Jul 19, 2021 13:35 UTC

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametoa ujumbe kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa siku hizi za Hija akisema kuwa kuendelea majonzi ya nyoyo za Waislamu wenye hamu kubwa ya kushiriki katika ugeni wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu ni mtihani wa muda na wa kupita.

Amesisitiza udharura wa kutopuuzwa ujumbe wa ibada ya Hija na kusema kuwa, mapambano dhidi ya madola ya kibeberu hususan Marekani ni miongoni mwa jumbe hizo.

Sambamba na kuashiria matatizo na mashaka ya Ulimwengu wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei ametaja fahari za wanamapambano na mwamko wa sasa hususan huko Palestina, Yemen na Iraq kuwa ni hakika inayotia matumaini katika eneo la Magharibi mwa Asia na kusema kuwa: Ahadi ya kweli ya Mwenyezi Mungu ni kwamba atawapa nusra wapiganaji wa Jihadi, na athari ya kwanza ya Jihadi hiyo ni kuizuia Marekani na madola mengine ya kibeberu kuingilia na kufanya vitendo vya shari katika nchi za Waislamu.

Matini kamili ya ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni hii ifuatayo:

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei

 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehrama, Mwenye kurehemu

Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu, na sala na salamu zake zimshukie Muhammad, Aali zake watoharifu, Masahaba zake wema na wafuasi wao hadi Siku ya Mwisho.

Mwaka huu pia Umma wa Kiislamu umekosa kupata neema adhimu ya ibada ya Hija, na nyoyo zenye shauku kubwa (ya kuhudhuria katika ibada hiyo) zimeshindwa kushiriki katika ugeni kwenye nyumba ya heshima kubwa ambayo Mwenyezi Mungu Mwenye hikima na Mrehemevu ameitengeneza kwa ajili ya watu.

Huu ni mwaka wa pili ambapo msimu wa raha na furaha ya kiroho wa Hija umebadilika na kuwa msimu wa kutengana na masikitiko, na balaa la maradhi ya kuambukiza, na pengine pia balaa la siasa zinazotawala Haram ya Makka zinazuia macho yenye shauku kubwa ya waumini kushuhudia nembo ya umoja na adhama na masuala ya kiroho ya Umma wa Kiislamu na kufunika kilele hicho cha juu cha adhama na fahari kwa kiwingu na vumbi.

Huu ni mtihani, sawa na mitihani mingine ya kupita ya historia ya Uma wa Kiislamu ambayo inaweza kuwa sababu ya kesho bora na yenye kung'aa; na jambo muhimu ni kwamba, Hija kwa sura yake halisi, ibakie hai katika nyoyo za kila Mwislamu, na ujumbe wake aali usinyauke, hususan hivi sasa ambapo amali zake zimesitishwa kwa muda.

Hija ni ibada yenye siri nyingi. Muundo na mpangilio wa kuvutia wa harakati na visimamo vyake, hujenga utambulisho wa Mwislamu na jamii ya Kiislamu na ni dhihihirisho la umaridadi wake katika macho ya walimwengu. Katika upande mmoja inazipandisha juu kabisa nyoyo za waja kwa dhikri, khushui na unyenyekevu na kuzikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, na katika upande mwingine, ibada hiyo huwafungamanisha ndugu waliotoka maeneo yote ya dunia kwa mavazi na harakati zao za aina moja na zenye uwiano. Katika upande mwingine pia Hija huwaonesha walimwengu nembo kubwa zaidi ya Umma wa Kiislamu kwa amali zake zilizojaa maana na siri nyingi na kuwadhihirishia wasiowatakia mema Waislamu azma na adhama kubwa ya Umma.

Vita vya Upanga wa Quds vilivyowapa ushindi wanamapambano wa Palestina

Mwaka huu haiwezekani kuhiji kwenye Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, lakini inawezekana kuelekeza nyoyo zetu kwa Mwenye Nyumba hiyo, kumdukuru, kunyenyekea mbele yake, kutaradhia kwake na kufanya istighfar na kuomba msamaha wake. Hatuwezi kuhudhuria kisimamo cha Arafa, lakini tunaweza kuomba dua na kunong'ona na Mola katika Siku ya Arafa. Haiwezekani kumpiga mawe Shetani huko Mina, lakini inawezekana kuwafukuzia mbali mashetani wanaopenda madaraka na jaha mahala pote. Haiwezekani kuhudhuria kwa pamoja kandokando ya al Kaaba, lakini ni wajibu wa siku zote wa nyoyo zetu kutufu na kuzunguka Aya za wazi za Qur'ani tukufu na kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu.

