Apr 24, 2021 09:37 UTC
  • Kifo cha Bibi Khadija (as), mke mwema na kipenzi cha Mtume Muhammad (saw)

Siku hiyo maradhi yalimzidia Bibi Khadija binti Khuwailid. Alikuwa akitafakari kuhusu njia ndefu iliyokuwa mbele yake.

Mashaka ya kutengana na kipenzi, habibi na kiongozi wake aliyeishi naye katika vipindi vya shida na raha, yalikuwa yakimzonga zaidi. Maradhi yalikuwa yakizidi kumuumiza na taratibu alianza kupoteza fahamu na kuzinduka. Mtume Muhammad (saw) ambaye alikuwa akiishuhudia mandhari hiyo ya kuhuzunisha na mashaka ya kipenzi chake, Bibi Khadija, alimsogelea karibu zaidi na kumnong'oneza sikio akisema: "Karibuni utakuwa mgeni wa wanawake wateule, wape salamu zangu."

Maneno hayo yalimpa Bibi Khadija uhai mpya. Alipepesa mboni za macho na kuonekana mwenye furaha na bashasha, kisha akamuuliza Mtume (saw) kwamba: Hao wanawake uliosema ni kina nani? Mtume (saw) alijibu kwamba: Ni Maryam, mama yake Issa, Kulthum dada yake Mussa, Asia mke wa Firauni na...  Hapa Bibi Khadija hakuweza tena kusikia lolote. Aliwakumbuka mashoga zake waliokuwa pamoja naye wakati wa kuzaliwa binti yake kipenzi, Fatimatu Zahra na akatamani kukutana nao kwa mara ya mwisho. Katika upande mwingine maneno ya Mtume Muhammad (saw) yalimtia Bibi Khadija shauku kubwa ya kuingia Peponi.

Tarehe 10 Ramadhani inakumbusha siku chungu ya kufariki dunia mwanamke adhimu, mtukufu, kipenzi na mke mwema wa Mtume wetu Muhammad (saw), Bibi Khadija (as). Mwanamke ambaye kwa hakika alikuwa na mtukufu huyo katika vipindi vyote vya raha na mashaka na alimsaidia Mtume katika njia iliyojaa misukosuko na vizingiti vingi ya kutangaza ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Mtume (saw) alimtambua Bibi Khadija kama waziri na shauri wake, na alitumia vyema busara na hekima zake, kujitolea na ukarimu wake. Mtume (saw) anasema kuhusu kujitolea kwa bibi huyo mwema kwamba: "Mwenyezi Mungu amrehemu Khadija. Aliniamini wakati watu wengine waliponikadhibisha. Aliniunga mkono wakati watu wengine waliponipiga vita. Akanipa mali yake wakati nilipokuwa bila mali." 

Bibi Khadija alikuwa mwanamke mwaminifu ambaye alisabilia mali yake yote kwa ajili ya Uislamu na kuiweka katika mikono ya mumewe. Alikuwa mwenza na msaidizi mkubwa sana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu katika zama za upweke na kutengwa kwake. Alijihisi kuwa katika dunia iliyojaa amani kandokando ya mume wake mtukufu na alimsaidia katika harakati zote za kutimiza malengo yake. Wakati Malaika wa Wahyi, Jibril (as) alipoteremka kwa Mtume (saw) na kumkabidhi jukumu zito la kuongoza wanadamu, Bibi Khadija (as) alikuwa wa kwanza kusadikisha maneno yake na alikuwa mwanamke wa kwanza kukubali dini ya Uislamu. Mtume (saw) anasema kuhusiana na suala hili kwamba: "Mwanamke wa kwanza duniani kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni Khadija." 

Bibi Khadija alikuwa na mchango mkubwa katika kukua na kustawi dini changa ya Uislamu katika kipindi hicho kilichokua na mashaka na misukosuko mingi. Alitetea dini hiyo na ujumbe wa Mtume kwa hali na mali yake yote. Wakati wote Mtume alipokuwa akikabiliana na adha na maudhi ya washirikina, Bibi Khadija (as) alikuwa akimpa moyo wa mustakbali mwema kwa upendo, mahaba na mapenzi yake. Alifanya jitihada za kubadilisha mashaka na machungu hayo ya Mtume katika njia ya kulingania ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kujaza furaha na bashasha katika maisha ya mtukufu huyo. Ibn Hajar al Asqalani ambaye ni miongoni mwa maulama wa Ahlusunna ameandika kuwa: Miongoni mwa sifa nzuri za Bibi Khadija ni kwamba, daima alimtukuza Mtume na kusadikisha maneno yake kabda na baada ya kubaathiwa na kupewa utume."  

