Feb 02, 2021 11:48 UTC
  • Sera ya

Makala hii itabainisha chimbuko na historia ya kaulimbiu na sera ya Si Mashariki, Si Magharibi katika mageuzi ya kifikra na kisiasa nchini Iran, duniani na katika mahubiri ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika Makala hii tutazungumzia moja ya kaulimbiu kuu na muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo inahusiana na kujitawala kitaifa Iran katika Zama za Vita Baridi za wakati wa enzi za kambi kuu kinzani za Mashariki na Magharibi. Kaulimbiu hii, ambayo imekuwa ndio msingi wa sera za nje za Iran katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ambayo imeweza kuifanya Iran taifa huru lisilo na utegemezi katika uga wa kimataifa ni "Si Mashariki, Si Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu". Tunachokusudia kuchambua katika mazungumzo yetu ni kujua kaulimbiu hii ilianzia wapi katika rai za wanafikra na wapigania uhuru wa Iran na ulimwenguni; na ilikuwaje mpaka ikawa moja ya matilaba na matakwa makuu ya wananchi wa Iran katika Mapinduzi ya Kiislamu? Endelea basi kunitegea sikio hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Tangu miaka karibu 500 iliyopita, yaani kuanzia zama za utawala wa Safawiyyah, ambapo mfumo wa Dola Taifa kwa kitaalamu Nation State kwa maana yake mpya ulikuwa umeshakuwepo nchini Iran, taifa hili lilianza taratibu kugeuka kuwa nukta ya mvuto kwa madola makubwa duniani. Umuhimu wa kistratejia wa Iran na kupanuka kwa mahusiano ya kimataifa katika zama hizo kulipelekea masuala ya siasa na sera za nje za Iran yavuke mpaka wa vita na suluhu na majirani zake na kujengewa aina maalumu ya mfungamano baina ya sera za nje za Iran na mfumo wa kimataifa. Maelewano hayo yalipanuka na kufikia upeo wa juu zaidi kuanzia miaka takriban miaka mbili iliyopita, yaani katika enzi za utawala wa Qajar. Katika kipindi hicho, madola mawili makubwa ya Urusi na Uingereza yalikuwa yakichuana vikali kupigania satua na ushawishi ndani ya Iran, huku serikali dhaifu ya wakati huo ya Iran, nayo pia ikijaribu kulinda usalama na uthabiti wake wa kisiasa kwa njia ya kujenga hali ya mlingano chanya baina ya madola mawili hayo na kuliridhisha kila moja kwa kulipatia baadhi ya fursa. Ushawishi na uingiliaji wa maajinabi, hususan madola mawili ya Urusi na Uingereza katika kipindi cha Qajar ulikuwa mkubwa, kiasi ambacho kukabiliana na maajinabi na kujitawala yaligeuka taratibu kuwa moja ya matilaba muhimu waliyopigania wananchi katika Mapinduzi ya Katiba; na madai hayo yakapata nguvu zaidi katika miaka ya baada yake hususan baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Katika kipindi hicho, licha ya serikali ya Iran kufuata sera ya kutoegemea upande wowote, lakini kutokana na uingiliaji wa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo, nchi hii iligeuzwa mhanga wa moto wa vita; na matokeo ya vita hivyo angamizi vya dunia, yalikuwa ni kuihilikisha na kuinakamisha Iran kwa janga kubwa la njaa lililoenea nchini, mripuko wa maradhi ya kipindupindu pamoja na hali mbaya sana ya uchumi na mvurugiko wa uthabiti wa kisiasa ulioiandama serikali na wananchi wake.

Mohammad Mosaddegh

Katika miaka ya baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, kutokana na kujitokeza mfumo wa kambi mbili na kuasisiwa mfumo mpya wa mlingano wa nguvu za kijeshi na kisiasa katika nidhamu ya kimataifa uliopewa jina la Vita Baridi, takriban nchi zote duniani zililazimika kuwa wanachama wa moja ya kambi mbili za Mashariki na Magharibi zilizokuwa zikiongozwa na Shirikisho la Kisovieti la Urusi na Marekani. Lakini sambamba na kupamba moto mapambano dhidi ya Ukoloni duniani, nchi kadhaa za Asia na Afrika ziliamua kwamba, ili kuweza kujivua na utegemezi wa kambi hizo mbili na wanaoziongoza, yaani Marekani na Urusi, zifuate siasa na sera huru na za kujitegemea katika mahusiano ya kimataifa. Kwa hivyo mnamo mwezi Aprili 1955, mkutano wa kwanza wa nchi za Asia na Afrika ulifanyika mjini Bandung Indonesia kwa madhumuni ya kuasisi kambi mpya ya kutojifungamanisha na upande wowote. Katika mkutano huo, wawakilishi wa nchi washiriki walimtaja Dakta Mohammad Mosaddegh, waziri mkuu wa serikali halali ya Iran, ambaye alichukiwa na Uingereza kwa kupigania kutaifishwa sekta ya mafuta ya nchi yake, na matokeo yake akaondoshwa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1953 yaliyotekelezwa kwa ushirikiano wa Marekani na Uingereza, kuwa ndio kiranja na mwasisi wa siasa za kutofungamana na upande wowote duniani na wakayaenzi mapambano yake dhidi ya ukoloni. Katika mkutano mwingine uliofanyika Septemba 1961 mjini Belgrade, Yugoslavia, nchi wanachama wa Vuguvugu la Kutofungamana na Siasa za Upande Wowote, yaani Non Alligned Movement NAM, zilitangaza kuwa, siasa na sera za mlingano hasi alizofuata na kutekeleza Dakta Mosaddiq katika kipindi cha harakati ya utaifishaji sekta ya mafuta na kupambana na Uingereza, ndizo watakazofuata wao. Kwa kufuata siasa hizo za mlingano hasi, waziri mkuu huyo wa Iran aliweza kukomesha uingiliaji wa madola makubwa nchini Iran na kutoa mfano wa kivitendo kwa wapigania uhuru duniani wa kutojifungamanisha na upande wowote katika ulimwengu wa wakati huo wa kambi mbili.

