May 20, 2021 08:17 UTC
  • Mashambulizi ya Israel dhidi ya waandishi na vyombo vya habari Ukanda wa Gaza

Zaidi ya Wapalestina 230 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kikatili ya Israel yaliyoanza yapata siku kumi zilizopita. Zaidi ya 63 kati ya waliouliwa shahidi ni watoto na karibu 40 ni wanawake.

Israel haitosheki na kushambulia na kuua raia wasio na hatia wa Palestina. Jumamosi iliyopita jeshi la utawala huo lilishambulia jengo la al-Jalaa ambalo lilikuwa na ofisi za mashirika kadhaa ya habari ya kimataifa kama televisheni ya al Jazeera ya Qatar na shirika la habari la Marekani la Associated Press. Jengo hilo pia lilikuwa na ofisi za wanasheria na makazi ya raia. Shambulizi hilo dhidi ya ofisi za mashirika ya habari ya kimataifa kwa hakika ni shambulizi dhidi ya vyombo vyote vya habari vinavyofanya kazi kubwa ya kufichua jinai na uhalifu unaoendelea kufanyika huko Gaza na Palestina kwa ujumla. Jinai na uhalifu huo ni doa jingine la fedheha kwa utawala huo haramu na bandia unaoendelea kuua watoto wadogo na wanawake. 

Wafanyakazi wa mashirika ya habari ambayo yanawapasha walimwengu habari za matukio halisi yanayojiri huko Palestina, sasa wao wenyewe wanalengwa na kuuliwa na makatili wa Israel. Jengo lililokuwa na ghorofa 13 la al Jalaa lilipigwa kwa mambora kadhaa na kungushwa chini tena mbele ya macho ya kamera na vyombo vya habari vya kimataifa. Israel imedai kuwa, jengo hilo lilikuwa na zana za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS). Hata hivyo madai hayo yamepingwa vikali na mmiliki wa jengo hilo. Jawad Mahdi anasema: Kinyume na madai ya Israel, hakukuwepo zana za kijeshi katika jengo la al Jalaa na lilikuwa makazi ya mashirika ya habari na makampuni ya kibiashara. Vilevile nyumba 60 katika jengo hilo zilikuwa makazi ya raia wa kawaida. Jawad Mahdi anaongeza kusema kuwa, kabla ya shambulizi hilo afisa mmoja wa shirika la ujasusi la Israel alimtahadharisha na kutaka walioko kwenye jengo hilo waondoke. Anasema nilimuomba afisa huyo wa Israel anipe dakika 10 ili waandishi habari waondoe zana navifaa vyao vya kazi lakini ombi hilo likakataliwa.

Siku kadhaa zilizopita aghlabu ya vyombo vya habari vilionyesha picha ya mazungumzo hayo ya Jawad Mahdi na afisa wa ujasusi wa Israel na baadaye kidogo kuporomoka kwa jego la al Jalaa kwa kushambuliwa na makombora ya utawala haramu wa Israel. Japokuwa tukio hilo halikusababisha kifo cha mtu yeyote lakini ni kielelezo cha kifo cha uhuru wa kusema na kujieleza, na kushambuliwa uhuru huo katika zama ambapo nchi za Magharibi zinajigamba na kutoa nara za kulinda uhuru wa kusema na vyombo vya habari. Siku ya Jumamosi iliyopita kwa hakika ilikuwa siku nyeusi kwa ulimwengu wa vyombo vya habari na mawasiliano ya umma. Siku mbayo ilisadifiana na kutimia mwaka wa 73 tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoasisiwa katika ardhi ya Palestina. Siku hiyo kwa Wapalestina inajulikana kama Siku ya Nakba yaani siku ya janga na maafa. 

 

Shirika la habari la Associated Press limetangaza kuwa, limeshushwa mno na shambulizi hilo. Shirika hilo limesema: "Israel ilikuwa na habari kwamba, jengo hilo linatumiwa na mashirika na waandishi wa habari; sasa dunia inapata habari chache zaidi kuhusu yanayojiri Ukanda wa Gaza kuliko ilivyokuwa hapo kabla." 

Mkurugenzi Mtendaji wa Associated Press, Gary Pruitt ametoa taarifa akisema: "Tumeshtushwa na kutishwa" na shambulio la anga la Israeli dhidi ya ofisi za AP na mashirika mengine ya habari na kuharibiwa jengo hilo. Israel ilikuwa ikijua mahali zilipo ofisi zetu na kwamba waandishi habari wanafanya kazi katika jengo hilo.   

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar pia imetoa taarifa ikilaani shambulio la jeshi la Israel dhidi jengo la al Jalaa na ofisi yake katika Ukanda wa Gaza. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Al Jazeera, Mostefa Souag amesema: "Tunaitaka jamii ya kimataifa ilaani vikali hatua hiyo ya kinyama na kushambuliwa waandishi wa habari. Kuharibu ofisi za vyombo vya habari ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na kunahesabiwa kuwa ni jinai kivita."

 Taarifa ya al Jazeera imesema: Shambulizi la Israel dhidi ya jengo la al Jalaa ni kitendo cha kutaka kuwazuia waandishi wa habari kutekeleza jukumu lao takatifu la kuhabarisha ulimwengu na kuripoti matukio yanayojiri Ukanda wa Gaza."    

