Aug 12, 2020 13:27 UTC
  • Maytham al-Tammar; Kigezo cha Subira na Kusimama Kidete (Kumbukumbu ya kuuawa kwake shahidi)

Assalaamu Alaykum Wapenzi Wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi Maytham al-Tammar mmoja wa masahaba na wafuasi wa Mtume SAW na Imam bin Abi Talib AS ambaye aliondokea kuwa mashuhuri kutokana na Imani thabiti, subira na msimamo usiotetereka katika njia ya haki.

Huku nikitoa mkono wa pole kwa waislamu wote na hasa wafuasi wakweli wa Uislamu na wapigania haki na uadilifu duniani nina matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki maalumu.

Tarehe 22 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja inasadifiana na kumbukumbu ya kuuawa shahidi Maytham al-Tammar mtu aliyepata umashuhuri kutokana elimu yake na kufuata njia ya haki na kusimama kwake kidete katika njia hiyo huku akiwa na subira isiyo na kifani. Kurasa za historia zinaonesha kwamba, Maytham al-Tammar alikuwa muuza tende wa kawaida sana, lakini imani thabiti aliyokuwa nayo ilimfanya kuwa mmoja wa wasomi na mafakihi wakubwa kati ya masahaba wa Imam Ali AS. Alisoma tafsiri ya Qurani tukufu na hadithi katika maktaba ya Ali bin Abi Twalib AS na kuondokea kuwa hazina na dafina ya elimu na maarifa ya Mwenyezi Mungu.

Maytham al-Tammar katu hakunyamazia kimya dhulma iliyokuwa ikifanywa na watawala waovu katika zama zake. Alikuwa akisimama na kufichua wazi wazi kwa kinywa chake dhulma, fitina na ufisadi uliokuwa ukifanywa na watawala madhalimu katika zama hizo. Imani yake hiyo thabiti na taqwa na uchaji Mungu wake usio na mithili sambamba na kujitolea kwake na kusimama kidete katika njia ya haki na uadilifu, ndivyo vilivyomgharimu maisha yake na kumfanye auawa shahidi kwa kusulubiwa katika mtende baada ya kukatwa, mikono, miguu na ulimi wake. Hiyo ilitokana na watawala katika zama hizo kushindwa kuvumilia msimamo thabiti wa Maytham al-Tammar ulikuwa ukileta mwamko baina ya watu.

 

Maytham Yahya al-Tammar alileleka na kukulia katika maktaba ya kuwajenga wanadamu yaani Maktaba ya Uislamu na alikuwa mmoja wa masahaba wa karibu wa Imam Ali AS.  Maytham alikuwa Muirani na alikuwa na hamu kubwa ya kusoma elimu na hekima kwa Imam Ali bin Abi Twalib AS. Kwa msingi huo akaiweka roho na uhai wake kwa maarifa ya elimu ya Imam Ali. Kwa upande wake Imam Ali As ambaye alimkuta Maytham al-Tammar kwamba, ni mstahiki na mtu mwenye kipawa ambapo baadhi ya wakati alikuwa akienda katika kibanda cha Maytham al-Tammar alipokuwa akiuzia tende na kukaa akizungumza pamoja naye. Katika vikao hivyo, Imam alikuwa akimfundisha Maytham Qur'ani na hekima tofauti za dini. Sahaba huyo mwema wa Imam Ali alifanikiwa kujifunza elimu mbalimbali kutoka kwa kiongozi huyo wa wacha Mungu. Kubobea Maytham al-Tammar katika Tafsiri ya Qur'ani kulimfanya mwanamapambano huyo kuhesabiwa kuwa mtu mwenye daraja maalumu katika elimu hiyo baada ya Imam Ali AS.  Katika moja ya safari zake mjini Madina, Maytham al-Tammar alikutana na Ibn Abbas ambaye naye ni mfasiri wa Qur'ani na mwanafunzi mwingine wa Imam Ali bin Abi Twalib na kumwambia:

Ewe mwana wa Abbas! Uliza utakacho kuhusu tafsiri ya Qur'ani; kwani nimesoma lafudhi za Qur'ani kwa Amir al-Muuminina Ali AS na kwa hakika yeye amenifundisha maana zake za batini. Kisha Ibn Abbas akaomba aletewe kalamu na karatasi ili aweze kuandika dondoo za kila atakachomuuliza Maytham al-Tammar.