Viongozi wakuu wa Asia na Afrika walioshiriki mkutano wa Bandung

Kile ambacho katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kilitajwa kama kaulimbiu ya Si Mashariki, Si Magharibi, mbali na kuwa ni jambo linalotokana na mafunzo ya dini na Qur’ani, ambayo yanasisitiza kuepukana na utegemezi na kutokubali kutawaliwa; kwa upande wa kisiasa na kihistoria chimbuko lake ni siasa za mlingano hasi zilizofuatwa na kutekelezwa katika kipindi cha utaifishwaji wa sekta ya mafuta ambazo baadaye zikawa ni mfano wa kuigwa na nchi wanachama wa Vuguvugu la Kutofungamana Upande Wowote. Taifa la Iran liliamini kwamba, kuwa huru kitaifa katika kujitawala, na maajinabi kutoingilia masuala ya ndani ya nchi, ni haki ya kimaumbile na ya wazi kabisa ya mataifa yote; na kutokana na tajiriba ya kusikitisha ya kihistoria ya uingiliaji wa Urusi na Uingereza nchini Iran, taifa hili haliko tayari kurudi nyuma katika kupigania haki yake hiyo isiyo na shaka.Ijapokuwa sera za mlingano hasi za serikali halali ya Iran katika zama za mapambano ya kutaifisha sekta ya mafuta ilikuwa mfano mzuri sana wa kuigwa na nchi zilizokuwa zikinyongeshwa duniani kwa ajili ya kujitawala na kufuata siasa za kutofungamana na kambi za Mashariki na Magharibi, lakini mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1953, yaliyofanywa na Marekani ikishirikiana na Uingereza yalimfanya dikteta Mohammad Reza Shah abadilishe sera za nje za Iran kutoka zile za mlingano hasi wa kutofungamana na upande wowote na kuelekea kwenye utaifa chanya na mfungamano na madola ya Magharibi na hasa Marekani. Shah, ambaye aliamini kwamba kukalia kwake tena kiti cha ufalme kulitokana na hisani ya Marekani, alijiunga rasmi na kambi ya Magharibi; na kwa hatua yake ya kuipatia Marekani fursa chungu nzima za upendeleo wa kiuchumi, kisiasa na kisheria na kufunga nayo mikataba ya kijeshi na kiusalama, aliugeuza utawala wake kibaraka wa nchi hiyo na Magharibi. Kwa kutegemea uungaji mkono wa Marekani na kujifakharisha kwa donge nono la pato la mafuta na zana za kisasa za kijeshi na kiusalama alizonunua Marekani, Shah aliitawala nchi kwa mkono wa chuma na ukandamizaji mkubwa. Mbali na utawala wa kidikteta wa Mohammad Reza Shah kuifanya Iran ipoteze uhuru wake wa kujitawala na kuifanya tegemezi kwa madola ya Magharibi hususan Marekani, uliukaba pia uhuru wa kisiasa na kiraia na kuubadilisha utawala wa Katiba kuwa utawala mutlaki wa kifalme na kiimla, ambao ulimkandamiza na kumuangamiza kila aliyeupinga na kutoruhusu ukosoaji na upinzani wa aina yoyote.

Ilikuwa ni katika mazingira hayo, ndipo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipotokea chini ya uongozi wa Imam Khomeini na kwa lengo la kuhuisha uhuru na kujitawala kwa taifa la Iran. Kwa kuitangaza kaulimbiu ya Si Mashariki, Si Magharibi, Imam Khomeini aliweza kulifanya suala la kujitawala na kutokuwa na utegemezi kuwa moja ya mihimili mikuu ya mahubiri ya Mapinduzi ya Kiislamu na dira ya siasa na sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu.

Katika muendelezo wa hatua hiyo, misimamo ya Imam Khomeini ya kubainisha sera hiyo ikawa ndiyo msingi wa sera za nje za Iran ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ambapo katika ibara ya 152 ya katiba hiyo imefafanuliwa kuwa, kukataa ubeberu wa aina yoyote ile wa kuifanyia au kufanyiwa na nchi nyingine, kulinda umoja wa ardhi yote ya nchi pamoja uhuru na kujitawala kwa kila hali, kutetea haki za Waislamu wote, kutojifungamanisha na madola ya kibeberu na kuwa na uhusiano wa amani na wa kuheshimiana na nchi zisizoipiga vita, ndio msingi wa siasa na sera za nje za Iran. Msingi huu na kaulimbiu hii ya Si Mashariki, Si Magharibi, ambao umeandikwa pia kwenye bango la mlango mkuu wa kuingilia jengo la wizara ya mambo ya nje ya Iran, unadhihirisha jinsi Iran ilivyo huru katika uga wa kimataifa na inavyokataa kuburuzwa na kuwa tegemezi kwa nchi zingine hasa madola makuu ya Mashariki na Magharibi; lakini haumaanishi kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitaki kuwa na uhusiano mzuri na kwa msingi wa kuheshimiana na nchi zingine. Kwa maneno mengine ni kwamba, lengo kuu la kutekeleza sera ya "Si Mashariki, Si Magharibi, Jamhuri ya Kiislamu" ni kukataa ubeberu wa maajinabi; na si kukata mahusiano na nchi nyingine duniani.