Feb 01, 2021 05:49 UTC
  • Juhudi za Iran za kuimarisha uthabiti, usalama na ushirikiano kati ya nchi za eneo

Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu usalama wa eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) zimesimama juu ya msingi wa usalama wa pamoja. Ni kwa msingi huo ndipo ikaamini kuwa kuvurugwa usalama wa eneo ni kwa madhara ya nchi zote za eneo hili.

Ikiwa moja ya nchi zenye umuhimu mkubwa katika eneo hili la Asia Magharibi Jamhuri ya Kiislamu ya siku zote imekuwa ikisisitiza udharura wa kubuniwa na kupitishwa mfumo wa kieneo wa pande mbili na pande kadhaa wa kisasa na kiusalama utakaodamini maslahi ya kiusalama ya nchi zote za eneo hili. Kuhusu suala hili, imetangaza wazi mara kadhaa kuwa kwake tayari kwa ajili ya kushirikiana na kubadilishana mawazo na nchi zote za eneo kwa ajili ya kufuatilia njia za kufikia lengo hilo na kukabiliana na vitisho, changamoto na vizuizi vinavyozuia kufikiwa suala hilo.

Juhudi za Iran kwa ajili ya kuleta uthabiti na usalama katika eneo zimesimama juu ya msingi wa usalama kwa ajili ya wote. Kwa msingi huo, Iran inaamini kwamba uthabiti na usalama wa eneo unapaswa kudhaminiwa kwa pamoja na kwa ushirikiano wa nchi zote za eneo, bila ya uingiliaji wa kijeshi wa madola ya kigeni.

Maadhimisho ya Bahman 22 nchini Iran

 

Uzoefu unaonyesha kwamba iwapo usalama utapatikana katika eneo, hilo litakuwa ni kwa manufaa ya nchi zote na iwapo utakosekana nchi zote za eneo zitadhurika.

Uzoefu wa kushindwa nchi za kigeni kudhamini usalama wa eneo pia unathibitisha kwamba mitazamo ya upande mmoja haiwezi kwa vyo vyote vile kudhamini usalama huo na kwamba ni kosa la wazi na lisilokuwa na natija yoyote isipokuwa kuyaletea madhara na gharama zisiso na maana mataifa ya eneo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka nchi zote za eneo zishirikishwe kweye mipango ya pamoja ya kudhamini usalama. Nia njema ya Iran kuhusu jambo hilo ilitangazwa wazi na Rais Hassan Rouhani kupitia mpango wa amani na usalama aliouwasilisha katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2019, kwa jila la Mpango wa Amani wa Hormoz.

Kwa kuwasilisha mpango huo, Iran ilizitaka nchi zote za Asia Magharibi na hasa za Ghuba ya Uajewmi kushirikiana katika kudhamini usalama wa eneo hili nyeti na la kistratijia. Suala hilo linathibitisha wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa umuhimu mkubwa suala zima la kupatikana uthabiti na usalama wa kudumu katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz na kwamba jambo hilo ni sawa na kudhaminiwa usalama wa nchi zote jirani na vilevile za kimataifa. Ni kutokana na ukweli huo ndipo ikawa inafanya juhudi kubwa za kupambana na vitendo vyo vyote vinavyovuruga amani na usalama katika eneo.

Mwaka wa 42 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

 

Muungano bandia uliobuniwa na Marekani kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa meli zinazopita katika Lango Bahari la Hormoz ni hatua hatari na ya kichochezi ambayo imelenga kuvuruga amani na usalama wa lango bahari hilo. Marekani imepanga kufikia malengo kadhaa ya kiusalama, kisiasa na kiuchumi katika uwanja huo.

Kuhusu suala la usalama, Marekani imebuni muungano huo kwa ajili ya kuzua hofu duniani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuzidisha mashinikizo ya kimataifa dhidi yake. Muungano huo pia unakusudia kudhoofisha ushirikiano wa Iran na majirani zake na hivyo kuibua wingi la kutoaminiana pande mbili hizo.

Lengo la kiuchumi la Marekani katika uwanja huo ni kuendelea kuimarisha soko la silaha zake za mauaji ya umati kati ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kupitia madai matupu ya kuzidhaminia usalama. Katika miongo kadhaa iliyopita na hasa wa hivi karibuni, Marekani imekuwa ikieneza uvumi wa tishio la Iran kati ya nchi za Kiarabu na hivyo kujiandalia fursa ya kurundika silaha zake angamizi katika nchi hizo na hasa Saudi Arabia na Imarati. Kwa muhtasari ni kwamba kwa kueneza siasa hizo chafu dhidi ya Iran katika eneo la kistartijia la Ghuba ya Uajemi, Marekani imefanikiwa kueneza hofu bandia kati ya nchi za Kiarabu ili kufikia malengo yake haramu katika nchi hizo na kwa madhara ya nchi zote za eneo hili.

Baradi kali na mabadiliko ya hali ya hewa hayawazuii wananchi wa Iran kuadhimisha kwa hamasa kubwa ushindi wa Mapinduzi yao matukufu ya Kiislamu

 

Kwa bahati mbaya, baadhi ya nchi za eneo zimehadaika na siasa hizo za hadaa za Marekani na hivyo kuvuruga zaidi amani na usalama wa eneo hili muhimu kimataifa. Qassem Muhibbali,mwanadiplomasia wa zamani na mchambuzi wa masuala ya kisiasa anaashiria muungano huo wa Kizayuni na Kiarabu ulioanzishwa na Marekani dhidi ya Iran na kusema: 'Utawala wa Kizayuni, Saudi Arabia na baadhi ya viongozi katika serikali ya Trump kama vile Mike Pompeo wana hamu kubwa ya kuanzisha mgogoro, mvutano au mapigano mapya katika eneo.'