Miongoni mwa majina ya Bibi huyu mwema ni "al Mubarakah" kwa maana ya mwanamke aliyepewa baraka nyingi. Mwanazuoni wa Hadithi wa Kiislamu, marehemu Sheikh Abbas Qummi ameandika kuwa: Imenukuliwa katika ujumbe Mwenyezi Mungu aliomtumia Nabii Issa Masih kuhusu nafasi ya juu ya Bibi Khadija mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba yeye ni mbarikiwa na mwenza wa Bibi Maryam huko Peponi. Imepokewa pia katika Injili katika kifungu kinachoeleza sifa za Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu kwamba: "Kizazi chake kitatokana na "Mubarakah" (mwanamke aliyebarikiwa), na mwanamke huyo ni mwenza wa mama yako huko peponi."  

Katika zama za ujahilia na kabla ya Muhammad kupewa utume, mwanamke alinyimwa haki zake zote na kuishi katika hali ya kusikitisha sana. Katika baadhi ya makabila mtoto wa kike alitambuliwa kuwa ni aibu na fedheha, na alikuwa akizikwa akiwa hai. Katika kipindi hicho Bibi Khadija na kwa kutumia mafundisho ya Uislamu, alithibitisha kuwa, mwanamke ana haki ya kuishi, kupata haki zake zote kama mwanadamu na hata kukwea ngazi za juu kabisa za ukamilifu, kiasi cha Mtume Muhammad (saw) kumtambua kuwa ni mmoja kati ya wanawake wanne bora kuliko wote duniani. Nafasi hii adhimu ya Bibi Khadija (as) ilithibitishwa zaidi na salamu alizokuwa akitumiwa na Mwenyezi Mungu SW kupitia ujumbe uliokuwa ukiletwa na Malaika Jubril kwa Mtume Muhammad (saw). Vilevile Abu Said al Khudri amepokea kwamba: Mtume Muhammad (saw) amesema: Usiku nilipokuwa katika safari ya M'iraji, wakati wa kurejea Jibril alinikaribia. Nilimwambia: Ewe Jibril! Unayo haja? Alijibu kwa kusema: Haja yangu ni kwamba mfikishie Khadija salamu za Mwenyezi Mungu na salamu zangu. Wakati Mtume alipowasilisha ujumbe huo wa Malaika Jibril kwa Khadija, Bibi huyo mwema alisema" Mwenyezi Mungu ni amani, na amani inatoka kwake, na amani iwe juu ya Jibril.

Bibi Khadija pia ni mmoja kati ya wanawake wanne boza zaidi wa Peponi ambao Mtume Muhammad (saw) anasema katika Hadithi iliyopokewa na Ibn Abbas na Ikrimah kuwa ni Khadija binti Khuwailid, Fatima binti Muhammad, Maryam binti Imran na Asia binti Muzahim. Bibi Khadija alikuwa na hadhi na utukufu mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kiasi kwamba, wakati anajifungua Fatimatu Zahra, zama alipokuwa ametengwa na wanawake wenzake wa Kiquraish, Mwenyezi Mungu SW hakumuacha peke yake, bali aliwatuma wanawake bora wa Peponi kama Asia na Bibi Maryam mama yake Nabii Issa kwenda kumsaidia katika mashaka ya kujifungua.

Mtume Muhammad (saw) aliishi na mke wake mwema, Bibi Khadija kipindi cha miaka 25. Watukufu hao wawili waliishi miaka mitatu katika mzingiro wa Maquraish katika pango maarufu la Shiibi Abi Twalib mjini Makka. Kipindi hiki cha mzingiro wa Mtume na Ahlibaiti zake pamoja na idadi kadhaa ya Waislamu kimesajili kumbukumbu nyingi kuhusiana na Bibi Khadija. Katika kipindi chote cha miaka mitatu ya mzingiro huo uliosababisha mashaka makubwa ya kiuchumi kwa Waislamu, Bibi Khadija alitoa mali yake kwa ajili ya kuhudumia Waislamu wote waliokuwa wamezingirwa katika eneo hilo. Wakati huo Waislamu waliuziwa bidhaa kwa bei kubwa mara kadhaa zaidi ya bei yake ya kawaida na kwa kificho hadi mali yote ya Bibi Khadija ikamalizika. Kipindi hicho Waislamu wakiongozwa na Mtume (saw) ambaye alikuwa pamoja na Bibi Khadija, ami na mlinzi wake mkubwa, Abu Twalib, Ali bin Abi Twalib na kadhalika walilazimika kula nyasi na mizizi ya miti kutokana na mashaka makubwa waliyokabiliana nayo.  

