Feb 07, 2021 06:55 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu katika njia ya kuhuisha ustaarabu wa Kiislamu

Licha ya kupitia milima na mabonde mengi, lakini kufikia sasa Jamhuri ya Kiislamu imefanikiwa kulinda nafasi na itibari yake ndani na nje ya nchi na ikiwa inaingia katika mwaka wake wa 42, imeongeza kasi yake kuelekea ustaarabu mpya wa Kiislamu.

Sambamba na kuwadia siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo ni tarehe 22 Bahman (10 Februari), tunakuombeni muwe pamoja nasi ili tupate kusikiliza na kunufaika na yale tuliyokuandalieni katika kipindi hiki maalumu, karibuni.

*********************

Katika kipindi chote cha historia ya mwanadamu, kumedhihiri mapinduzi mengi katika pembe tofauti za dunia ambapo baada ya mapinduzi hayo kung'ara kwa muda mfupi na kufikia malengo yaliyokusudiwa, yalidhoofika na hatimaye kutoweka. Ustaarabu kama vile wa Iran, Baina Nahrain nchini Iraq, Ugiriki, Roma, Misri na China zote hizo zilikuwa na huduma muhimu katika maendeleo ya kielimu na kiutamaduni ya mwanadamu. Kati ya staarabu hizo zote, ni ustaarabu wa Kiislamu pekee ambao ulienea na kuwa na matunda makubwa mara tu baada ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu, ndio uliokuwa na umuhimu na ubora mkubwa zaidi ukilinganishwa na staraabu nyinginezo.

Utamaduni huo ambao ulisimama juu ya msingi wa mafundisho ya Kiislamu, ulimsisitizia mwanadamu kutafuta elimu katika kila pembe ya dunia, tokea siku ya kuzaliwa kwake hadi siku ya kuaga kwake dunia. Ni kutokana na sisitizo hilio ndipo kukadhihiri wasomi na wanafikra wakubwa waliobobea katika nyanja mbali mbali za sayansi, uvumbuzi, ubunifu, historia, falsafa, utungaji mashairi na usanii. Kwa bahati mbaya jua la mwangaza wa ustaarabu wa Kiislamu lilianza kutua taratibu kutokana na sababu mbali mbali za ndani na nje na hivyo kuanza kuingia zama za kubakia nyuma kielimu na kiutamduni na wakatika huo huo ukoloni wa Wamagharibi ukanza kupenya na kukita mizizi katika ulimwengu wa Kiislamu.

kiUstawi wa sayansi katika ustaarabu wa Kiislamu


Kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mnamo Februari 1979, msisimuko na matumaini mapya ya kuhuishwa fikra na utamaduni wa Kiislamu yaliibuka nchini. Baadhi ya mambo na viashiria vya ustaarabu wa Kiislamu kama vile ustaawi wa umaanawi, maendeleo ya kielimu, kutegemewa nguvukazi na wanafikra wanaofaa wa ndani ya nchi, kuimarishwa uwezo wa kitaifa na kufanyika juhudi za kuunganisha ulimwengu wa Kiislamu, viliiweka Iran katika njia sahihi ya kuhuisha ustaarabu wa Kislamu. Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kwamba njia halisi ya mapinduzi haya makubwa inapasa kuyafikisha katika ustaarabu wa  Kiislamu wa kisasa.

Katika kipindi chote cha zaidi ya miungo minne ya umri wake wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini, maadui wamekuwa wakifanya njama nyingi za kuusababishaia matatizo mengi kwa ajili ya kuufuta kabisa au kwa uchache kupotosha njia yake. Lakini licha ya kuwepo milima, mabonde na changamoto mbali mbali, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelinda na kuimarisha nafasi na itibari yake ndani na nje ya nchi, na kuongeza kasi yake kuelekea ustaarabu mpya wa Kiislamu.