Uingiliaji ghalati wa Marekani katika eneo katika miongo kadhaa iliyopita ulimpelekea Donald Trump kukiri kwamba licha ya nchi hiyo kutumia zaidi ya dola trilioni saba katika eneo lakini haikupata faida yoyote ya maana katika uwanja huo.

Uingiliaji wa Marekani Asia Magharibi uliongezeka kwa kiwango kikubwa hasa kufuatia tukio la Septemba 11 nchini humo, na uingiliaji wake katika nchi za Afghanistan, Iraq na Syria ulipelekea kubuniwa makundi hatari ya kigaidi yakiongozwa na Daesh. Marekani inadai kwamba inapambana na ugaidi wa kimataifa katika hali ambayo vitendo vyake vinathibitisha wazi kwamba yenyewe ndio mdhamini mkubwa wa makundi ya kigaidi duniani. Kwa hakika kila hatua ambayo imechukuliwa na Marekani kwa kisingizio cha kuleta amani katika eneo imezidisha tu madhara na matatizo ya nchi za eneo hilo.

Sehemu ya maadhimisho ya Bahman 22

 

Leo jamii ya kimataifa inakiri wazi nafasi haribifu ya serikali iliyopita ya Donald Trump katika kuvuruga usalama wa nchi za Asia Magharibi. Hali ya sasa ya nchi za Palestina, Iraq, Syria, Afghanistan na Yemen inathibitisha wazi matokeo ya siasa hizo mbovu za Washington kuhusu nchi za eneo katika miaka kadhaa iliyopita. Siasa za uingiliaji za nchi hiyo katika Ghuba ya Uajemi pia zina matokeo hayo hayo. Uwepo wa Marekani katika eneo hili unaweza kutathminiwa kuwa unafuatilia malengo matatu makuu:

Lengo la kwanza ni kuidhihirisha visivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kudai kuwa ndiyo inahatarisha usalama wa eneo.

La pili ni kuvuruga usalama wa eneo na kubuni muungano ulio dhidi ya Iran na wakati huo huo kuongeza vikwazo na mashinikizo ya kimataifa dhidi yake. Lengo la tatu ni kuanzisha changamoto na kuvuruga usalama ndani ya mipaka ya Iran. Baadhi ya nchi vibaraka wa Marekani katika eneo zinashirikiana kikamilifu na nchi hiyo ya Magharibi dhidi ya Iran bila kujali madhara ya siasa hizo mbovu kwa usalama wa eneo zima la Asia Magharibi.

Kwa hakika lengo la kistratijia la Marekani ni kuanzisha migogoro na mivutano ya kisiasa katika eneo, kuzuia ushirikiano wa kiusalama kati ya Iran na majirani zake na hatimaye kuzifanya nchi za Kiarabu za eneo ziwe tegemezi milele kwa jeshi la Marekani katika kujidhaminia usalama. Siasa hizo mbovu ziliwahi kutekelezwa na Uingereza hata kabla ya Marekani lakini matokeo yake yalikuwa ni kuibuliwa migawanyiko kati ya mataifa ya eneo hili na kuporwa utajiri wao na madola ya Magharibi. Hivi sasa Wamarekani wameingia katika mchezo mpya wa kuvuruga usalama wa eneo na kuzua uongo wa kuwepo tishio la Iran ili wapate kufikia lengo lao la eti kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz. Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuwa na uhusiano mzuri na majirani zake wote na ndio maana katika siasa zake za nje ikalipa umuhimu mkubwa suala la kuwa na uhusiano mzuri na uliosimama juu ya msingi wa kuheshimiana na kushirikiana pande zote na majira hao.

Rais Rouhani na Baraza la Mawazidi wakitangaza utiifu wao kwa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini MA kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 42 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Ikiwa ngome madhubuti dhidi ya ugaidi na utakfiri, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kivitendo nia yake hiyo njema katika nchi za Syria na Iraq ambapo kivitendo imezuia kuenea kwa makundi ya kigaidi katika nchi nyingine za dunia, na hivyo kuchangia pakubwa katika kudhamini amani na usalama wa kimataifa. Vile vile tokea kuvamiwa kijeshi nchi ya Yemen na maadui wa kigeni, Iran imewasilisha mipango kadhaa ya amani kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa nchi hiyo ambao unatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu katika karne hii ya 21.

Hakuna wakati wowote ambapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewahi kuanzisha vita katika eneo au nje ya eneo lakini pamoja na hayo ni wazi kuwa haitakaa kimya usalama wake utakapohatarishwa bali itatumia nguvu zake zote kukabiliana na tishio lolote la adui atakayejaribu kuhatarisha usalama huo. Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabiliana na vitisho viwe ni vya vita, ugaidi au uharamia wa baharini ni kuweka mikakati ya kuzuia mashambulio ya adui na kuondoa tishio lolote la adui katika mipaka yake.

Iran inaamini kwamba usalama wake ni usalama wa majirani zake na dunia nzima kwa ujumla na kwamba kupatikana usalama na maendeleo ya eneo kunawezekana tu kupitia ushirikiano wa majirani zake wote.