Miaka mitatu kabla ya Mtume kuhamia Makka na muda mfupi baada ya mtukufu huyo kuondoka katika mzingiro wa Maquraish katika Shiibi Abi Twalib, Bibi Khadija alipatwa na maradhi. Wakati huo Mtume Muhammad (saw) alizungumza na Bibi Khadija na kumwambia: "Ewe Khadija! Hivi unajua kuwa, Mwenyezi Mungu amekufanya mke wangu pia huko Peponi?" Kisha Mtume alimjulia hali na kumpa bishara njema ya kuingia katika daraja za juu Peponi kutokana na huduma zake kubwa kwa Uislamu.

Maradhi ya Bibi Khadija yalishadidi zaidi na kwa sababu hiyo alimwambia Mtume wasia wake na kusema: Yaa Rasulallah! Ninataka kuusia mambo kadhaa. Kama sikutimiza wajibu wangu kwako naomba unisamehe. Mtume (saw) alisema: Katu hujanikosea na daima ulifanya bidii na juhudi kubwa katika kazi na majukumu yako. Umehangaika sana nyumbani kwangu na umesabilia mali yako katika njia ya Mwenyezi Mungu. Khadija alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezii Mungu! Wasia wangu wa pili ni kwamba muangalie vyema binti yangu Fatima. Kwa sababu baada yangu mimi atakuwa yatima na mpweke; tafadhali mlinde wanawake wa Kiquraish wasije wakamuudhi. Asije mtu akamzaba kibao au kumkaripia. Mchunge asije mtu akaamiliana naye kwa njia isiyofaa. 

Jengo lililokuwa na kaburi la Bibi Khadija huko Makka kabla ya kubomolewa na Mawahabi wa Saudi Arabia.

Nukuu za historia zinasema kuwa, wakati Bibi Khadija alipokuwa kwenye dakika za mwisho za uhai wake alimwita Asmaa bint Umais na kumuusia binti yake, Fatimatu Zahra. Baada ya hapo alimtuma Fatima kwa baba yake na kumwambia amuombe moja ya nguo na mavazi yake ili iwe kafani yake baada ya kufariki dunia. Wakati Fatima alipokwenda kwa baba yake na kumwambia ombi la Bibi Khadija, Mtume (saw) alilia na kububujikwa na machozi na muda mfupi baadaye aliteremka Malaika Jibril akiwa na nguo ya kafani kutoka mbinguni ambayo ilitumwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Khadija.

Mtume Muhammad (saw) alimpenda sana Bibi Khadija kuliko wake zake wote na daima alikuwa akimtaja kwa wema na kumuombea dua na maghufira. Hatimaye bibi huyo mtukufu alifariki dunia katika siku ya tarehe 10 mwezi wa Ramadhani mwaka wa 10 baada ya Mtume kubaathiwa akiwa na umri wa miaka 65 kama wanavyosema baadhi ya wanahistoria. Mtume (saw) aliosha mwili wa Bibi Khadija na kumkafini katika nguo aliyoletewa na Malaika Jibril kutoka mbinguni. Mtume (saw) aliingia yeye mwenyewe kwenye kaburi la Bibi Khadija (as) na kumzika huku akilia na kububujikwa na machozi. Alikuwa akiomba dua na kumtakia maghufira kwa Mwenyezi Mungu. Tunaweza kusema kuwa, tukio chungu zaidi katika maisha ya Mtume Muhammad (saw) lilikuwa hili la kuondokewa na mke wake kipenzi, mwema na mwaminifu yaani Bibi Khadija (as). Kwa kadiri kwamba, mwaka huo aliofariki dunia ndani yake Bibi Khadija na ami yake, Abu Twalib ambao ndio waliokuwa nguzo mbili muhimu za kueneza risala na ujumbe wa Mwenyezi Mungu katika zama za awali, umepewa jina la "Mwaka wa Huzuni". Tangu wakati huo kila mara jina la Khadija lilipotajwa, Mtume alikuwa akilia na kutokwa na machozi na kumuombea dua. Sala na salamu za Allah zimshukie Bibi mwema, kipenzi, mwaminifu na mbora wa wanawake wa Peponi, Khadija Binti Khuwailid. 

Tags