Jun 18, 2020 05:41 UTC
  • Mafundisho ya afya na usafi ya Uislamu, suluhisho la kukabiliana na corona

Afya na siha ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu ambayo thamani yake huonekana vyema wakati mwanadamu anapopatwa na maradhi.

Japokuwa wanadamu daima na siku zote hupatwa na aina mbalimbali za maradhi na mashaka mengine mengi, lakini maradhi ya kuambukiza huwatia wahka na wasiwasi mkubwa zaidi kutokana na kuenea kwake kwa wingi, katika kipindi kifupi na kuua idadi kubwa ya watu. Virusi vya corona vilivyoanzia China ambavyo sasa vimeenea na kusambaa katika kona zote za dunia katika kipindi kifupi, ni miongoni mwa maradhi ya aina hiyo. Hadi sasa virusi hivyo vilivyopewa jina la COVID-19, vimewakumba mamilioni ya watu kote dunia na inasikitisha kusema kwamba, tayari vimeua karibu nusu milioni ya watu.

Kwa sasa madaktari na wataalamu wa dawa na tiba wametoa maagizo mengi ya jinsi ya kujikinga na virusi hivi visivyo na tiba wala dawa. Uislamu kama dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu pia umekuja na mafundisho na maelekezo ya jinsi ya kujikinga na maradhi, na hapana shaka kuwa, mafundisho na miongozo hiyo ya Uislamu inaweza kuwa na thamani kubwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.  

Tunaweza kusema kwa ujasiri kwamba, hakuna dini wala mfumo wowote wa kifikra wa kiroho au kimaada uliolipa umuhimu suala ya afya na siha ya wanadamu kuliko dini tukufu ya Uislamu. Mtume Muhammad (swa) anasema: "Kuna neema mbili ambazo wanadamu hawatambua thamani zake: Moja ni siha na afya, na nyingine ni ujana." Wasii na Khalifa wake wa haki, Imam Ali bin Abi Twalib (as) pia ameitaja sifa na afya kuwa ndiyo neema kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu. Anasema: "Mwanadamu hujua ladha halisi ya maisha pale anapokuwa na siha na afya." Mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Jafar Swadiq (as) pia ameitaja siha kuwa ni neema ambayo ni muhali kuweza kupanga thamani yake. Ni kwa kutilia maanani mafundisho na miongozo kama hii ya viongozi wa Uislamu ndiyo maana Waislamu wakafanikiwa kupata maendeleo makubwa sana katika elimu ya tiba miaka kadhaa baada ya kudhihiri dini hiyo. Vilevile tunapotazama haraka haraka aya za Qur'ani tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu tunaona kuwa, dini ya Uislamu imetenguliza na kuweka mbele suala la kujikinga na maradhi. Zaidi ya miaka 1,400 iliyopita dini hiyo ilitoa maagizo na mafundisho ya kina kuhusu afya na siha ya mtu binafsi na jamii, mazingira na kadhalika na kuwahimiza wafuasi wake wasizembee katika kulinda afya na siha zao.

Wataalamu wanasema kuwa, miongoni mwa njia za kukabiliana na virusi vya corona ni kuimarisha mfumo wa ulinzi wa mwili. Katika uwanja huo Mtume Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake watukufu wametuusia kutumia mimea na vyakula ambavyo hii leo watalaamu wa tiba ya Kiislamu na Kiirani wanatuhimiza kuvitumia mara kwa mara. Mfano wa vyakula na mimea hiyo ni asali, mdalasini, tangawizi, thyme, kitunguu saumu na kadhalika. Vilevile Mtume (saw) na maimamu katika kizazi chake wamewausia wanadamu kutumia lishe sahihi, kujiepusha kula kupita kiasi na kutumia vyakula salama na vinavyoimarisha mwili kwa ajili ya kulinda siha na afya. Kwa mfano tu Qur'ani tukufu inasisitiza katika Aya zake kwamba, Mwenyezi Mungu SW amekuhalalishieni vyakula safi na salama na kukuharamishieni vyakula na vinywaji visivyo safi na salama. Akitoa tafsiri ya aya hizi za Qur'ani, Imam Jaafar Swadiq (as) anasema: "Mwenyezi Mungu SW ambaye ndiye aliyemuumba mwanadamu, anajua nini kina faida kwa mwanadamu huyo na kipi kina madhara; na kwa sababu hiyo amehalalisha vyakula na vinywaji vyenye faida kwa mwanadamu, na kuharamisha vinavyokuwa na madhara kwake." Kwa mfano, dini ya Uislamu imeharamisha kula nyama ya baadhi ya wanyama wakiwemo popo. Hivyo basi iwapo dhana ya baadhi ya madaktari itakuwa ya kweli kwamba virusi vya corona vimeingia kwenye mwili wa mwanadamu kutokana na kula nyama ya popo, basi tunaweza kuelewa vyama zaidi hekima na thamani ya mafundisho ya Uislamu.

