Mar 28, 2020 08:09 UTC
  • Virusi vya Corona na jinsi ya kukabiliana navyo

Mwezi Disemba mwaka uliopita wa 2019 kuliripotiwa aina ya ugonjwa mkali wa matatizo ya kupumua katika mji wa Wuhan nchini China.

Awali ilionekana kuwa, baadhi ya wagonjwa wamepatwa na matatizo hayo ya kiafya kutokana na kwenda kwenye soko la samaki la mji wa Wuhan. Kwa msingi huo soko hilo lilifungwa haraka hapo tarehe Mosi Januari na zikachukuliwa hatua za dharura za kuanza kusafisha eneo hilo. Siku kadhaa baadaye ilibainika kuwa, tatizo hilo la kiafya lililojitokeza katika mji wa Wuhan halitokani na aina ya virusi mashuhuri kama SARS, MERS, mafua ya ndege na kadhalika. Tarehe 9 Januari mwaka huu wa 2020 madaktari wa nchi hiyo waligundua kwamba matatizo hayo ya kupumua yanasababishwa na kirusi kipya ambacho tayari kilikuwa kimewakumba watu 15 kati ya 59 waliokuwa wamelazwa hospitalini. Ugunduzi huo ulisabababisha wasiwasi mkubwa. Kirusi hicho kilikuwa aina mpya ya virusi vya Corona ambacho, kijeni, kinakaribiana kwa asilimia 70 na kirusi cha SARS na ni katika jamii ya virusi vya "Sarbecovirus". Kwa sasa virusi hivyo vimepewa jina la COVID-2019.

Tarehe 11 Januari mwaka huu kuliripotiwa kifo cha kwanza cha mtu aliyeaga dunia kutokana na kirusi cha Corona nchini China. Habari hiyo ilifuatiwa na ripoti za kuenea virusi hivyo katika nchi kama Japan, Thailand, Korea Kusini na Marekani. Kuzagaa haraka virusi hivyo baina ya madaktari na wahudumu wa afya kulitatiza sana juhudi za kukabiliana na janga hilo jipya. Mbinu zinazotumiwa sasa kugundua na kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo inashabihiana sana na ile ya kukabiliana na virusi vya MERS. Virusi hivi vipya vinaweza kuambukizwa kutoka kwa mnyama kwenda kwa mwanadamu lakini hadi sasa haijajulikana vyema jinsi kinavyoambukizwa, njia haswa za kuzuia maambukizi yake na masuala mengine mengi yanayohusiana na kirusi hicho. 

Dalili za Corona:

Ugonjwa wa virusi vya Corona ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na kirusi kipya ambacho awali hakikutambuliwa kuwa baina ya binadamu. Virusi hivi vinasababisha matatizo ya kupumua kama yale ya virusi vya homa ya mafua (influenza) na huwa na dalili kama kukohoa, homa, na wakati mwingine nimonia au kichomi (Pneumonia). Dalili kuu za virusi vya Corona ni kama kutokwa na makamasi, matatizo ya figo, kukohowa na homa. Kwa baadhi ya watu, virusi hivi yumkini vikawa shadidi zaidi na kusababisha matatizo katika mfumo wa kupumua. Baadhi ya kesi nadra za virusi hivi husababisha kifo. 

Wazee, watu wanaosumbuliwa na maradhi kama ya pumu, kisukari na matatizo ya moyo yumkini wakadhuriwa zaidi na virusi hivi. Kwa sasa hakuna kinga ya kuzuia virusi vya Corona, lakini inawezekana kupunguza hatari ya kupatwa na virusi hivyo kwa kufuata taratibu na maagizo ya wataalamu wa afya kama vile kuosha mikono kwa maji na sabuni mara kwa mara, kujipaka spiriti (alcohol), kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kuhakikisha unakuwa mbali na watu wenye dalili za mafua au influenza kwa mita moja na zaidi au futi tatu. 

Tiba ya Corona:

Ugonjwa huo hauna tiba maalumu, na pale mgonjwa anaposumbuliwa na matatizo ya kupumua hupelekwa hospitalini na kuwekwa chini ya uangalizi wa madaktari. 

Mtu anayekuwa na dalili hafifu za virusi vya Corona anatakiwa kubakia nyumbani hadi pale atakapopata nafuu kamili. Dalili hafifu za Corona zinaweza kupunguzwa kwa kupumzika au kulala nyumbani, kuhakikisha mwili haupati baridi, kunywa vimiminika kwa wingi au kuoga maji ya moto. Mgonjwa anapopatwa na homa na kukohoa analazimika kupumzika nyumbani kwa kipindi kisichopungua siku 14 ili asiwaambukize wenzake. Iwapo homa na kukohoa kutaendelea baada ya siku 9 hadi 14 mgonjwa analazimika kumuona daktari.

