Mar 01, 2021 09:53 UTC
  • Kubadilishwa Kibla cha Waislamu, Tukio Kubwa na Muhimu

Tukio la kubadilishwa kibla cha Waislamu kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Masjidul Haram linahesabiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa na yenye taathira kubwa sana katika historia ya Uislamu ambalo pia lilikuwa na athari nyingi za kustaajabisha.

Ulikuwa umepita muda Mtume Muhammad (saw) akiangalia mbingu na kuonekana kama mtu anayesubiri jambo adhimu na muhimu sana. Mtukufu huyo alionekana kama mtu anayesubiri jambo jipya katika suala makhsusi lililokuwa likimtia wasiwasi. Hatimaye Malaika wa Wahyi na Ufunuo, Jibrilu (as) aliteremka kwa Mtume (saw) katika siku ya tarehe 15 Rajab mwaka wa pili Hijria na kumuondolea wasiwasi wake. Malaika Jibrilu alimwambia Mtume kwamba: Kwa yakini tunakuona unavyogeuza geuza uso wako mbinguni. Basi tutakuelekeza kwenye kibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu, na popote mnapokuwa zielekezeni nyuso zenu upande huo. Na hakika wale waliopewa Kitabu wanajua kwamba, hiyo ni haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda. (Baqarah-144)  

Naam, Mtume Muhammad (saw) alitaka kubadilishwa kibla kutoka Baitul Muqaddas na kuelekezwa Masjidul Haram, na Mwenyezi Mungu SW alikubali na kutekeleza ombi hilo la Mtume Wake wa Mwisho. Nukta ya kuvutia ni kwamba, ََAya hiyo iliteremshwa wakati Mtume (saw) alipokuwa katikati ya Swala ya Adhuhuri katika Msikiti wa Banii Salim bin Auf. Mtume alikuwa tayari ameswali rakaa mbili za Swala hiyo akielekea Baitul Muqaddas na akakamilisha rakaa mbili za mwisho akiwa ameelekea Makkah. Kwa sababu hii msikiti huo ulipewa jina la Dhul Qiblatain kwa maana ya msikiti wenye kibla mbili.

Masjid al Haram na al Kaaba, Kibla cha hivi sasa cha Waislamu wote

 

Hapa inapaswa kueleweka kwamba, kuelekea upande makhsusi kama kibla hakuna maana kwamba Mwenyezi Mungu SW yuko upande huo pekee, la hasha, bali Yeye, Jalla Waalaa, yuko kila mahala kama inavyotwambia Qur'ani tukufu kwamba: Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnakoelekea, huko Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa na Mjuzi. (Baqarah:115) Hivyo kubadilishwa kibla ni kwa ajili ya kuwafanya Waislamu wawe na kituo makhsusi kwa ajili yao, hususan wakati wa ibada ya Swala, na wote waelekee huko. Hatua hiyo ilizidisha moyo wa umoja na mshikamano kati ya wafuasi wa dini ya Uislamu na kukurubisha zaidi nyoyo zao. Hisia hii ya umoja na ushirikeli huonekana zaidi wakati wa ibada ya Hija pindi mahujaji wote wanapozunguka kituo kimoja yaani al Kaaba. Mfasiri mkubwa wa Qur'ani tukufu, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai anasema kuhusu athari za kijamii za kibla katika tafsiri yake ya al Mizan kwamba: Faida za kijamii za al Kaaba ni za kustaajabisha, athari zake ziko wazi zaidi na ni za kuvutia. Ni kuwaelekeza watu wote, licha ya hitilafu zao zote za zama na maeneo yao tofauti, katika eneo na nukta moja na kudhihirisha umoja na mshikamano wao wa kifikra, mfungamano wa jamii zao na mshikamano wa nyoyo zao kwa kuwaelekeza katika nukta na upande mmoja. Hii ndiyo roho bora zaidi inayoweza kupulizwa na kuwekwa katika kiwiliwili cha binadamu", mwisho wa kunukuu.

Kumetolewa maswali kadhaa kuhusu sababu za kubadilishwa kibla katika mwaka wa pili Hijria. Miongoni mwa maswali hayo ni kwamba, ni kwa nini hapo mwanzoni kibla cha Waislamu kikawa Baitul Muqaddas? Ni kwa nini Mtume Muhammad (saw) aliomba kubadilishwa kibla na kuelekea Makkah baada ya Waislamu kutekeleza Swala zao wakielekea Baitul Muqaddas kwa kipindi cha miaka 14 na nusu?