Ni kutokana na ukweli huo ndipo katika taarifa yake ya 'Hatua ya Pili' aliyoitoa kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 40 wa Mapinduzi ya Kiislamu, Kiongozi Muadhamu aliwahutubu vijana kwa kusema: "Miongo inayokuja ni miongo yenu. Huku mkiwa wasomi wenye hamu kubwa, mnapasa kuyafuata Mapinduzi yenu na kuyakurubisha na lengo lake kuu ambalo ni kufikia ustaarabu mpya wa Kiislamu na hivyo kujiweka tayari kwa ajili ya kuchomoza jua la 'Wilaya Kuu'."

Kwa maneno mengine ni kuwa, Kiongozi Muadhamu anazichukulia zama hizi kuwa ni zama nzuri zaidi za kuhuishwa ustaarabu wa Kiislamu na kutayarishwa mazingira ya kudhihiri Imam Mahdi (af).


Ili kufanikisha ustaarabu wowote ule, utangulizi na mipango inayofaa inapaswa kuandaliwa. Hata kama kazi hiyo ni ngumu na inayochukua muda mrefu lakini ni wazi kuwa matunda yake huwa ni makubwa na ya kuvutia. Moja ya viashiria muhimu vya kila ustaarabu ni utamaduni na fikra zake. Kinyume na ulivyo ustaarabu wa nchi za Magharibi, ustaarabu wa Kiislamu umesimama juu ya msingi wa umaanawi, maadili mema na imani juu ya Mwenyezi Mungu mmoja. Ustaarabu wa aina hii huwa haukanyagi haki za mataifa mengine, kutumia elimu vibaya, kimaslahi na kwa njia za haramu wala kuzuia mataifa mengine kunufaika na elimu hiyo kwa ajili tu ya kujistawisha yenyewe.

Kwa msingi huo, moyo unaotawala katika ustaarabu wa Kiislamu ni moyo wa kiungu na kimaanawi. Kwa maelezo hayo na kama linavyoashiria jina lake lenyewe, Mapinduzi ya Kiislamu ni mapinduzi ambayo yamesimama juu ya msingi wa mafundisho matukufu ya Uislamu na yenye malengo matukufu ambayo yanalenga kumletea mwanadamu saada ya mtu binafsi na ya kijamii katika pande zote mbili za kimaanawi na kimaasa. Kuhusu hilo Ayatullah Khamenei anasema: "Katika ustaarabu mpya wa Kiislamu, umaanawi huandamana na umaada, maadili na unyenyekevu sambamba na kufikiwa ustawi wa kimaada wa mwanadamu."

Hii leo watu wengi katika mataifa mengi ya dunia wanakubali na kupokea vyema fikra hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuandaa uwanja unaofaa kwa ajili ya kuhuishwa ustaarabu mpya wa Kiislamu duniani. Moja ya sifa za kimsingi za kila ustaarabu ni maendeleo yake ya kielimu na kiteknolojia. Tokea mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na licha ya kutwishwa vita haribifu vya miaka minane pamoja na vikwazo vya kila upande kutoka nchi adui za Magharibi lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua muhimu katika uwanja huo. Kwa kuwa na ustawi wa asilimia 10, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya pili duniani baada ya China, kuwa na kasi ya kiwango hicho cha ustawi wa kielimu ulimwenguni.

Ni ya nne duniani katika uwanja wa ustawi wa teknolojia na pia ni miongoni mwa nchi zilizo mstari wa mbele katika nyanja mbalimbali za teknolojia ya nyuklia, selishina, tiba, uundaji wa zana za kijeshi za kisasa na hasa makombora na ndege zisizokuwa na rubani (droni). Bila shaka maendeleo hayo makubwa ya kielimu na kitekolojia yamepatikana kutokana na kuwepo miundomsingi ya dharura nchini. Katika umri wake wa miaka 42 Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeandaa mazingira yanayofaa ya kielimu na kisayansi nchini na wananchi wake na hasa tabaka la vijana wameonyesha hamu kubwa ya kufuatilia masuala ya kielimu nchini.

