Mar 28, 2020 08:36 UTC
  • Taathira za kisiasa, kijamii na kiuchumi za virusi vya COVID-19 (Corona)

Katika kipindi cha sasa kadhia ya maambukizi ya virusi vya COVID-19 au Corona ndiyo gumzo na kadhia muhimu zaidi inayojadiliwa katika duru zote za kisiasa na vyombo vya mawasiliano ya kijamii na hata baina ya watu wa familia.

Hadi sasa karibu watu laki sita wameambukizwa virusi hivyo katika nchi mbalimbali duniani. Virusi vya Corona viliibuka mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana 2019 katika mji wa Wuhan wa mkoa wa Hubei nchini China na sasa vimekuwa balaa kwa jamii nzima ya wanadamu.  

Virusi hivyo, kama wanavyosema wataalamu, si janga la kiafya na mfumo wa tiba pekee bali pia vimesababisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na vitaathiri sana siasa za ndani za nchi mbalimbali na katika upeo wa siasa za kimataifa. Taathira mbaya za virusi hivyo zimeenda mbali zaidi ya masuala ya kiafya, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na hata katika mahusiano baina ya wanadamu. Hii si mara ya kwanza kwa dunia kukumbwa na janga la maradhi ya kuambukiza kama hili la virusi vya Corona. Hata hivyo inaonekana kuwa, kutokana na upana wa virusi hivyo na kasi ya maambukizi yake, virusi vya Corona vinawekwa katika orodha ya magonjwa nadra ya kuambukiza yaliyoathiri watu katika pembe mbalimbali za duniani. Si ajabu pia hii ikawa mara ya kwanza katika historia kwa wanadamu wote kujihisi kwamba, wanayo hatima moja na kuwa na imani kwamba, virusi vya Corona vinatishia mustakbali wao wote kwa pamoja.

Kumetolewa nadharia na mitazamo mingi kuhusiana na jinsi virusi hivi vilivyoanza na kujitokeza. Moja na nadharia hizo ni kwamba, virusi vya Corona vilianzia katika soko la wanyama katika mji wa Wuhan huko China na kuhamia kwa wanadamu. Nadharia yenye nguvu zaidi ni ile inayosema kuwa, mtindo na aina ya vyakula wa Wachina na kula kwao wanyama kama popo, mbwa na kadhalika umekuwa na taathira kubwa katika kuhamia virusi hivi kwa wanadamu. Mtaalamu mmoja wa tiba za mitishamba na tiba za asili anasema: "Ni vigumu sana kupuuza tabia ya Wachina ya kula kila kitu wakati tunapochunguza chanzo cha virusi vya Corona. Anasema, utaratibu na ada hii ya Wachina ya kula kila kitu wakiwemo wanyama kama mbwa, nyani na mapopo, ulianza wakati Wachina waliposhambuliwa na kuzingirwa na Wajapani. Wakati huo Wachina walisumbuliwa na njaa kwa kipindi kirefu na tangu wakati huo ndipo walipoanza kula kila kitu na viumbe vya aina mbalimbali. Mtindo huu na aina mpya ya lishe baina ya Wachina ilivuruga mlingano wa lishe katika taifa hilo."

Pamoja na hayo inatupasa kusema kuwa, tabia na ada hii ya kula kila kitu haipo katika maeneo yote ya China na zaidi inashuhudiwa katika maeneo pwani ya nchi hiyo. Kwa maana kwamba, suala hili linashuhudiwa kwa nadra sana katika maeneo ya magharibi mwa China. Huwenda ni kwa sababu hii ndiyo maana tunaona kuwa, kiwango cha maambukizi ya virusi vya Corona magharibi mwa China, ambako watu wengi wanatumia vyakula halali, ni kidogo sana ikilinganishwa na maeneo mengine ya nchi hiyo. Inatupasa kusisitiza hapa kuwa, nadharia hii inayotajwa kuwa sababu ya virusi vya Corona bado inafanyiwa utafiti baina ya wasomi na waataamu.  

Nadhari na mtazamo mwingine kuhusu chanzo cha virusi vya Corona ni ule unaosema kuwa, virusi vya Corona (COVID-19) vilizalishwa katika maabara za Marekani kwa ajili ya kudumaza uchumi wa China na kwamba, virusi hivyo ni silaha inayotumiwa katika vita vya kibiolojia.

Katika kila nadharia inayotolewa kuhusiana na chanzo cha virusi vya Corona kunaonekana jambo moja lisilokuwa na shaka ndani yake, nalo ni taathira mbaya za virusi hivyo katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama kwa nchi mbalimbali duniani. Hadi sasa hakujawahi kushuhudiwa ugonjwa uliokuwa na taathira kubwa za kiafya, kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama katika upeo wa dunia nzima kuliko virusi hivi vya Corona. Athari kubwa ya virusi hivi inatokana na mapinduzi ya vyombo vya mawasiliano, utandawazi na dunia kuwa ndogo kama kijiji kimoja. Suala hili la “udogo” wa dunia ni katika awamu za mabadiliko makubwa katika maisha ya kiumbe mwanadamu na imeleta mabadiliko pia katika mtindo wa maisha, biashara na uhai wa kiumbe hicho. Pamoja na hayo utandawazi huu umeambatana na changamoto nyingi kwa mwanadamu na nchi mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizo ni kama hii ya maambukizi ya virusi vya Corona katika upeo wa dunia kwa kasi ambayo, mwanadamu hajawahi kushuhudia mfano wake.  