Jarida la Kimarekani la Variety pia limeandika kuwa, shambulizi la Israel dhidi ya ofisi za mashirika ya habari ya kigeni katika Ukanda wa Gaza ni shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari. Kamati ya Kulinda Waandishi Habari (CPJ) yenye makao yake mjini New York pia imesema kuwa: Hujuma dhidi ya jengo la vyombo mashuhuri vya habari vya kimataifa inaonesha kuwa Wizara ya Ulinzi ya Utawala unaoikalia kwa mabavu Quds inalenga vyombo vya habari ili kuzuia upashaji habari unaoanika na kuweka wazi mashaka ya watu wa Gaza. 
Mkurugenzi wa CPJ, Joel Simon amesema shamblizi hili limekiuka sheria za kimataifa na kuongeza kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel unalazimika kutoa sababu madhubuti na makini ya kuhalalisha shambulizi dhidi ya taasisi ya kiraia."  

Jeshi la Israel lielenga jengo la mashirika ya habari kama al Jazeera na Associated Press

Jumuiya ya PEN America pia imeitaka Israel itoe maelezo kamili na ya kutosha kuhusu hujuma hiyo na kusema: Uharibu uliosababishwa na shambulizi hilo unawazuia waandishi habari weledi kusajili matukio ya mapigano yanayotia wasiwasi na tata katika kipindi hiki nyeti.          

Mbali na vyombo vya habari na taasisi husika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres pia amesema kuwa shambulizi dhidi ya ofisi za vyombo vya habari vya kimataifa na makazi ya raia huko Gaza limekiuka sheria za kimataifa na mashambulizi kama hayo yanapaswa kuzuiwa kwa thamani yoyot ile. 

Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu nchini Uingereza (Islamic Human Rights Commission (IHRC)) Massoud Shajareh amesema kuhusiana na shambulizi ya Israel dhidi ya makao ya mashirika ya habari ya kimataifa mjini Gaza kuwa, Wazayuni hawastahamili kusikliza haki na kweli. Wazayuni wanatumia nguvu zote ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga ili kuziba mdomo wa mtu yeyote anayejaribu kufichua ukweli na kuzua upashaji habari.
Mjumbe wa ngazi za juu wa jumuiya kubwa zaidi inayopinga vita ya Uingereza amesema hujuma iliyofanywa na Israel dhidi ya jengo la mashirika ya habari katika Ukanda wa Gaza ni kielelezo cha hujuma dhidi ya uhuru wa kusema, na jithada za kuzuia upashaji habari zinazohusiana na jinai zinazofanyika katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.  

Stephane Bell amesema: Katika vita vya sasa serikali ya Israel imeazimia kuzuia upashaji wa habari, suala ambalo linakwenda kinyume na msingi wa upashaji huru wa habari. Wapalestina na watu huru duniani hawatasalimu amri kwa hatua hiyo ya waungaji mkono wa Israel na ubebe. Bell amesema kuwa, upashaji habari unaendelea katika mitandao ya kijamii na kuongeza kuwa: "Sauti ya wapigania uhuru wa Palestina itaendelea kusikika kupitia maandamano yanayofanyika katika kona zote za dunia." Ameongeza kuwa: Inawezekana kuvunja na kuharibu majengo, lakini haki na hakika itabakia hai siku zote."

Ofisi za mshirika ya habari ya kimataifa zimeshambuliwa na kubomolewa na Israel, Gaza

Nukta muhimu ya kuashiria ni kwamba, moja kati ya changamoto kubwa katika migogoro yote ya utawala ghasibu wa Israel na wamiliki halisi wa Palestina ni tufani ya upashaji habari wa vyombo na waandishi wa habari ambayo huwaathiri sana mamilioni ya watu kote duniani na hata ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel yenyewe. Mbinu ambayo imekuwa ikitumiwa na Israel kukabiliana na tufani hiyo hadi sasa ni kuchuja habari zote za vyombo vya habari kabla ya kurushwa hewani au kuchapishwa kwa kisingizio cha kulinda siri za utawala huo ghasibu. Wazayuni walielewa mapema umuhimu wa vyombo vya habari na taathira yake katika fikra za walimwengu; hivyo tangu miaka mingi huko nyuma waliamua kudhibiti vyombo vya habari na mawasiliano ya umma ili kuweza kupata nguvu kubwa ya taathira kuliko hata nguvu ya dola. 

Mbinu ya utawala wa kizayuni ya kuzuia upashaji habari haiishii katika kubana uhuru wa kusema na kukandamiza waandishi na vyombo vya habari, bali tunaweza kuashiria pia nukta kwamba, wanahabari wengi na waandishi wa Israel ni wanajeshi na maafisa wa dhiba wa jeshi au wanajeshi waliostaafu. Waandishi hawa huakisi tu habari zinazooana na maslahi ya utawala haramu wa Israel. 

Tangu kulipoanzishwa harakati ya kupinga Uzayuni, Wazayuni walianza kufuatilia malengo kadhaa kupitia propaganda na kuanzisha mitandao mikubwa ya kufanya propaganda kote duniani. Malengo hayo huwa yamejadiliwa na kupasishwa katika protokali za vinara wa Uzayuni na huwa yanajikita zaidi katika kuzihadaa fikra za walimwengu na kuangamiza jamii za kifikra za wasio wa Wayahudi. 

Kwa sasa Israel imejikuta ikimulikwa na aghlabu ya vyombo vya habari duniani ambavyo vinafichua na kuweka wazi jinai na uhalifu unaofanyika huko Palestina hususan Ukanda wa Gaza na kutuma picha na filamu zinazofichua ukatili na mauaji ya watu wasio na hatia hususan wanawake na watoro wadogo. Hatua ya walimwengu ya kulaani hujuma ya Israel dhidi ya jumba la mashirika ya habari huko Gaza na kujikita zaidi vyombo vya habari katika kazi ya kuakisi ukweli na matukio ya kweli, itaendelea kuwatia kiwewe na wahka Wazayuni maghasibu na kuwaandamana wakati wote.     

Tags