Maytham al-Tammar alikuwa mtu mwenye kutunza sana siri na katu hakuwa akieleza isipokuwa kwa dharura na mahala inapohitajika kile alichojifunza kutoka kwa Imam Ali AS. Uaminifu mkubwa na utunzaji siri wa hali ya juu aliokuwa nao Maytham al-Tammar, ulimfanya Imam Ali AS amueleze na kumhadithia sahaba wake huyo baadhi ya siri ambazo kwa hakika hakuwa akimueleza kila mtu. Hivyo akamjuza kuhusiana na mambo yatakayotokea baadaye, yakiwemo mabalaa na fitina mbalimbali. Imam Ali alimueleza pia Maytham al-Tammar jinsi atakavyouawa shahidi. Baada ya kusikia hayo, Maytham akawa amejitayarisha kwa ajili ya kifo cha heshima na fakhari. Historia inasimulia kwamba, siku moja Maytham alikwenda kwa Imam Ali AS na mara Imam Ali alipomuona alimkodolea macho na kusema: Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, ninaiona siku ambayo mikono na ulimi wako vitakatwa na wewe kusulubiwa katika mtende. Maytham alishangaa na kuuliza: Ina maana ni kweli tukio hilo litatokea? Imam Ali As akasema: Ndio, ninaapa kwa Mola wa Kaaba, hilo litatokea na hii ni siri ambayo Mtume SAW alinieleza. Maytham al-Tammar akasema kumwambia Imam Ali AS kwamba: Kamwe Mtume wa Allah hasemi uongo na mimi nina imani kwamba, hili unalilosema litatokea hivi hivi. Kisha Imam Ali AS akamwambia Maytham: Njoo pamoja nami nikuonyeshe mtende ambao utatundikwa na kusulubiwa juu yake. Imam alimuonyesha Mytham mtende huo. Baadhi ya wakati, Mytham alikuwa akiswali chini ya mtende huo na kusema: Ewe mtende! Mimi nimeumbwa kwa ajili yako na wewe umekuwa na kustawi kwa ajili yangu.

سردر مقبره میثم تمار

 

Ikapita miaka mingi baada ya tukio hilo na utawala ukaangukia mikononi mwa watu madhalimu kama Muawiyah na baada yake mwanawe yaani Yazid, aliyejulikana kwa ufuska na ulevi. Katika kipindi hicho dhulma na ukandamizaji wa watawala madhalimu wa zama hizo ulikuwa mkubwa na wa kinyama kiasi kwamba, kama mtu atamsema vibaya mtawala au akamlalamikia mmoja wa maafisa wa utawala, basi hukabaliwa na mashtaka ya kujibu, vitisho, maudhi, mateso na kubaidishwa au hata kupoteza maisha yake. Mintarafu hiyo, watu walikuwa wakificha haki ili kumridhisha na kumfurahisha mtawala na sio kutaka radhi za Mwenyezi Mungu.

Katika mazingiara hayo magumu na ya kutisha, Maytham al-Tammar alikuwa akiizungumzia wazi wazi haki na uadilifu pamoja na fadhila na utukufu wa Bwana Mtume SAW na Ahlul Byat zake AS. Ufichuaji huo wa Maytham pamoja na msimamo wake thabiti, uliwakasirisha mno watawala wa zama hizo hususan Ubaidullah ibn Ziyad mtawala wa wakati huo wa mji wa Kufa nchini Iraq ambaye alitoa amri ya kutiwa mbaroni Maytham.

Licha ya kuwa katika zama hizo Maytham al-Tammar alikuwa mzee na mtu mzima na hakukubakia katika mifupa yake ya mwili isipokuwa ngozi iliyokunjana kunjana, lakini kwa upande wa ushujaa, uwezo wa kiroho, uzungumzaji, ufasaha na imani thabiti alikuwa imara mno jambo ambalo liliwatisha na kuwaogopesha askari wa utawala wa Ibn Ziyad. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana walitumwa watu mia moja kwenda kumtia mbaroni Maytham al-Tammar.