Tangu virusi vya corona vilipoanza kusambaa baina ya wanadamu huko China madaktari wamekuwa wakihimiza suala la kujali usafi na udharura wa kuosha mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni. Haya ndiyo mafundisho yaliyohimizwa na Uislamu tangu karne nyingi zilizopita na kuwataka wafuasi wake kuyatekeleza. Suala la kulinda na kujali usafi limehimizwa sana na wakati mwingine kufanywa faradhi na wajibu katika mafundisho ya dini hiyo. Mtume Muhammad (saw) anasema: "Uislamu umejengeka juu ya msingi wa usafi na hataingia Peponi isipokuwa mtu nadhifu." Si hayo tu bali Uislamu umelipa umuhimu mkubwa suala la mtu kuwa safi na nadhifu kiasi kwamba, umelitambua suala la kuwa nadhifu na msafi kuwa ni sehemu ya imani. Mtume (saw) anasema: "Kuwa nadhifu na msafi ni sehemu ya imani."

Miongoni mwa mafundisho muhimu ya Uislamu ambayo yamehimizwa kufanywa katika nyakati zote ni usafi wa mwili hususan mikono. Waislamu wanalazimishwa kuosha mikono na nyuso zao mara kadhaa kila siku kwa ajili ya ibada ya Swala. Vilevile dini hiyo inawahimiza wanadamu kuosha mikono yao kabla na baada ya kula chakula. Dini hiyo pia inamuwajibisha kila mtu kulinda na kujali afya na siha za wanadamu wenzake na inamtambua mtu anayemsababishia mwanadamu mwingine maradhi na matatizo ya kiafya kwa sababu ya yeye mwenyewe kutojali usafi, kwamba amefanya dhambi.

Hivyo basi pale madaktari wanapotangaza kwamba, kugusana na watu kunazidisha hatari ya kuambukizana maradhi na virusi vya corona, inakuwa wajibu kwa watu wote, hususan Waislamu, kufuata na kuheshimu maagizo hayo kwa ajili ya kulinda afya zao wenyewe na jamii nzima kwa ujumla ili wasije wakajikuta wanafanya dhambi. Dini hiyo pia, licha ya kwamba inahimiza sana mikutano na mijumuiko ya wafuasi wake kwa ajili ya ibada na mambo mengine yenye umuhimu kwa jamii, lakini imejuzisha kuzuia mikusanyiko na mikutano hiyo ya kidini na kiroho pale inapobainika kuwa, yumkini ikahatarisha afya na uhai wa wanadamu. Ukweli huu unashuhudiwa hivi sasa ambapo maeneo mengi matakatifu kama Msikiti wa Makka, Msikiti wa Madina, maziara matukufu ya Maimamu na wajukuu wa Mtume (saw), misikiti ya Swala za Ijumaa na jamaa yote imefungwa kwa shabaha ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona vinavyohatarisha uhai wa wa wanadamu. Historia pia inasimulia kwamba, Mtume Muhammad (saw) alijiepusha kugusana na watu waliokuwa na magonjwa ya kuambukiza na kuwaamuru watu wengine wasio matabibu kukaa mbali na wagonjwa wa aina hii. 

