasa hatujaingia katika kipindi cha maambukizi ya dunia nzima. Tumo katika awamu ya maambukizi ya maeneo kadhaa na tufanya jitihada za kusimamisha maambukizi ya virusi hivi katika maeneo mengine".

Katika uwanja huo serikali ya China imepongezwa sana na jumuiya za kimataifa na nchi mbalimbali kwa jitihada zake kubwa za kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya Corona katika maeneo mengine ya dunia. Kwa mfano tu katika mji wenye jamii ya watu milioni 9 wa Wuhan ambako ndiko kulikoripotiwa maambukizi ya kwanza kabisa ya virusi vya Corona nchini China, kumechukuliwa hatua maalumu za kuzuia maambukizi zaidi ya virusi hivyo. Viwanja vya ndege na vituo vya treni vimefungwa kwa ajili ya watu wanaotaka kusafiri na kwenda nje ya mji huo, na zimewekwa sheria na kanuni maalumu kwa wakazi wa mji huo kwa ajili ya usafiri wa mabasi, metro na vyombo vingine vya usafiri wa umma ndani ya mji huo. Vilevile wakazi wa mji wa Wuhan wametakiwa wajiepushe kufanya mijumuiko na mukusanyiko ya watu wengi. Ujenzi wa hospitali maalumu yenye vitanda elfu moja katika mji huo wa Wuhan katika kipindi kifupi sana cha siku kumi tu ni miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na serikali ya China kwa ajili ya kukabiliana na kasi ya maambukizi ya virusi hatari vya Corona. Majmui ya hatua kama hizi zimekuwa sababu ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kusifu jitihada kubwa za serikali ya China na kusema: "Ni hatua madhubuti sana zitakazosaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona katika upeo wa kimataifa."

Vilevile katika kikao cha 46 cha Kamati ya Utendaji ya WHO kilichofanyika tarehe 3 Februari mjini Geneva, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la Afya Duniani, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus alitangaza uungaji mkono kamili wa shirika hilo kwa serikali ya China katika mapambano yake dhidi ya virusi vya Corona. Ghebreyesus amesema: China imechukua stratijia madhubuti na yenye taathira. Nje ya China kumeripotiwa kesi 146 za maambukizi ya virusi vya Corona katika nchi zisizopungua 23 na kiwango hicho kinahesabiwa kuwa cha chini sana ikilinganishwa na maambukizi ya magonjwa mengine, hivyo hakuna sababu ya kuwa na woga na wahka.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Dakta Muhammad Javad Zarif amefanya mazungumzo na mwenzake wa China, Wang Yi akiipongeza serikali ya Beijing kwa hatua zake zenye mafanikio katika kupambana na ugonjwa hatari wa virusi vya Corona. Zarif amesema: "China imeweza si tu kuzuia kujitokeza hali mbaya zaidi ndani ya nchi bali pia imefanikiwa kuzuia maambukizi zaidi duniani." Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameikosoa Marekani kutokana na misimamo yake kuhusu mgogoro wa virusi vya Corona nchini China na kuuandika katika mtandao wa Twitter kwamba: Tehran inalaani hatua ya serikali ya Washington ya kutumia vibaya hatari hiyo. Hapana shaka kuwa, China iliwajibika na kufanikiwa zaidi katika kuzuia na kudhibiti homa ya mafua ya H1N1 hapo mwaka 2009 ikilinganishwa na Marekani."

Muhammad Javad Zarif

Itakumbukwa kuwa, Waziri wa Biashara nchini Marekani, Wilbur Ross amesema kwamba mripuko wa virusi vya Corona nchini China unaweza kuinua uchumi wa Marekani. Waziri huo wa serikali ya Trump aslisema: Virusi hivyo vitasaidia kurudisha ajira kaskazini mwa Marekani."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Hua Chunying amekosoa msimamo huo wa Marekani akisema imekuwa ikieneza anga ya hofu na wasiwasi tangu virusi vya Corona vilipolipuka nchini humo na kuongeza kuwa, Washington haijatoa msaada wowote katika uwanja huo.

Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya China imelishukuru serikali na taifa la Iran kwa kushirikiana na Beijing katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona. Msemaji wa Wizara hiyo, Hua Chunying amewaambia waandishi habari kwamba: Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Muhammad Javad Zarif alikuwa waziri wa mambo ya nje wa kwanza kati ya nchi zote duniani aliyeunga mkono juhudi za China za kukabiliana na virusi vya Corona. Vilevile ameipongea Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia msaada wa maski na barakoa milioni tatu za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona. Kitendo hiki cha Jamhuri ya Kiislamu kinaakisi hadithi ya Mtume Muhammad (saw) aliyewafananisha wanadamu wote na mwili mmoja ambao pale kiungo chake kimoja kinapopatwa na maumivu, viungo vingine vya mwili pia huumia na kupatwa na maumivu.           

Tags

Maoni