Mahala alipozikwa Maytham al-Tammar katika mji wa Kufa Iraq

 

Baada ya kutiwa mbaroni sahaba huyo wa Imam Ali AS alisimama kwa ushujaa kamili bila ya woga wowote mbele ya mtawala Ibn Ziyad. Mtawala huyo dhalimu alimshinikiza Maytham ili abadilishe itikadi yake. Hata hivyo Maytham hakusalimu amri. Ubaidullah Ibn Ziyad alikasirishwa mno akamwambia kwa chuki na ujeuri: Pamoja na kuwa wewe ni Muirani na sio Mwarabu, vipi unathubutu kuzungumza na mimi kwa njia hii? Kisha akizungumza kwa vitisho aliendelea kusema: Nimepatiwa habari kwamba, wewe ulikuwa mtu wa karibu sana na Ali! Lazima umchukie Ali na umtaje kwa ubaya la sivyo nitaikata mikono na miguu yako na kukusulubu. Katika kujibu vitisho hivyo Maytham alisema: Imam Ali alinipa khabari kwamba, utanisulubu. Ibn Ziyad akamwambia Maythamn, basi kwa kuwa unasema hivyo, mimi nitafanya kinyume na utabiri wa Ali! Maytham akasema: Huwezi, kwa sababu Ali amelisema hilo akinukuu kutoka kwa Mtume SAW. Ninaapa kwa Mola, nifahamu hata mahala ambapo nitasulubiwa katika mji wa Kufa. Ibn Ziyad akiwa amepandwa na ghadhabu akasema, Ninaapa kwa Mola! Ninakata mikono na miguu yako na kuacha ulimi wako ili uongo wa kiongozi wako udhihirike.

Akiwa ametundikwa juu ya mtende huku miguu na mikono yake iliyokatwa ikichirizika damu, Maytham alikuwa akipaza sauti na kuwaita watu waje wasikilize ukweli wa Uislamu na hadithi alizosikia kutoka kwa Imam Ali AS. Aliendelea kutaja fadhila za Ahlul Bayt AS na kufichua khiyana na ufisadi wa utawala wa Bani Umaiyyah. Maneno yake hayo yalikuwa na taathira mno kiasi kwamba, Ibn Ziyad akapewa habari kwamba, bwana huyu yaani Maytham al-Tammar amekuumbua. Ubaidullah bin Ziyad ambaye hakuwa akiamini kwamba, Maytham al-Tammar aliendelea kuzungumza tu na kuonyesha msimamo wake thabiti hata akiwa amesulubiwa juu ya mtende aliamrisha akatwe ulimi na hivyo kuwa Mwislamu wa kwanza kukatwa ulimi katika njia ya Uislamu. Baada ya Maytham al-Tammar kuuawa shahidi, mtawala dhalimu Ibnu Ziyad hakuruhusu mwili wake uzikwe ili kwa njia hiyo kama alivyodai awe ameunjia heshima mwili wa mwanapamabano huyo na kuwafahamisha watu wengine kwamba, hii ndio hatima na majaaliwa ya wafuasi wa haki na uadilifu. Hata hivyo marafiki wa Maythamn al-Tammar na wafanyabiashara wenzake wa tende walitumia hila na kufanikiwa kuuzika mwili wa Shahidi huyo. Hii leo kaburi la Maytham al-Tammar lipo baina ya Najaf na Kufa na watafuta haki hulizuru na kulitembelea kaburi hilo.

Amani ya Mwenyezi Mungu, Malaika na watu wema iwe juu ya Maytham al-Tammar ambaye, hadi leo angali anatoa nuru katika njia ya ubinadamu na kuonyesha watu njia ya haki.

Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na hasa wafuasi wa kizazi cha Bwana Mtume SAW na masahaba wema kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Maytham al-Tammar.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.