Jinsi ya Kupima Corona:

Virusi vya Corona vya mwaka 2019 vinaweza kupimwa kwa kutumia mbinu kama zile za kupima virusi vingine kama vile kuchukua sampuli za damu, mate au tishu iliyotumiwa na mtu aliyeambukizwa. Baadaye sampuli hizo hutumwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi. Mgonjwa hutibiwa kwa kutumia mbinu za kudhibiti dalili za ugonjwa huo hadi kipindi chake kitakapomalizika. Kwa sasa wataalamu wangali wanafanyia majaribio chanjo mbalimbali za kutibu virusi hivyo. Aina nyingine za virusi vya Corona kama SARS na MERS zina chanjo na tiba yake. Virusi hivyo vinaweza kutibiwa kwa kutumia dawa za kukabiliana na virusi au kwa kutumia tiba ya tatizo la mapafu na kadhalika.   

Jinsi ya kuamiliana na Corona: 

Kuhusiana na virusi hivi, watu wanashauriwa kuwa watulivu na kujiepusha na tetesi na habari za vyanzo visivyo vya kuamini katika masuala ya tiba au takwimu zisizokuwa sahihi. Hakuna haja ya watu kuwa na wasiwasi na kukimbilia katika kutumia maski (barakoa) au kujifungia majumbani kabla ya kuhisi dalili za Corona. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wimbi la habari zinazotolewa mitandaoni kuhusiana na maambukizi ya Corona na idadi ya wahanga wa ugonjwa huo limesababisha wasiwasi na wahka mkubwa baina ya watu, na sasa wimbi hilo lenyewe limekuwa maradhi yanayohitajia tiba. Inatupasa kuelewa kwamba, virusi hivi vya Corona ni si vikali sana katika maambukizi na ukali wake kama virusi vya homa ya mafua (efluenza). Mtu anayepimwa na kukutwa na virusi vya Corona anashauriwa kuwa na utulivu na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya hadi pale atakapopata nafuu.

Chanjo na tiba ya Corona?

Kwa sasa wataalamu kote dunia anachacharika kutafuta chanjo na tiba ya virusi vya Corona. Baadhi ya wataalamu hao wanafanya jitihada za kupata tiba ya virusi hivyo kwa kutumia plasma ya damu ya wagonjwa waliopona na kupata shifaa. Wataalamu wengine wanachunguza athari za dawa za kufubaza virusi vya HIV Ukwimi na virusi vya Ebola kwa ajili ya kutibu virusi vya Corona. Ziko mbinu na njia na yingine kadhaa zinazotumiwa na wataalamu kwa ajili ya kupata tiba na chanjo ya Corona.

Ripoti ya jarida la The Scientist imesema kuwa, kunafanyika majaribio (clinical trial) karibu mia moja katika maeneo mbalimbali ya dunia kwa ajili ya kupata tiba ya virusi vya Corona (COVID19). Baadhi ya majaribio hayo yanafanyika katika nchi za China, Japan, Thailand, Iran, marekani, Ujerumani na Uingereza. Kwa mfano tu katika baadhi ya majaribio hayo yanayofanyika Shanghai, madaktari wanafanya jitihada za kuchanganya pasma ya damu (blood plasma) ya mgonjwa wa Corona aliyepata shifaa na kupona na damu ya mtu mwenye virusi hivyo kwa ajili ya kutengeneza dawa na Corona. Huko Japan wataalamu wanataka kutumia dawa za kufubaza Ukwimi (antiretroviral drugs) kutibu wagonjwa wa Corona. Huko Thailand madaktari wamefanikiwa kumtibu bibi kizee mwenye umri wa miaka 70 aliyekuwa na virusi vya Corona kwa kutumia mchanganyiko wa dawa za homa ya mafua (enfluenza) na dawa za virusi vya HIV. Mgonjwa huyo alipata ahueni masaa 48 baada ya kupewa mchanganyiko huo.

Madaktai wakipima joto la washukiwa wa Corona

Kampuni moja ya Marekani pia inadai kuwa imegundua chanjo ya virusi vya Corona.

Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, matokeo ya awali ya majaribio mawili muhimu ya virusi vya COVID 19 yatatangazwa karibuni. Moja kati ya majaribio hayo ni mchanganyiko wa dawa za Lopinavir na Ritonavir zinazotumika kutibu wagonjwa wa virusi vya Ukimwi.

Vilevile wataalamu wa Chuo Kikuu cha Tianjin karibu na mji wa Beijing wamefanikiwa kutengeneza chanjo ya kunywa na virusi vya Corona. Wataalamu hao wanasema chanjo hiyo pia inaweza kutumiwa kama dawa ya kutibu virusi hivyo.

https://multimedia.scmp.com/widgets/china/wuhanvirus/   

Maoni