Kiwango cha kujua kusoma na kuandika kimeongezeka kwa kiwango kikubwa nchini ambapo kwa wastani sasa kuna karibu wanachuo milioni nne katika vyuo vikuu hapa nchini. Kuwepo kwa idadi hiyo kubwa ya wanachuo nchini bila shaka kumeiweka Iran katika nafasi nzuri ya kunufaika na wataalamu wa ndani na wenye uzoefu mkubwa katika nyanya mbali mbali za kielimu na kiteknolohia nchini. Ni kutokana na suala hilo ndipo ikatabiriwa kwamba katika miaka michache ijayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kunufaika na wasomi na wanasayansi wa ndani watakaohudumu katika nyanja mbalimbali za kielimu na kiteknolojia kwa manufaa na maendeleo ya taifa zima la Iran.

Utafiti wa wanasayansi wa Iran

Kwa kawaida staarabu huwa zinakabiliwa na vitisho vya nje na mashambulio ya kijeshi na hatimaye kudhoofishwa au kusambaratishwa kabisa. Kwa mfano ustaarabu wa Kiislamu ulipata pigo kubwa kutokana na mashambulio ya msalaba ya Wakristo wa Ulaya, mashambulio ambayo yalianza takriban kwa wakati mmoja na mashambulio ya wa Wamogholi kutokea upande wa Mashariki. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inataka kuanzisha ustaarabu mpya wa Kiislamu, tokea mwanzo wa kudhihiri kwake ilikabiliwa na tishio kubwa na hata kukumbwa na mashambulio ya kijeshi ya maadui. Kwa msingi huo majeshi ya Iran yametayarishwa kwa namna ambayo yako tayari wakati wowote ule kuilinda nchi na ustaarabu wa Kiislamu.

Nchi dhaifu na tegemezi ambayo haina uwezo wa kujitetea wala kusimama mbele ya uchokozi wa kijeshi wa adui, haiwezi kuwa na matumaini ya kuandaa mazingira yanayofaa ya kudhihiri ustaarabu mkubwa na unaong'ara.

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, kinyume na zilivyo staarabu za nchi za Magharibi na staarabu nyingine za kale, kuimarika na kuenea kwa ustaarabu mpya wa Kiislamu, hakutegemei vita na kutekwa ardhi za mataifa mengine bali hufungua njia na kuingia kwenye mataifa mengine kupitia fikra na itikadi za hali ya juu na zinazotegemea utamaduni uliojengeka kwenye misingi ya mafundisho ya kidini. Hii ndio maana Iran ikawa inakabiliwa na wimbi kali la hujuma na propaganda potofu za maadui wa Magharibi.

Kama anavyoamini Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mfumo huu wa Kiislamu unaandaa mazingira ya kudhihiri Mwokozi wa Dunia, Imam Mahdi (af). Ustaarabu wa Kiislamu ulokamilika na mpana zaidi pia utaweza tu kupatikana katika zama za mtukufu huyo, na jambo hilo limebainishwa wazi katika 'Hatua ya Pili ya Mapinduzi ya Kiislamu' ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu. Hii ni kwa sababu katika zama za Imam huyo mtukufu ulimwengu mzima utaishi katika mazingira ya hali ya juu ya utulivu na uadilifu, usalama na umaanawi, udugu na utu na elimu na teknolojia kwa kadiri kwamba wanadamu wote watafaidika na kunufaika kwa njia bora zaidi na neema watakazokuwa nazo.

Kwa mara nyingine tena tunakupongezeni nyote wasikilizaji wetu wapendwa na wapenzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba huu adhimu wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Tunakuageni nyote huku tukitumai kwamba Mwenyezi Mungu atazidi kuyajalia mapinduzi haya yakaribie zaidi malengo yake matukufu kwa manufaa ya Waislamu wote ulimwenguni, kwaherini.

Tags