Sep 12, 2021 02:21 UTC
  • Mchango wa Ruqayyah (a.s) Katika Kufikisha Ujumbe wa Ashura Kwa Walimwengu

Assalaam alaykum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale yanapokufikieni matangazo haya. Karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu nilichokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyoaga dunia Ruqayyah, binti mdogo wa Imam Hussein (as). Huku nikitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na hasa wafuasi wa watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume (saw), nina wingi wa matumaini kwamba, mtakuwa pamoja nami ili mnufaike na yale niliyokuandalieni kwa mnasaba huu. Karibuni

 

Moja ya matukio muhimu na yaliyobakia katika historia na ambayo yamekuwa na taathira kubwa kwa jamii ya Kiislamu, hususan Mashia ni tukio la Karbala, mauaji na masaibu yaliyompata Imam Hussein AS, wafuasi wake na watu wa familia yake. Katika historia kumetokea matukio mengi makubwa na yenye engo pana kuliko tukio la Ashura, lakini hakuna hata tukio moja kati ya hayo ambalo limekuwa na mchango muhimu katika uga wa maisha ya kiutamaduni na kijamii ya jamii na athari zake kubakia hata baada ya kupita karne nyingi kama ilivcyo kwa tukio la Ashura na harakati ya Imam Hussein (as) huko Karbala. Bila shaka shakhsia iliyojaa nuru ya Imam Hussein na wafuasi wake pamoja na ushujaa wao mkubwa ni mambo yaliyokuwa na nafasi muhimu katika tukio hilo. Masahaba wa Imam Hussein na watu wa familia yake hasa waliochukuliwa mateka walikuwa na nafasi ya aina yake katika kuendeleza harakati ya Imam Hussein na kuonyesha dhulma kubwa iliyofanywa dhidi ya mjukuu huyo wa Mtume. Mmoja wa watu hao ni binti mdogo wa Imam Hussein aliyejulikana kwa jina la Ruqayyah  (a.s).

 

Wanahistoria wengi wanasema kuwa tarehe 5 Safar mwaka 61 Hijria ndiyo inayosadifiana na siku Ruqayyah alipoaga dunia. Ruqayyah aliyekuwa binti mdogo wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as), alikamatwa mateka pamoja na Bani Hashim na wajukuu wengine wa Mtume Muhammad (saw) baada ya mauaji ya kutisha ya baba yake, Imam Hussein (as) katika jangwa la Karbala. Wanahistoria wanasimulia kwamba, alasiri ya tarehe 10 Muharram, Omar Bin Sa'ad aliyekuwa kamanda wa jeshi la Yazid bin Muawiya aliamuru kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Imam Hussein kipelekwe katika mji wa Kufa kwa gavana wa Yazid, yaani Ubaydullah bin Ziyad. Khawli bin Yazid na Hamid bin Muslim ndio waliopewa jukumu la kupeleka kichwa hicho kitukufu cha mjukuu wa Mtume (saw). Khawli ambaye alikuwa amebeba habari kubwa, alitangulia mbele na kwenda mbio hadi kwenye kasri ya Ibn Ziyad mjini Kufa, lakini alifika kwa kuchelewa na akakuta milango ya kasri imekwishafungwa. Alilazimika kuchukua kichwa cha Imam Hussein nyumbani kwake na kukificha kwenye tanuri. Alimwambia mke wake kwamba: Nimekuja na kitu ambacho kitatupa utajiri wa milele. Nimeleta nyumbani kichwa cha Hussein bin Ali. Mke wa Khawli alisema kwa mshangao mkubwa kwamba: Ole wako! Watu wanapeleka dhahabu na fedha majumbani mwao, wewe unaleta nyumbani kichwa cha mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu?!! Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba, kamwe sitalala tena na wewe katika nyumba moja.

Baada ya kusema hayo, mke wa Khawli alitoka nje na ghafla aliona nuru kubwa iliyokuwa ikiangaza kuelekea mbinguni. Asubuhi mapema Khawli alichukua kichwa hicho kitukufu na kukipeleka kwa Ubaydullah bin Ziyad. Wanahistoria wanasema kichwa cha Imam Hussein (as) kilikuwa kikisoma baadhi ya Aya za Qur'ani katika maeneo na minasaba tofauti hadi kilipofikishwa kwa mtawala mal'uni na dhalimu Yazid bin Muawiya. Sheikh Mufid katika kitabu cha al Irshad, Sayyid Hashim al Bahrani katika kitabu cha Madinatul Maajiz na Allamah Majlisi katika Biharul-Anwar wanasema kuwa, miongoni mwa Aya zilizosomwa na kichwa kitukufu cha Imam ni ile ya 13 ya Suratul Kahaf inayosema: Sisi tunakusimulia habari zao kwa haki. Hakika hao ni vijana waliomwamini Mola wao na tukawazidishia uongofu. Vilevile kilisoma sehemu ya Aya ya 227 ya Suratu Shuaraa inayosema:

«وَ سَیَعْلَمُ الَّذِینَ ظَلَمُوا أَیَّ مُنْقَلَبٍ یَنْقَلِبُونَ‏»  "Na wale waliodhulumu watajua mgeuko watakaogeukia." 