Sisi, wafuasi wa dini ya Uislamu, ambao hii leo tuna jamii kubwa, ardhi pana, utajiri wa maliasili na mataifa hai na yaliyomacho, tunapaswa kutumia rasilimali zetu kujenga na kutengeneza mustakbali. Katika kipindi cha miaka 150 ya hivi karibuni mataifa ya Waislamu hayakuwa na nafasi na mchango wowote katika mustakbali wa nchi na serikali zao wao wenyewe, na ukitoa mifano michache tu, yametawaliwa na madola vamizi ya Kimagharibi na kusumbuliwa na jicho la tamaa, uingiliaji na shari zao. Kubakia nyuma kielimu na utegemezi wa kisiasa wa sasa wa nchi nyingi ni matokeo ya utendaji usiofaa. Mataifa yetu, vijana wetu, wasomi wetu wanazuoni wa dini wanafikra wetu wanasiasa, vyama na jumuiya zetu sasa vinapaswa kufidia kipindi kilichopita cha kuaibisha; wanapaswa kusimama kidete na kupambana dhidi ya utumiaji mabavu, uingiliaji na uovu wa madola ya Magharibi.

Neno la Jamhuri ya Kiislamu Kiislamu ambalo limeutia wasiwasi na hasira ulimwengu wa ubeberu ni wito mapambano hayo. Ni wito wa kupambana dhidi ya uingiliaji kati na uovu wa Marekani na madola mengine vamizi na kushika hatamu za mustakbali wa Dunia ya Kiislamu kwa kutegemea maarifa ya Kiislamu.

Hapana shaka kuwa Marekani na washirika wake wanakerwa sana na anwani ya "mapambano na muqawama" na wamezidisha uhasama dhidi ya "kambi ya mapambano ya Kiislamu". Ushirikiano wa baadhi ya nchi za eneo la Asia Magharibi pia ni ukweli mchungu unaosaidia kuendelezwa uovu huo.   

Wanamapambano wa Ansarullah nchini Yemen

Njia nyoofu ambayo sisi huainishiwa na amali za Hija zikiwemo sai', tawaf, kusimama Arafat, kutupa mawe Jamarat, shaari za Hija na mkusanyiko mkubwa wa umoja (wa Waislamu) huimarisha imani zetu kuhusiana na kumtegemea Mwenyezi Mungu, kutegemea nguvu zake zisizo na mwisho, kutegemea uwezo wa taifa, kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kufikia malengo na kutupa matumaini makubwa ya kufikia ushindi.

Ukweli wa mambo katika uwanja na eneo la Kiislamu unaimarisha zaidi matumaini na azma hiyo. Kwa upande mmoja, matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu, kubakia nyuma kielimu, utegemezi wa kisiasa na changamoto za kiuchumi na kijamii, zinatuwajibisha kufanya jitihada kubwa zaidi ili kutatua matatizo na changamoto hizo. Palestina inayodhulumiwa inahitajia msaada wetu, Yemen inayodhulumiwa na kutapakaa damu inaumiza nyoyo, matatizo ya Afghanistan yanawatia wote wasiwasi, matukio machungu katika nchi za Iraq, Lebanon, Syria na nchi nyingine za Waislamu, ambayo yamesababishwa na mikono ya shari ya Marekani na washirika wake yanapasa kukabiliwa na ghera (uchungu/heshima) na juhudi zisizochoka za vijana. Wakati huo huo kudhihiri mrengo wa mapambano ya Kiislamu katika kipindi hiki nyeti, mwamko wa mataifa ya Kiislamu na mvuto wa vijana wenye uchungamfu na msisimko kwa upande wa pili, ni jambo linalozidisha matumaini kwenye nyoyo. Palestina nzima imechukua 'upanga wa Quds'; Qus, Gaza, Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, ardhi zilizoporwa na kukaliwa kwa mabavu (na Wazayuni) mwaka 1948 na kambi zote za wakimbizi zimeamka na kumtia adabu mvamizi katika kipindi cha siku kumi na mbili. Yemen ambayo imedhulimiwa na kuachwa peke yake, imevumilia na kusimama imara kwa miaka saba mbele ya vita, jinai na mauaji ya kidhulma ya adui asiye na huruma na katili. Licha ya kuwepo uhaba wa chakula, dawa na bidhaa nyingine nyingi za msingi maishani, lakini haijasilimu amri mbele ya maadui dhalimu wanaotumia mabavu bali maadui hao wamewashangaza na ujasiri, uwezo na ubunifu wao (Wayemen) katika medani ya vita.

