Feb 25, 2020 08:46 UTC
  • Katika Mwangwi wa Fikra za Imam Baqir (AS), kwa Mnasaba wa Kuzaliwa Mtukufu Huyo

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Siku ya mwanzo ya mwezi wa Rajab, mwezi mtukufu wa Mwenyezi Mungu, ambao ameufanya wasila na wenzo wa kumuunganisha mja na Yeye Mola Muunmba imesadifiana na imezidishiwa baraka zake kwa kuzaliwa Ahlul-Bayt mwingine wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

Mwaka 57 baada ya hijra ya Bwana Mtume SAW ya kuhama Makka na kuhamia Madina, siku ya kwanza ya mwezi wenye fadhila kubwa wa Rajab, ilipambazuka kwa kuzaliwa nuru. Katika siku hii yenye baraka, alizaliwa mwana katika ukoo wa Mtume Muhammad SAW; na sawa na Ahlul Bayt wengine wa mtukufu huyo, akawa ni nguzo kati ya nguzo imara na madhubuti katika historia ya Uislamu. Yeye ni mwana wa Imam Sajjad AS na ni maarufu kwa jina la Baqir.

Lakabu ya Baqir ina maana ya mwenye kunawirisha. Mtukufu huyo alitajwa kuwa mtu aliyechanua na kunawirisha elimu. Alikuwa stadi katika elimu mbali mbali na alitajwa kuwa bahari ya elimu. Tunachukua fursa hii kutoa mkono wa pongezi, kheri na baraka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Muhammad Baqir AS.

Baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Sajjad AS, Imam Baqir AS alichukua jukumu muhimu la uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 19. Kipindi hicho kiliandamana na matukio ya kisiasa na kuhamishwa utawala kutoka mikononi mwa ukoo wa Bani Umayya na kuingia mikononi mwa ukoo wa Bani Abbas. Katika kipindi hicho, Imam alitumia nafasi yake kueneza ukweli kuhusu elimu na utamaduni wa Kiislamu. Imam Baqir AS alianzisha harakati ya kiutamaduni na kielimu katika ulimwengu wa Kiislamu na natija ya juhudi zake ilionekana katika zama zilizofuatia. Imam Baqir alifanya kazi kubwa sana katika masuala ya elimu na utamaduni ili kuweza kukabiliana kikamilifu na imani batili na potofu katika jamii. Aidha alianzisha chuo kikubwa cha elimu na utamaduni ili kueneza mafundisho matukufu na a'ali ya Bwana Mtume SAW na Watu wa Nyumba yake.

Sheikh Tousi, mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu amewataja wanafunzi waliobobea wa Imam Baqir AS kuwa ni watu 462. Vigogo na shakhsia wakubwa wa kisiasa wa zama hizo, wote walihudhuria darsa za Imam Baqir AS ili kupata angalau tone moja la bahari yake pana na ya kina ya elimu. Watu kama Jabir bin Yazid Jofi, Zohri, Abu Hanifa, Anas ibn Malik na Shafi ni miongoni mwa wanazuoni walionufaika na hazina kubwa ya elimu ya Imam Baqir AS. Muhammad Ibn Talha Shafi'i katika kuelezea sifa za Imam Baqir ameandika yafuatayo: "Alikuwa mwenye kunawirisha elimu. Hotuba zake zilikuwa fupi lakini zilizojaa maana na moyo wake ulijaa mwanga. Alipambika kwa amali njema. Alikuwa na akhlaqi njema na alitumia umri wake katika kutii amri za Mwenyezi Mungu. Alikuwa amejikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na alistahiki uongozi."

Uimamu wa Imam Muhammad Baqir AS ulianza katika kipindi ambacho, Umma wa Kiislamu ulikuwa unakabiliwa na changamoto za kina za kiitikadi na kifiqhi baina ya matapo mbali mbali ya Kiislamu. Kuwepo Imam Baqir AS katika mazingira hayo kulipelekea kuchukuliwa hatua muafaka katika kubainisha mitazamo ya Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW. Katika kipindi cha muda mfupi, Imam aliweza kuzivunja kwa hoja na kwa kiwango kikubwa itikadi za makundi potofu. Katika zama za Uimamu wake na za mwanawe mteule Imam Sadiq AS, hitilafu na mivutano katika utawala wa kisiasa zilifika kileleni na hali ya kisiasa na kijamii haikuweza kuwa na uthabiti. Matokeo yake yalikuwa ni Makhalifa kubadilishwa kwa kasi, kiasi kwamba makhalifa watano walitawala katika kipindi cha Uimamu wa Imam Baqir AS. Kwa hivyo hali hiyo ilitoa fursa adhimu kwa Imam ya kujiweka mbali na mashinikizo ya kisiasa ya watawala na kuwavuta karibu naye wanazuoni wakubwa pamoja na wasomi bingwa wa elimu na hekima. Wanazuoni waliokuwa karibu na Imam waliweza kunufaika kwa njia ya moja kwa moja na mafundisho yake ya Kiislamu aliyokuwa akiyabainisha kwa lugha fasaha.