Magonjwa ya kuambukiza yamekuwepo siku zote na yamekuwa yakijitokeza ghafla hapa na pale, kuzusha wahka na hofu na kuua wanadamu. Zamani, tauni na kipindupindu vilikuwa vikichukua uhai na roho za watu wengi. Magonjwa haya yalikuwa yakitokea na kusababisha misiba na mjonzi baina ya wanadamu. Sasa magonjwa kama SARS, MERS, Ebola, Corona na kadhalika yamechukua nafasi ya magonjwa ya tauni na kipindupindu. Maradhi haya ya sasa hayatosheki wala kushiba kwa kuchukua nafsi na roho za wanadamu, bali yameatili na kudumaza maisha yao, na kila mahali yanapotia mguu yanaua, yanakwamisha kabisa kazi, biashara, burudani, masomo bali hata fikra na akili za watu. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, virusi vya Corona ni virusi vya teknolojia, na kama alivyosema Bill Gates, hata teknolojia ya kisasa inashindwa kushikana mieleka na kukabiliana na virusi hivyo. Inaonekana kuwa teknolojia inaweza kukabiliana na mabalaa ya kimaumbile na si majanga yanayosababishwa na teknolojia yenyewe. Hata hivyo tunaamini kwamba, ni mwanadamu ndiye anayeweza kushinda virusi hivi. 

Kipindi cha sasa kinafungua ukurasa mwingine katika historia ya mwanadamu yenye mashaka na pandashuka nyingi. Maambukizi ya viusi vya Corona na kasi yake vinaonyesha kuwa, janga hili halitambui mipaka ya nchi, kaumu, rika na vyeo vya watu. Virusi vya Corona vimemfundisha tena mwanadamu kwamba, huweza kudhamini usalama wako kwa njia ya kuvuruga usalama na amani ya wanadamu wenzako. Dunia tunamoishi imeshikamana sana kwa kadiri kwamba, ni muhali kuweza kujikinga na hatari na mabalaa kwa kujenga na kujizunguushia kuta ndefu au kujichimbia kwenye mahandaki nyuma ya mipaka ya kijiografia. Wakati Rais Donald Trump wa Marekani alipochukua hatua ya kustaajabisha na kuzindua mpango wake eti wa “Marekani Kwanza”, wanafikra wengi walitambua kwamba, kiongozi huyo amekwenda mrama na kupotoka njia sahihi. Hii leo serikali ya Marekani ambayo awali ilikana na kukadhibisha hatari ya mambukizi ya virusi vya Corona nchini humo, inawajihiana uso kwa uso na maambukizi ya virusi hivyo yanayoshika kasi siku baada ya nyingine. Viongozi wa White House walipaswa kufikiria suala hili hapo kabla na kuelewa kwamba, katika dunia ya leo ambayo imeungana na kuwa kama kijiji kimoja, moja ya mbinu bora zaidi za kujilinda na mabalaa ni kuwasaidia na kuwalinda wanadamu wa mataifa mengine na balaa mfano wake.   

Kama tulivyosema mwanzoni mwa makala hii, maambukizi ya virusi vya Corona yamekuwa na taathira kubwa za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kupungua kwa kiwango kikubwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa kutokana na tathmini ya wataalamu ya kupungua kwa ukuaji wa uchumi wa dunia ni miongoni mwa athari mbaya za virusi vya Corona. Sababu kuu ya kupungua ukuaji wa uchumi wa dunia inatajwa kuwa ni kupungua ustawi na ukuaji wa uchumi wa China ambayo inashika nafasi ya pili ya chumi kubwa zaidi duniani na mtumiaji mkubwa nambari mbili wa mafuta kote duniani. Uchumi wa China unahesabiwa kuwa ndiyo injini ya uchumi wa dunia. Ni vigumu sana kuweza kupata kampuni au shirika lolote kubwa na mashuhuri duniani lisilokuwa na tawi au soko nchini China.   

Mhadhiri wa academia ya Chuo Kikuu cha Pennsylvania nchini Marekani, Mauro Guillen anasema, katika miaka ya hivi karibuni masuala mawili yaani siasa na vita vya kibiashara vimekuwa vikitajwa kuwa ndio sababu za ukosefu wa uthabiti na kuyumbayumba imani katika uchumi wa dunia, na sasa kumejitokesa sababu ya tatu nayo ni virusi vya Corona. Guillen anaamini kwamba, virusi hivyo vitakuwa na taathira kubwa na nyingi kwa uchumi si kwa China pekee bali dunia nzima         

Tags

Maoni