Imepokewa pia kutoka kwa Salama bin Kahiil akisema: Nilikiona kichwa cha Imam Hussein kikiwa juu ya mkuki kikisoma sehemu ya Aya ya 137 ya Suratul Baqara inayosema: «فَسَیَکْفِیکَهُمُ اللَّهُ وَ هُوَ السَّمِیعُ الْعَلِیم‏» "Basi Mwenyezi Mungu anakutosha shari yao, na Yeye ndiye Msikizi na Mjuzi."

 

Kichwa cha Imam Hussein na mashahidi wengine wa Karbala vilitundikwa kwenye mishale na kupelekwa Damascus kwa Yazid bin Muawiya vikitangulia msafara wa wajukuu wa Mtume (saw) waliotekwa baada ya mauaji ya tarehe 10 Muharram. Katika msafara huo alikuwamo Ruqayyah binti wa Imam Hussein aliyekuwa na umri wa miaka 4 kama wanavyosema baadhi ya wanahistoria. Baada ya kufikishwa makao makuu ya utawala wa Bani Umayyah, Yazid mal'uni aliamuru mateka hao wa Bani Hashim washikiliwe kwenye gofu moja lililokuwa kando kidogo ya kasri yake. Usiku, binti huyo malaika wa Imam Hussein alimuona baba yake kwenye ndoto na akaamka kwa fadhaa na kuanza kulia. Ruqayyah alikuwa akipiga mayowe na kumwita baba yake. Walijaribu sana kumtuliza mtoto huyo bila ya mafanikio na kadiri walivyomtuliza ndivyo kilio na masikitiko yake yalivyozidi. Kilio na maumivu ya mtoto Ruqayyah viliwaliza watu wote waliokuwa pamoja naye mahala hapo.

Baada ya kupata habari hiyo Yazid aliwaamuru askari wake waingie kwenye gofu hilo wakiwa na sinia lililokuwa limefunikwa. Baadhi ya mateka hao walidhani kwamba, sinia hiyo ilikuwa na chakula kwa ajili ya mtoto huyo aliyekuwa akilia sana kwa huzuni. Hata hivyo hali ilikuwa tofauti kabisa. Sinia hiyo ilisogezwa mbele ya mtoto Ruqayyah kisha kifuniko chake kikaondolewa. Sinia ilikuwa na kichwa cha mjukuu wa Mtume Hussein bin Ali (as). Mtoto huyo alipoona kichwa cha baba yake kilichokuwa kimejaa damu alitahayari mno na kuangua kilio kikubwa. Alikikumbatia kichwa cha baba yake na kukibusu kisha akasema: Baba yangu! Nani amekupaka damu? Ewe baba yangu! Nani amekata shingo yako… Nami amenifanya yatima…. Ruqayyah aliendelea kulia na kuzungumza na kichwa cha baba yake hadi sauti yake ikakatika. Watu waliokuwa kandokando yake walidhani amepatwa na usingizi na walipomsogelea walikuta amekata roho na kufariki dunia. Inna lillah wainna ilayhi rajiuun….   

 

Katika tukio la kusikitisha la tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria, watu wa rika zote, wanaume na wanawake, mabwana na watwana, weupe na weusi, vijana na wazee watoto na hata vichanga vilivyokuwa vikinyonya vilitengeneza historia. Kana kwamba Mwenyezi Mungu alitaka kutimiza hoja yake kwa walimwengu na kuthibitisha haki ya Hussein na masahaba zake.

Watoto walioongozana na wazazi wao katika msafara wa nuru wa Karbala waliwaona kwa macho yao baba zao wakiuawa shahidi na kukatwakatwa kwa mapanga ya adui. Watoto hao walijifunza jinsi ya kusimama imara na kupambana na dhulma na madhalimu wakiwa bado wadogo na kufuata nyayo za wazazi na ndugu zao. Japokuwa hawakupigana vita lakini kuwepo katika medani ya vita peke yake na kufa shahidi kwa wengine kama Sayyidat Ruqayyah kulitajirisha harakati ya mapambano ya Karbala na kuharakisha zaidi kuporomoka na kuangamia utawala dhalimu wa Bani Umayyah.    