Wanahistoria wengi wameandika kuwa, wakati Waislamu walipokuwa Makkah kibla chao kilikuwa Baitul Muqaddas, kwa sababu wakati huo washirikina walikuwa wakiweka masanamu yao ndani ya al Kaaba na kuyaabudu au kufanya ibada zao wakielekea kwenye masanamu hayo. Hivyo, ili kujitenga na waabudu masanamu, Waislamu walijiepusha kuswali wakielekea kwenye masanamu hayo na wakaamrishwa na Mwenyezi Mungu kuelekea Baitul Muqaddas wakati wa kutekeleza ibada hiyo. Mji huo ulikuwa kibla na kituo cha dini za mbinguni na baadhi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu waliufanya kituo kikuu cha kueneza Tauhidi na itikadi ya Mungu Mmoja. Vilevile Msikiti wa al Aqsa katika mji wa Baitul Muqaddas, kihistoria, lilikuwa eneo la pili kujengwa duniani kwa ajili ya ibada za watu wanaompwekesha Mwenyezi Mungu baada ya Masjidul Haram huko Makkah.

Msikiti wa al Aqsa, Palestina, Kibla cha Kwanza cha Waislamu hivi sasa kinakaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Ni wajibu wa kisheria wa Waislamu kusaidiana na Wapalestina kukikomboa

 

Baada ya Mtume (saw) na masahaba zake kuhamia Madina hali ilibadilika kabisa. Katika mji huo hakukuwa na washirikina na waabudu masanamu wengi kama ilivyokuwa Makkah. Hata hivyo Mayahudi waliokuwa wakiishi kandokando ya Madina daima walikuwa wakitafuta vijisababu vya kuukosoa na kuutia doa Uislamu. Walikuwa wakisema kwamba, Mtume wa Uislamu anaswali akielekea kwenye kibla chao licha ya kuwapinga. Kebehi na maudhi hayo yaliendelea na kushadidi zaidi hadi Mtume Muhammad (saw) akaomba kubadilishwa kibla na kuelekea Makkah, eneo ambalo ni takatifu zaidi lililojengwa na Nabii Adam na baadaye likajengwa tena na Nabii Ibrahim akisaidia na mwanaye, Ismail kisha wakaswali kuelekea kwenye nyumba hiyo. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 96 ya Suratu Aal Imran kwamba: Hakika Nyumba ya kwanza waliowekewa watu kwa ibada ni ile iliyoko Bakka, iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote. Hivi ndivyo ilivyotolewa hukumu ya kubadilishwa kibla kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili wafuasi wa Uislamu kama dini ya Mwisho ya Mwenyezi Mungu, wapate kujitawala na kuwa na utambulisho. Mwenyezi Mungu pia anasema katika aya ya 149 ya Suratul Baqarah kwamba: Na popote wendako elekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na hiyo ndiyo haki itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayoyatenda. 

Ni wazi kuwa, baada ya kubadilishwa kibla, kebehi na chokochoko za wapinzani hususan Mayahudi zingeongezeka. Walikuwa wakisema, kama kufanya ibada kwa kuelekea Baitul Muqaddas ni jambo sahihi basi kwa nini mumebadilisha kibla? Na kama al Kaaba ndiyo kibla halisi na cha kweli, kwa nini huko nyuma mlikuwa mkielekea Baitul Muqaddas wakati wa kufanya ibada zenu? Jambo la kuvutia ni kwamba, tangu mwanzoni mwa kuteremshwa aya za kubadilishwa kibla, Qur'ani tukufu ilijibu chokochoko na kebehi za Mayahudi na wapinzani wa Uislamu. Miongoni mwa majibu ya Qur'ani kwa Mayahudi hao ni yale yaliyomo katika aya ya 142 ya Suratul Baqarah inayosema: WAPUMBAVU miongoni mwa watu watasema: Nini kilichowageuza kutoka kibla chao walichokuwa wakikielekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka. Kwa utaratibu huo Mwenyezi Mungu SW anasema kuwa, dunia yote ni mali na milki yake Yeye, na wakati wowote anaweza kuchagua eneo lolote kuwa kibla cha wale wanaompwekesha na kumwabudu Yeye tu.

Kibla cha Kwanza cha Waislamu katika muonekano mwingine

 

Katika aya mbili zinazofuatia za sura hiyo hiyo, Qur'ani inaendelea kutoa mwanga zaidi kwa walimwengu na kusisitiza kuwa, Ahlul Kitab, kwa maana ya Mayahudi na Manasara, wanajua vyema kwamba suala la kubadilishwa kibla cha Waislamu ni haki na kweli, kwa sababu wamesoma katika vitabu vyao kwamba, Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu ataswali kwa kuelekea kwenye kibla mbili, lakini hawakuwa tayari kuweka wazi ukweli huo na kukiri kwamba, Muhammad (saw) amekuja na haki na kweli yote.