Wapenzi wasikiliza inatupasa kutambua kwamba, katika fikra za dini ya Kiislamu, matibabu ya maradhi ukiwemo ugonjwa wa sasa wa COVID-19 (corona), yanafuata kanuni kuu zinazotawala ulimwengu. Dini hii inasisitiza kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye muumbaji wa dunia, mbingu na vilivyomo na kazi yoyote haiwezi kuwa na taathira katika dunia hii bila ya idhini na matakwa yake Yeye. Kwa kutilia maanani kanuni hii kuu inayotawala dunia, tunatambua kwamba, ni Yeye Mwenyezi Mungu Hakimu na Mjuzi pekee ndiye anayetoa shifaa na kuponya magonjwa. Suala hili limeelezwa kwa uwazi zaidi katika aya ya 80 ya Suratu Shu'araa pale Nabii Ibrahim anaposema: Na ninapougua ni Yeye ndiye anayeniponesha.

Pamoja na haya inatupasa kutambua kwamba, wakati mwingi Mwenyezi Mungu SW hutekeleza matakwa na irada yake kupitia viumbe vyake, sawa viumbe hivyo vikawa wanadamu, malaika, mimea na kadhalika. Kuhusiana magonjwa inatupasa kusema kuwa, sehemu ya awamu za shifaa ya Mwenyezi Mungu hutimia kupitia kwa madaktari, tabibu na wataalamu wa tiba. Ni kwa sababu hiyo pia ndiyo maana haikubaliki katika Uislamu mtu kuacha kwenda kwa tabibu na daktari kwa hoja kwamba, ataomba shifaa na maponyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu tu. Hatua kama hii pia inapingana na mienendo ya Mitume na Mawalii wema wa Mwenyezi Mungu ambao walikuwa wakifuatilia awamu mbalimbali za kujikinga au kutibu maradhi sambamba na kutawasali, kuomba dua na kumlilia Mwenyezi Mungu.

Imam Swadiq (as) anasimulia kwamba: "Mmoja kati ya Mitume wa Mwenyezi Mungu alipatwa na maradhi na akasema: Sitajitibia mpaka Mwenyezi Mungu mwenyewe anipe shifaa na kuniponesha. Mwenyezi Mungu aliteremsha Wahyi na ufunuo akisema: Sitakuponya hadi pale utakapojitibu. Elewa kwamba shifaa na ponyo ni kutoka kwangu."

Dini ya Uislamu pia imethamini sana kazi ya madaktari na wauguzi na imepokewa kwamba Mtume (saw) amesema: "Mtu anayefanya jitihada za kukidhi matakwa ya ngonjwa, atafutiwa madhambi yake na kuwa kama siku aliyozaliwa na mama yake, sawa haja ya mgonjwa ikidhiwe au la."  

Dua, maombi na kumtaradhia Mwenyezi Mungu Muumba ni miongoni mwa njia za kijikinga na maradhi.

Miongoni mwa njia muhimu zilizohimizwa na dini ya Uislamu kwa ajili ya kutatua matatizo yakiwemo ya kutibu maradhi, ni dua, maombi na kumtaradhia Mwenyezi Mungu Muumba na Mwenye huruma. Hii leo pia wasomi wamethibitisha kwamba, imani ya dini ina taathira kubwa katika koboresha afya na siha za wanadamu. Wakati mgonjwa anapomkimbilia Mwenyezi Mungu na kumlilia Yeye huwa amejiegemeza kwa Mola Karima, Mwenye huruma, Rahman na Rahiim ambaye ndiye anayetoa ponyo na shifaa ya mwisho. Ni wazi kuwa kadiri imani ya Mtu kwa Mwenyezi Mungu Muweza wa yote inavyokuwa kubwa zaidi, ndivyo dua na maombi yake yanavyokuwa na taathira kubwa zaidi.

Daktari na mwanabiolojia maarufu wa Ufaransa Alexis Carrel na mshindi wa tuzo ya Nobel anasema: "Dua na maombi ndiyo nguvu kubwa zaidi inayoweza kuanzishwa na wanadamu ndani ya nafsi yake. Mimi katika kazi yangu ya udaktari, nimewaona watu ambao baada ya matibabu yote kushindwa kutibu maradhi yao walifanikiwa kutibu magonjwa mbalimbali na matatizo yao ya kinafsi kwa kutumia nguvu ya dua na maombi." Katika uwanja huo zimepokewa dua kadhaa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake ambazo wanadamu wanaushauriwa kuzisoma wakati wanapopatwa na mabalaa na magonjwa kama corona.  

Tags