Mwandishi wa Kitabu cha Sahabe Rahmat (yaani Wingu la Rehma) Abbas Ismaili amenukuu baadhi ya karama za Sayyidat Ruqayyah katika kitabu hicho. Anasema: Sayyid Ibrahim Dimishqi ambaye alikuwa miongoni mwa walinzi wa Haram ya Ruqayyah (as) alitimiza umri wa miaka 90 bila ya kupata mtoto wa kiume. Sayyid Dimishqi alikuwa na watoto watatu wa kike. Usiku mmoja binti mkubwa wa Sayyid Ibrahim alimuona Sayyidat Ruqayyah kwenye ndoto akimwambia kwamba: "Mwambie baba yako aende kwa liwali na amwambie, baina ya mwili na lahadi ya kaburi langu kuna maji yanayoniudhi na kunikera. Mwambie aje akarabati kaburi na lahadi yangu." Binti wa Sayyid Ibrahim alimsimulia baba yake ndoto hiyo lakini baba hakutilia maanani.

Usiku wa pili binti wa pili wa Sayyid Ibrahim aliona ndoto hiyo hiyo na kumsimulia baba yake ambaye pia hakutilia maanani. Usiku wa tatu binti wa tatu wa Sayyid Ibrahim alisimulia ndoto hiyo hiyo lakini baba hakuchukua hatua. Usiku wa nne Sayyid Ibrahim Dimishqi mwenyewe alimuona Hadhrat Ruqayyah kwenye ndoto akimwambia: "Kwa nini hujamfikishia liwali ujumbe wangu?" Sayyid aliamka kwa hamaki na kwenda kwa liwali na kumpa ujumbe huo.

Liwali aliwakusanya maulama wa Kishia na Kisuni wa eneo la Sham na akawaamuru waoge na kuvaa nguo safi na nadhifu. Kisha akamwamuru kila mmoja wao afungue kufuli ya mlango wa haramu ya Ruqayyah na kusema, mtu ambaye mlango utamfungukia ndiye atakayechimba kaburi la mjukuu huyo wa Mtume na kuondoa maiti yake kaburini. Maulama wote walijaribu kufungua lakini kufuli haikufunguka. Baada ya hapo Sayyid Ibrahim ndiye aliyeweza kufungua kufuli ya Haram ya Sayyidat Ruqayyah. Aliingia ndani na kufukua kaburi na lahadi yake akakuta mwili wa mjukuu huyo wa Mtume ukiwa bado mzima kana kwamba amezikwa leo. Maji mengi yalikuwa yamekusanyika katika lahadi na mwanandani wa kaburi hilo. Sayyid Ibrahim alichukua mwili huo kutoka kwenye lahadi na kuulaza kwenye magoti yake kwa muda wa siku tatu. Alikuwa akilia katika siku zote hizo hadi kaburi lilipokarabatiwa. Wakati wa haja au Swala, Sayyid Ibrahim alikuwa akiuweka mwili wa Sayyidat Ruqayyah juu ya kitu safi na nadhifu na kuuchukua na kuulaza tena kwenye magoti baada ya kukamilisha ibada. Alipotaka kuuzika tena mwili wa Ruqayyah, Sayyid Ibrahim alitawasali na kuomba dua kwa Mwenyezi Mungu ampe mtoto wa kiume. Dua yake ilikubaliwa na Mwenyezi Mungu akamruzuku mtoto wa kiume akiwa uzeeni. Mtoto huyo alipewa jina la Sayyid Mustafa. Tukio hilo lilijiri mwaka 1280 Hijria.

Haram ya Ruqayyah bint Hussein mjini Damascus Syria

 

Yazid bin Muawiya alizima sauti ya mtoto mdogo wa Imam Hussein (as) ili asiendelee kufichua maovu yake lakini kaburi dogo la mjukuu huyo wa Mtume (saw) limebakia daima kuwa waraka na ushahidi wa ukatili na dhulma za Yazidi na Mayazidi mithili yake. Roho ya binti mdogo Ruqayyah ilipaa na kuelekea juu mbinguni kama lilivyo jina lake, lakini dhulma alizofanyiwa yeye na mashahidi wengine wa haki zitabakia kuwa kielelezo cha ukatili wa madhalimu miaka na dahari.

Kwa sasa kaburi na haram ya mtoto huyo wa Imam Hussein (as) imekuwa eneo la ziara kwa maashiki na wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw). Kaburi dogo na mjukuu huyo wa Mtume linamliza na kumsikitisha kila mtu anayetembelea eneo hilo katika mji wa Damascus huko Syria. Kila Mwislamu anayekwenda kufanya ziara mahala hapo hujiuliza, kwa nini mtoto huyu mdogo alichukuliwa mateka na kufungwa katika gofu? Kwa nini aliaga dunia siku 25 tu baada ya mauaji ya baba yake? 

Kwa hakika kifo cha Ruqayyah ni nyaraka ya wazi ya dhulma ya madhalimu ambao waliokuwa wakidai kuwa ni viongozi wa Waislamu baada ya Mtume (saw).

Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu na wafuasi wa Ahlul-Baiti (as) kwa mnasaba wa kukumbuka kifo cha Ruqayyah binti Hussein (as). 

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh.

 

 

 

Tags