Nchini Iraq wanamapambano wamewafikishia ujumbe ulio wazi Marekani vamizi na vibaraka wao wa Daesh na kuweza kuwarejesha nyuma (katika medani ya vita). Kwa njia hiyo wamewafikishia ujumbe ulio wazi kuhusiana na azma yao thabiti ya kukabiliana na kila aina ya uingiliaji na shari kutoka kwa Marekani na washirika wake.

Wanamapambano wa Hashd al Shaabi nchini Iraq

Juhudi za kipropaganda za Wamarekani kwa ajili ya kupotosha ukweli wa mambo, azma, matakwa na matendo ya vijana shupavu na wanamapambano huko Iraq, Syria na nchi nyingine za Kiislamu, na kuwanasibisha na Iran au nchi nyingine yoyote ni kuwavunjia heshima vijana hao shujaa na wenye mwamko, na bila shaka  suala hilo linatokana na Wamarekani kutofahamu wala kuyadiriki vyema mataifa ya eneo hili.

Ni ufahamu huo usio sahihi ndo ulioifanya Marekani idhalilishwe nchini Afghanistan. Iliivamia nchi hiyo kwa mbwembwe na makelele mengi miaka ishirini iliyopita ambapo iliwaua kinyama raia wa kawaida na wasio na hatia wa nchi hiyo kwa silaha na mabomu. Pamoja na hayo lakini nchi hiyo ilijipata imekwama kwenye kinamasi na hatimaye kulazimika kuondoa askari na zana zake za kijeshi katika nchi hiyo. Ni wazi kwamba, taifa lenye mwamko la Afghanistan linapasa kuwa macho kuhusiana na vyombo vya ujasusi na silaha za vita laini za Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. Taifa hilo lipasa kusimama imara mbele ya vyombo na silaha hizo.

Mataifa ya eneo hili yamethibitisha kwamba yako macho na kuwa yamejitenga na baadhi ya tawala vibaraka ambazo zinasalimu amri mbele ya matakwa ya Marekani hata kuhusiana na suala nyeti mno la Palestina; tawala ambazo zinashirikiana na kuunyoshea mkono wa urafiki utawala ghasibu wa Israel kwa siri na kidhahiri. Kwa maneno mengine ni kwamba, wanapinga uwepo wa haki ya taifa la Palestina ndani ya ardhi yake ya kihistoria. Huu ni unyakuzi na uporaji wa rasilimali za Wapalestina. Hawajatosheka na uporaji wa maliasili za nchi zao na sasa wanataka kupora rasilimali za taifa la Palestina.

Ndugu Waislamu! Eneo letu na matukio yake tofauti yanayokwenda kwa kasi kubwa ni maonyesho ya masomo na ibra mbalimbali. Kwa upande mmoja tunashuhudia nguvu kubwa inayotokana na jitihada na mapambano mkabala wa mabavu na uchokozi, na kwa upande wa pili udhalili unaotokana na kusalimu amri na kuwa dhaifu mbele ya adui na mwishowe kukubali utwishaji wake. Ahadi ya kweli na isiyo na shaka ya Mwenyezi Mungu ni kuwanusuru mujahidina wanaopigana katika njia yake: : اِن تَنصُرُوا اللَّهَ یَنصُرکُم وَ یُثَبِّت اَقدامَکُمMkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu. Taathira ya kwanza ya jihadi na jitihada hizo ni kuinyima Marekani na nchi nyingine zinazotumia mabavu kimataifa, fursa ya uingiliaji na kufanya shari katika mataifa ya Kiislamu, Inshallah.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuyanusuru mataifa ya Waislamu, salamu zimwendee Imam wetu wa Zama Imam Mahdi (AF) na tunamwomba Mwenyezi Mungu ampandishie daraja Imam Khomeini (MA) pamoja na mashahidi watukufu.

Na salamu ziwaendee waja wema wa Mwenyezi Mungu.

Sayyid Ali Khamenei 26 Tir 1400

6 Dhil Hijja 1442.

Tags