Feb 06, 2021 07:36 UTC
  • Kusimama kidete Iran mbele ya vikwazo

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo wa vipindi hivi maalum vinavyokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Alfajiri Kumi kuelekea kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mpainduzi ya Kiislamu ya Iran.

Kipindi chetu cha leo kitajadili na kuzungumzi jinsi Iran ya Kiislamu ilivyosimama kidete mbele ya vikwazo vya madola ya kibeberu dhidi yake yakiongozwa na Marekani. Karibuni.

 

Vikwazo ni msamiati mashuhuri mno kwa wananchi wa Iran; lile lile taifa ambalo likiwa na lengo la kubadilisha mfumo wa kifalme wa utawala wa Shah uliokuwa kibaraka na tegemezi kwa Marekani, lilisimama na kuanzisha mapambano chini ya uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini (MA); na hatimaye mwaka 1979 kukaasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hapa nchini Iran baada ya mapinduzi ya Kiislamu kupata ushindi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilichomoza na kudhihiri ikiwa na nara na kaulimbiu yake ya kutokuwa tegemezi siyo kwa Magharibi wala Mashariki, na kuwatangazia mabeberu na waistikbari wote kwamba, mfumo huu utakua na kupata nguvu bila ya kuwa tegemezi si kwa madola ya Mashariki wala Magharibi; bali kwa kutegemea nguvu na hima ya vijana shupavu wa taifa hili hapa nchini na hivyo kuweza kusimama kwa miguu yake bila ya msaada wa yeyote kutoka nje.

 

Wananchi wa Iran wakiwa na lengo la kufikia mapinduzi ya Kiislamu walikuwa tayari kujitolea kwa hali, mali na hata roho na maisha yao. Tangu awali taifa la Iran liliandamwa na uadui na hasama ya Marekani na washirika wake kupitia njama mbalimbali kama vikwazo. Baada ya kutekwa na kudhibitiwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran uliokuwa umegeuzwa na kuwa Pango la Ujasusi na kutiwa mbaroni majasusi waliokuwamo humo na vijana wanamapianduzi, mashinikizo ya Marekani yalianza katika kalibu na fremu ya vikwazo.

Baada ya Marekani kupoteza tumaini lake la mwisho nchini Iran yaani Pango la Ujasusi lilililokuwa chini ya kivuli na pazia la ubalozi, haikuwa tena na ngome ya kuendeshea harakati zilizo dhidi ya mapinduzi nchini Iran. Ni kwa muktadha huo ndio maana, ikiwa na lengo la kuzuia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yasisonge mbele na kuchanua zaidi, ilikimbilia wenzo wa vikwazo na mashinikizo. Katika miaka yote hii ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ikisaidiana na washirika wake, Marekani imeliwekea taifa hili vikwazo vikali kabisa, ili kwa njia hiyo kama inavyojidanganya iweze kuvunja azma na irada ya wananchi na mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini. Na ikiwa na azma ya kufikia malengo yake haya ya kijinai dhidi ya Iran, serikali ya Marekani imekuwa ikitumia kila wenzo.

Vikwazo dhidi ya Iran (sanctions against Iran) ni majimui ya hatua za baadhi ya waitifaki wakiongozwa na Marekani, ambazo kwa uoni wao zinalenga kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuifanya isalimu amri na hivyo ikubaliane na matakwa yao ya kibeberu. Vikwazo maana yake ni kuzuia na kuinyima Iran fursa fulani na hivyo kukwamisha mfumo wa kiuchumi wa taifa hili na kama wanavyoota ndoto za alinacha wahusika, eti wausambaratishe kabisa uchumi wa taifa hili.

 

Vikwazo vya kwanza kabisa ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa ni katika miezi na miaka ya awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hata hivyo baada ya Iran kufanikiwa kumiliki teknolojia ya kisasa ya nishati ya nyuklia, vikwazo dhidi ya taifa hili vilichukua mkondo mpana zaidi. Licha ya kuwa kidhahiri vikwazo dhidi ya Iran vinagawanyika katika makundi manne ya vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vikwazo vya Umoja wa Ulaya, vikwazo vya upande mmoja vya mataifa mbalimbali kama Marekani na vikwazo vya Kongresi ya Marekani, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, vyote hivyo viliwekwa kwa uongozi na maelekezo au hata mashinikizo ya serikali ya Marekani.

 

Licha ya kuwa weledi wa mambo wanaamini kuwa, pamoja na vikwazo hivyo kuwa na baadhi ya taathira hasi katika kipindi cha muda mfupi, lakini kiujumla havijawa na taathira ya maana katika mwenendo wa ustawi wa kielimu na teknolojia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mbinu ya vikwazo, licha ya kuwa kwa kiwango fulani imepunguza ukuaji wa uchumi na sekta ya viwanda ya Iran na kupunguza pia uwekezaji wa kigeni hapa nchini, lakini hima na idili ya wanaume na wanawake wa Iran ya usiku na mchana ya kuasisi kigezo kipya  cha uchumi wa kimuqawama na kukataa utegemezi wa kigeni wa taifa, ni hatua ambazo zimekuwa na matunda mazuri mno.

