Jun 02, 2020 07:39 UTC
  • Khordad 15, siku ya harakati ya umwagaji damu ya wananchi mashujaa

Bismillahir Rahmanir Rahim. Karibuni katika kipindi hiki maalumu cha kuzungumzia tukio muhimu sana katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na katika historia ya zama hizi ya Iran. Tukio hilo ni maarufu kwa jina la Khordad 15 kwa kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia. Mwaka huu tarehe 15 Khordad, Hijria Shamsia inasadifiana na tarehe 4 Juni Milaadia. Leo tumeamua kusema machache kuhusu suala hilo.

Tarehe 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 5 Juni, 1963 Milaadia, ilikuwa ni siku ya matukio muhimu sana nchini Iran. Baada ya kukamatwa Imam Khomeini MA kutokana na kuukosoa vikali utawala wa kidikteta wa wakati huo wa Iran, miji mbalimbali ya Iran ikiwemo ya Tehran na Qum ilishuhudia maandamano ya wananchi ya kupinga serikali ya Amir Asadollah Alam, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo.

Tarehe 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia ilikuwa ni siku ambayo wananchi Waislamu wa Iran walimwaga damu yao kwa jina la Uislamu na kwa ajili ya Uislamu. Tarehe 15 Khordad ilikuwa ni mwanzo wa mwamko mtukufu wa Kiislamu, ilikuwa ni siku ya kumuasi taghuti na mataghuti na ilikuwa ni siku ambayo taifa la Iran lilianza kufanya harakati yake chini ya bendera ya Uislamu na kuingia katika medani ya kupambana na maadui wa Uislamu na Qur'ani Tukufu na kuzitikisa vibaya nguzo za utawala wa kiimla wa Shah.

Khordad 15, 1342 Hijria Shamsia ilikuwa siku ya umwagaji damu

 

Katika hotuba aliyoitoa siku ya Ijumaa na tarehe 8 Juni 1984, Ayatullahi Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye wakati huo alikuwa Imam wa muda wa Sala ya Ijumaa ya Tehran alisema: Khordad 15 ni harakati iliyotokana na wananchi wenyewe kwa msukumo wa Uislamu na kwa mapenzi yao kwa wanavyuoni wa dini na kwa mapenzi na imani yao kwa Imam wao. Uti wa mgongo wa harakati ya Khordad 15 ni mapenzi kwa Uislamu na Imam na wananchi ambao walifanya harakati hiyo. Hivyo kilichotokea tarehe 15 Khordad ni mshikamano madhubuti baina ya wananchi na Imam, tena kwa baraka za Uislamu.

Si vibaya hapa tukarudi nyuma kidogo katika kurasa za historia. Mfalme wa zamani wa Iran, Mohammad Reza Pahlavi alirejea madarakani baada ya mapinduzi ya mwaka 1954. Alichofanya baada ya kurejeshwa madarakani na Wamarekani, ilikuwa ni kutumia ukandamizaji wa kila namna kuimarisha utawala wake. Hata hivyo mwaka 1961 kulitokea mabadiliko katika siasa za kimataifa na kumlazimisha Shah wa Iran aangalie upya siasa zake.

Mwezi Januari 1961, John F. Kennedy alishinda urais nchini Marekani. Siasa za Kennedy zilikuwa ni kuzuia mapinduzi ya wananchi katika nchi za ulimwengu wa tatu, hivyo aliwashawishi viongozi wa nchi hizo wafanyie mabadiliko ya kimsingi siasa zao ili kuwalaghai wananchi. Shah wa Iran naye alilazimika kufanya mabadiliko hayo, ikiwa ni pamoja na kufungua kidogo milango ya siasa, kufanyia marekebisho sheria ya ardhi na kufanya mapinduzi meupe.

Sehemu nyingine ya maandamano ya wananchi wa Iran ya kumuhami kiongozi wao, Imam Khomeini MA

 

Alichoshindwa kutambua Shah wa Iran ni kwamba istilahi hizo za kupandikiza zilikuwa hazikubaliani na muundo wa jamii ya Iran iliyokuwa inaishi kijadi. Matokeo yake ilikuwa ni kuzuka ukosefu wa utulivu, ukosefu wa amani na malamiko ya wananchi akiwemo Imam Khomeini MA ambaye alikosoa vikali siasa hizo. Upinzani na ukosoaji huo haukumfurahisha Shah wa Iran hivyo aliamua kutumia mkono wa chuma kukabiliana nao. Alichofanya ni kushambulia madrasa ya Faiziya mjini Qum mwaka 1963 na kumkamata Imam Khomeini MA nyumbani kwake. Hatua hiyo iliamsha hasira za wananchi ambao waliamua kusimama imara na kuanzisha harakati hiyo ya Khordad 15, mwaka 1963, na huo ukawa mwanzo wa mwamko wa Kiislamu nchini Iran ulioishia kwenye ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Alfajiri ya siku ya Jumatano ya tarehe 15 Khordad 1342 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 5 Juni 1963 Milaadia, maafisa usalama wa Shah wa Iran waliivamia nyumba ya Imam Khomeini mjini Qum na kumpeleka katika jela moja mjini Tehran. Siku tatu kabla ya hapo Imam Khomeini (quddisa sirruh) alikuwa ametoa hotuba kali sana ya kufichua usaliti wa Shah na mabwana zake. Saa chache tu baada ya kukamatwa Imam Khomeini MA, barabara za mji wa Qum zilijaa wananchi, wanaume kwa wanawake, wakubwa kwa wadogo, kupinga jambo hilo. Siku hiyo hiyo wananchi Waislamu wa Tehran nao walimiminika barabarani kupinga na kulaani vikali jambo hilo. Wanajeshi wa Shah waliopewa amri ya kukandamiza maandamano ya aina yoyote ile, walitumia silaha za moto kuwashambulia wananchi Waislamu wa Iran. Damu ya Waislamu iliyomwagwa wakati huo iliongeza hasira za wananchi kwa utawala wa Shah. Hivyo Khorad 15 imekuwa ni siku ya kihistoria katika mapambano ya wananchi wa Iran na ilifungua ukurasa mpya wa mapambano ya watu wanyonge dhidi ya mabeberu na waistikbari duniani.