Katika kipindi cha Imam Baqir AS, hujuma ya kiutamaduni iliyokuwa imeratibiwa na Bani Umayyah ililenga kuvuruga itikadi za kidini za Umma wa Kiislamu. Aidha katika kipindi hicho, jamii ya Kiislamu ilishuhudia kuibuka nadharia zisizo sahihi za kifalsafa kuhusu misingi ya itikadi. Kwa sababu hiyo, baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu walichanganyikiwa katika jitihada zao za kuutafuta ukweli. Kwa kutumia hoja pambanuzi na za kimantiki, Imam Baqir AS alizichambua fikra hizo potofu za kifalsafa na kuweza kubainisha nukta pofotu zilizomo kwenye nadharia hizo mpya. Mtukufu huyo aliwaweka kitimoto wanafalsafa wa Kilahidi na kuweza kubainisha mitazamo ya itikadi sahihi za Kiislamu. Kutokana na mazingira hayo, elimu ya misingi ya itikadi, yaani ilmul-kalam iliweza kuvuma katika zama za Imam Baqir AS.

Imam Baqir AS alikuwa pamoja na watu na alichanganyika nao muda wote. Licha ya utukufu na adhama aliyokuwa nayo, Imam huyo mteule alikuwa akiwahudumia watu wa tabaka la wanyonge na waliotengwa katika jamii. Alikuwa akiketi na watu waliosahaulika kabisa, kuzungumza nao na kutatua matatizo yao. Muamala uliojaa ukarimu na unyenyekevu wa mtukufu huyo ulipelekea watu wengi kumfuata. Imam Baqir AS hakumrejesha mikono mitupu yeyote aliyekwenda kumuomba msaada na aliwasisitizia watu umuhimu wa kuwasaidia na kuwaheshimu wahitaji. Kutokana na muamala wake mwema ulioambatana na adabu na mapenzi, Imam Baqir AS aliweza kuwaathiri na kuwavutia hata wapinzani wake. Katika historia tunasoma kuwa mtu mmoja kutoka Sham ambaye hakuafikiana kiitikadi na Imam Baqir AS alikuwa akifika katika darsa za mtukufu huyo na kuchota mengi kwenye bahari hiyo ya elimu. Mtu huyo alisema, sababu ya maingiliano yake mazuri na Imam Baqir AS ni akhlaqi njema na muamala wake mzuri. Alikuwa akimwambia hivi mtukufu huyo: "Wewe unabainisha masuala kwa ufasaha na uwazi. Unatumia maneno mazuri katika kauli zako. Ni kwa sababu hii ndio napata furaha ya kushiriki kwenye darsa zako."

Pamoja na shughuli zake nyingi za kielimu na kiutamaduni, Imam Baqir AS hakughafilika na masuala ya kisiasa na alikuwa akiwakosoa sana watawala wa kiimla na madhalimu wa zama zake. Katika harakati zake za kuwazindua Waislamu kisiasa, Imam alibainisha sifa za viongozi wema ili watu waweze kuwatia kwenye mizani watawala na kufahamu udhaifu na upotofu wao.

Imam Baqir anasema: "Uongozi wa jamii unamstahiki mtu mwenye sifa tatu. Kwanza ni ucha Mungu ili takwa iweze kumkinga na mitihani ya madaraka kama vile kutumbukia katika mtego wa ufisadi. Pili awe mstahamilivu ili aweze kuzuia hasira zake. Tatu aamiliane na watu anaowatawala kama baba mkarimu na awe na tabia nzuri".

Wapenzi wasikilizaji kwa mara nyingine tunatoa mkono wa pongezi, kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Baqir AS na tunahitimisha kipindi chetu hiki maalumu kwa hadithi ya mtukufu huyo isemayo: "Tabasamu la mtu kwa ndugu yake muumini ni jambo lenye kupendeza mno; na kuondoa ukungu wa majonzi katika uso wake ni tendo jema, na hajaabudiwa Mwenyezi Mungu kwa kitu bora zaidi kuliko kuufurahisha moyo wa muumini." Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Maoni