Vikwazo dhidi ya Iran vilikuwa na taathira zake mbaya, lakini vimelifunza na kulionyesha taifa hili njia hii kwamba, linapaswa kujitegemea. Ni lazima kutegemea nguvukazi ya ndani pamoja na vipawa na vipaji vya vijana wa taifa hili humu nchini; na hivyo kuwatumia kwa ajili ya kukwea daraja za ustawi na maendeleo ya taifa. Ni kwa msingi huo, ndio maana taifa la Iran baada ya kuandamwa na vikwazo, badala ya kusalimu amri na kukubali kudhalilishwa, likaamua kuchagua njia ya kujitegemea kwa kutegemea wasomi vijana na watalaamu wenye vipawa hapa nchini kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la ustawi.

 

Hii leo walimwengu ni masuhuda wa jinsi Iran ilivyopiga hatua na kung’ara kielimu hata katika majukwaa ya kimataifa. Hii leo, ustawi na maendeleo ya kuelimu, kiteknolojia, kiviwanda, kijeshi na kitiba ya Iran hususan katika miongo mitatu ya hivi karibuni, yanafahamika na kila mtu na kuwa fakhari ya taifa hili la Kiislamu ambalo mwanzoni mwa kudhihiri na kuchomoza kwake, liliandamwa na kukabiliwa na vikwazo vikali vya kila upande.

Kuhusiana na hili, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema: “Maadui waliliwekea mbinyo taifa letu katika kila nyanja za kiuchumi na walililokuwa wakilifuatilia ni kuliwekea vikwazo; na lengo lao hasa lilikuwa ni kuhakikisha wanalipigisha magoti taifa la Iran, wanaupigisha magoti mfumo unaotawala hapa nchini; lakini mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ukipata msaada wa subira, busuri na muono wenu wa mbali nyinyi wananchi, umeweza kuzipigisha magoti siasa zile na wapangaji wa siasa hizo. Sisi tumeweza kutumia vizuri vikwazo hivi na kuvibadilisha kuwa fursa. Hii hii hali ya kusimama kidete na kukabilian na vikwazo, imekuwa sababu ya sisi kupiga hatua katika medani ya ubunifu, uvumbuzi wa kielimu na ustawi katika medani na nyuga zote, ambapo mataifa ya eneo hili katika kipindi cha miaka yote hii, hayajaweza kufikia maendeleo haya.”

Mtu wa kwanza kujitolea kudungwa chanjo wa Corona nchini Iran

 

 

Kutengeneza Satalaiti ya Omid na kuituma katika anga za mbali, kufanikiwa kufikia elimu ya seli shina na matumizi yake, kutengeza suhula na zana za kijeshi za kisasa, hususan makombora ya ardhini kwa baharini ya masafa marefu, kufikia teknojia ya nyuklia, kukamilisha mzunguko wa utegenezaji fueli ya nyuklia katika maabara, kupandikiza kwa mafanikio viungo vya mwili wa mwanadamu kama moyo, na kufanikiwa kufikia teknolojia ya Nano na kukwea nafasi ya kielimu katika orodha ya dunia, ni baadhi tu ya mafanikio ya Iran ambayo yamepatikana katika kipindi cha vikwazo. 

Nafasi na mchango wa teknolojia ya Nano hasa katika sekta ya afya hususan katika kipindi cha kuenea virusi vya Corona ulidhihirika na kuonekana zaidi. Kwa msaada wa teknolojia hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kudhamini mahitaji yake muhimu kama barakoa na mashine za kusaidia kupumua wagonjwa walio na hali mbaya, vyote hivyo vikiwa vinazalishwa hapa hapa nchini. Aidha hivi sasa uzalishaji wa chanjo ya corona unaofanywa na wataalamu wa Kiirani umepita kwa salama kabisa hatua ya majaribio ya kumdunga mwanadamu na kuna habari njema zinazoripotiwa katika uwanja huo. 

Akizungumzia maendeleo makubwa ya kielimu ya Iran yaliyopatikana hapa nchini kwa hima na juhudi za vijana wenye vipawa wa Kiirani, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasema: Ari na moyo wa kimapinduzi, kitaifa na Kiislamu wa kizazi cha vijana hapa nchini, umekuwa na nafasi na mchango mkubwa mno katika kupanua na kustawisha teknolojia ikiwemo teknolojia ya nano, bioteknolojia na nyuklia, na hali hii inapaswa kuongezwa na kuimarishwa zaidi. 

 

Kwa hakika vikwazo kwa taifa kama Iran ambalo limechagua njia ya maendeleo na ustawi sio kizingiti bali ni fursa kwa ajili ya kufanya hima na juhudi zaidi. 

Aidha hii leo, vifaa, zana na suhula za kisasa kabisa za kijeshi zilizotengenezwa na vijana mahiri na wenye vipawa wa Kiirani, ni jambo ambalo linafahamika na wote. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza mara chungu nzima kwamba, lengo la kutengeneza zana na silaha za kisasa, ni kwa ajili ya kujilinda na kujihami na kuinua kiwango cha amani na usalama katika eneo, na katu Iran haikuwa na haitakuwa muanzishaji wa vita. Lakini kama itashambuliwa, itatoa jibu kali litakalomfanya adui ajute kwa kosa lake hilo na kuwa funzo pia kwa wengine.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo, umefikia tamati. Tukutake tena wakati mwingine. Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Tags