Suala la kubadilishwa kibla kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makkah lilikuwa na taathira nyingi chanya kwa Umma wa Kiislamu. Huenda taathira kubwa zaidi ya tukio hilo ni kuwapa izza na utambulisho makhsusi Waislamu. Sasa walikuwa wamepata kibla chao wenyewe na walitakiwa kufanya ibada ya Swala kwa kuelekea kwenye kibla hicho. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, miaka 6 baada ya tukio hilo, wakati wa Fat'hu Makka, yaani wakati wa kukombolewa mji huo mtakatifu, Mtume Muhammad (saw) alivunja masanamu yaliyokuwa ndani ya al Kaaba, na tangu wakati huo Waislamu wakawa wanaswali kuelekea kwenye nyumba hiyo na Mwenyezi Mungu kwa amani na utulivu mkubwa zaidi.

Katika upande mwingine, tukio la kubadilishwa kibla ulikuwa mtihani na majaribio kwa baadhi ya Waislamu ambao awali walikuwa Wakristo au Mayahudi na baada ya kusilimu hawakupendelea kuswali wakielekea Masjidul Haram. Vivyo hivyo lilikuwa mtihani na majaribio kwa Waislamu wapya wa mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu ambao walikuwa na mfungamano makhsusi na al Kaaba na hawakuwa wakipendelea kufanya ibada ya Swala wakielekea Baitul Muqaddas. Hali zote mbili, yaani kuamrishwa kuelekea Baitul Muqaddas mwanzoni mwa kudhihiri Uislamu na baadaye kubadilishwa kibla ya kuelekezwa Makkah, zilionesha kiwango cha jinsi Waislamu walivyoshikamana na kuheshimu amri za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.

Kibla cha Kwanza na cha Pili cha Waislamu

 

Mbali na hayo, kuainishwa al Kaaba kuwa kibla, eneo ambalo ndio kituo cha kale zaidi cha ibada ya Mungu Mmoja na kambi kuu ya ulinganiaji wa Mitume kama Ibrahim na Ismail (as), ilikuwa fahari kubwa iliyowapa mori Waislamu. Hatua hiyo pia ilitayarisha mazingira mazuri ya watu wa bara Arabu waliokuwa wakiipa heshima maalumu al Kaaba, kukubali dini mpya ya Uislamu.  

Hapa inatupasa kuweka wazi kwamba, kubadilishwa kibla kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Masjidul Haram hakuna maana ya kupungua umuhimu wa Msikiti wa al Aqsa. Katika aya ya kwanza ya Suratul Israa, Qur'ani tukufu inaeleza umuhimu wa msikiti huo, na Waislamu daima walilipa heshima na umuhimu mkubwa eneo hilo takaifu ambalo ni dhihirisho la Tauhidi na mapambano dhidi ya dhulma ya Mitume wa Mwenyezi Mungu katika vipindi na nyakati mbalimbali. Waislamu wanautambua Msikiti wa al Aqsa kuwa ni kibla chao cha kwanza na eneo alikotokea Mtume Muhammad (saw) akielekea mbinguni katika tukio la Miiraji. Kwa msingi huo Waislamu wote wanajua kwamba, ni wadhifa na wajibu wao kulilinda eneo hilo tukufu na kulikomboa kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndiyo maana Waislamu wamekuwa wakiwakosoa vikali watawala wa nchi za Kiarabu na za Kiislamu kutokana na kuzembea kwao katika suala la kukomboa Msikiti wa al Aqsa unaoendelea kuharibiwa na kuvunjiwa heshima na Wazayuni wa Israel.

Hapana shaka kuwa, kubadilishwa kibla cha Waislamu lilikuwa tukio muhimu katika historia ya Uislamu ambalo miongoni mwa matunda yake makubwa ni kuimarisha umoja na mshimakano wa Kiislamu. Kwa msingi huo inaeleweka wazi kwamba, wale wanaopiga ngoma za kuzusha hitilafu na mifarakano katika Umma wa Kiislamu bado hawajaelewa maana ya Waislamu wote duniani kuwa na kibla na mwelekeo mmoja na kufanya ibada zao wakielekea upande mmoja wa kituo cha Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu SW.                 

Tags