Ijapokuwa wanajeshi na askari usalama wa Shah waliweza kuzima kwa muda mwamko huo, lakini harakati za wananchi wa Iran dhidi ya utawala kibaraka wa dikteta Shah ziliendelea hadi yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu Februari 11, 1979 nchini Iran.

Maandamano makubwa ya wananchi wa Iran baada ya kusikia mfalme Shah amemkata Imam Khomeini MA mwaka 1963

 

Baada ya tukio hilo la Khordad 15, 1342 Hijria Shamsia, na licha ya kuweko uchujaji mkubwa wa habari kutoka kwa taasisi za mfalme Shah, lakini ile sehemu ndogo tu ya habari iliyoenea kuhuSu kukamatwa Imam Khomeini MA na kufanyika mauaji ya kutisha ya Khordad 15, mwangwi wake haukuishia katika kona zote za Iran tu, bali ulitoka nje ya mipaka ya nchi na kuenea hadi katika maeneo mengine hasa ya Iraq.

Wimbi la hasira na ghadhabu dhidi ya mfalme Shah lilienea katika Hawza na vyuo vikuu vya kidini vya Najaf, Karbala na Kadhimein nchini Iraq na uungaji mkono kwa Imam Khomeini MA ukawa mkubwa ndani na nje ya Iran. Telegraph zilitumwa kutoka kona mbalimbali za nchi za Waislamu na taasisi za kimataifa kulaani vikali mauaji yaliyofanywa na mfalme Shah katika tukio hilo la Khordad 15. Matukio yote hayo yalitokea katika hali ambayo vyombo vya habari ndani ya Iran vilikuwa vimenyamazia kimya kabisa matukio hayo ya kutisha ya Khordad 15.

Baada ya Mfalme Shah kuona wimbi la hasira limekuwa kubwa, alilazimika kumwachilia huru mwanachuo mwanaharakati na mpigana jihadi, Imam Khomeini MA. Hata hivyo hilo nalo halikuzima hasira za wananchi, bali upinzani mkubwa uliendelea ndani na nje ya Iran. Hatua nyingine muhimu iliyochukuliwa na maulamaa wa daraja la kwanza nchini Iran, ni kukusanyika mjini Tehran, kutafuta njia za kuamiliana na suala hilo. Marajii walitoa tamko la pamoja na kusisitiza kuwa Imam Khomeini (MA), ni mujtahid aliyetimiza sifa zote na ni marja’a, hivyo ana kinga kwa mujibu wa sheria za nchi. Baada ya hapo, utawala wa kiimla wa Shah haukuwa na chaguo jingine isipokuwa kumwachilia huru Imam Khomeini tarehe 17 Farvardin 1343 Hijria Shamsia, ingawa hata hivyo mapambano yaliendelea hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi Februari 11, 1979 na kupinduliwa kikamilifu utawala kibaraka wa Shah, nchini Iran.

Mapambano ya Khordad 15, (Juni 4, 1963) yalichangia sana kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ya Februari 11, 1979

 

Hapa ni vizuri tukagusia kidogo mchango na taathira za mapambano ya Khordad 15 katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwezi Februari 1979 nchini Iran. Kiujumla mapambano ya Khordad 15 yalikuwa na taathira kubwa katika kufikia ushindi mapinduzi hayo matukufu. Mosi ni kwamba matukio ya Khordad 15 yalihamisha uongozi wa mapambano ya kupinga utawala kibaraka wa Shah kutoka kwa watu wenye misimamo ya mirengo ya kushoto na kitaifa na kuuingiza mikononi mwa viongozi wa kidini na sasa harakati za wanamapinduzi nchini Iran zikapata sura ya kidini zaidi.

Pili mauaji ya watu wasio na hatia yaliyofanywa na utawala wa Shah yalifichua sura halisi ya ukatili na ukibaraka ya mfalme dikteta Shah wakati ambapo kabla ya mapambano ya Khordad 15, mfalme Shah alikuwa akijificha nyuma ya Waziri Mkuu na alikuwa haoneshi kwamba yeye ndiye muhusika mkuu. Lakini baada ya mauaji ya Khordad 15, wanamapinduzi nchini Iran walielekeza nguvu zao kwenye kuuangusha kabisa utawala wa kiimla wa Shah na sio kupigania mabadiliko tu ndani ya utawala wake kibaraka.

Tatu, kuanzia wakati huo, suala la kuyatimua madola yote ajinabi na ya kibeberu nchini Iran lilipata nguvu na ndio maana mapambano ya Khordad 15 yanahesabiwa kwamba ndio uliokuwa mwanzo wa harakati ya kupigania kujitawala na kujitegemea taifa la Iran na kupinga utegemezi kwa wageni. Kuanzia wakati huo zilianza kuchipua jumuiya mbalimbali za Kiislamu katika kona tofauti za Iran na anga ya kupinga dini na iliyokuwa dhidi ya Uislamu ambayo ilikuwa imetawala katika vyuo vikuu na katika taasisi na jumuiya nyinginezo humu nchini, ilianza kusambaratika.

****