Oct 23, 2021 12:31 UTC
  • Kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad SAW

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa mbora wa viumbe Mtukufu Mtume Muhammad SAW.

Tunatoa mkono wa kheri baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwengu kwa mnasaba wa Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume SAW. Ni matumaini yanguu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kuutegea sikio nilichokuandalieni kwa leo.

 

Tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia, ulimwengu uliangaziwa nuru ya kuzaliwa Mtume Muhammad SAW, ambaye baada ya miaka arobaini alikuja kubaathiwa na kupewa Utume ili aje kukamilisha tabia njema na kuwaongoza wanadamu ili wafikie katika saada na ufanisi wakweli. Mtume SAW alibaathiwa na kupewa Utume katika kipindi ambacho ulimwengu ulikuwa umetawaliwa na dhulma, ukandamizaji na giza totoro la ujahili. Mtume SAW alikuwa na nara alioitoa kwa walimwengu wote ya

قولوا لااله الا الله تُفلِحوا

"Semeni, hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu, ili mpate kufaulu."

Katika kivuli cha maneno haya yaliyojaa nuru, Mtume SAW akawapa walimwengu adia kutoka kwa Allah, nayo ni dini bora na kamilifu zaidi ya Uislamu. Kwa baraka za risala ya Mtume Muhammad SAW moto wa vita na mauaji ya wana-ndugu ukazimika na kupitia kivuli cha mafundisho ya Uislamu, watu wote wakawa kitu kimoja na wakawa ni wenye kuhurumiana. Kutokana na kujipamba kwake kwa tabia njema, Mtume SAW amesifiwa na kupigiwa mfano katika Qur'ani Tukufu. Upole na ulaini wa Mtume ulimsaidia mbora huyo wa viumbe katika kufikia malengo yake ya muda mrefu. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani Tukufu aya ya 159 ya Surat al-Imran:

"Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungelikuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangelikukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. "

 

Umoja wa Umma wa Kiislamu ni miongoni mwa misingi muhimu iliyokuwa ikitiliwa mkazo na Bwana Mtume SAW mkabala na adui wa pamoja, na sira na mwenendo wa Mtume SAW unaonesha kwamba, mbora huyo wa viumbe alifanya hima na idili kubwa. Hii leo makusudio ya umoja wa umma wa Kiislamu ni haya kwamba, Waislamu kila mmoja akiwa na madhehebu yake wajumuike pamoja katika mambo ya kidini yanayowakutanisha pamoja kama Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Qur,ani, Mtume SAW, sunna na sira ya Mtume SAW mkabala na hatari zinazoikabili misingi na nguzo za Uislamu na jamii ya Waislamu. Kwa muktadha huo Waislamu wanapaswa kushikamana, kuunganisha nyoyo zao na kujiweka mbali na tofauti za Kimadhehebu, kisiasa, kikaumu na kilugha.

 

Moja ya mambo ambayo tunaweza kuyaashiria kama ni mbinu na mkakati muhimu wa Mtume wa Allah kwa ajili ya kuleta umoja ni namna alivyokuwa akiamiliana na watu sambamba na kujipamba kwake na tabia njema. Tabia njema, upole na ulaini wa Mtume uliwavutia wengi na kuwa sababu muhimu ya kuzima hitilafu na mifarakano. Tabia yake njema wakati mwingine iliwafanya hata maadui wake wakubwa kuungana na wafuasi wake.

Kutokana na Mtume SAW kufahamu na kudiriki vyema mazingira ya kijamii yaliyokuwa yakitawala katika zama hizo, aliandaa mazingira ya kuleta umoja baina ya watu. Kuingia Madina Bwana Mtume SAW kulikwenda sambamba na kutiliana saini mikataba na makundi mbalimbali. Mikataba hiyo inaweza kuwa mikakati ya wazi kabisa kwa ajili ya umoja wa Kiislamu katika jamii ya wakati huo.  Baada ya kuingia Yathrib, yaani Madina, Mtume Mtukufu alitayarisha mazingira ya kujenga umoja na mshikamano katika jamii mpya ya Kiislamu. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na mtukufu huyo ni kutayarisha mkataba wa kwanza kabisa katika Uislamu katika miezi ya mwanzoni mwa kuwepo kwake Yathrib (Madina). Mtume wa Mwenyezi Mungu aliandika mkataba kati ya Muhajirina na Ansar kwa upande mmoja na Mayahudi wa Madina kwa upande mwingine.

 

Katika mkataba huo Mtume aliahidi kwamba dini na mali za Mayahudi zitaheshimiwa kwa masharti maalumu. Mkataba huo ulionesha jinsi Mtume Muhammad SAW alivyoheshimu misingi ya uhuru, nidhamu na uadilifu katika maisha ya kijamii. Vilevile mkataba huo uliunda kambi moja ya watu wa Madina dhidi ya uvamizi na mashambulizi yoyote kutoka nje. Mkataba huo uliandaa uwanja wa kuweko umoja wa kisiasa na kiutawala. Aidha hatua yake ya kuunga udugu baina ya Muhajirina (Waislamu waliohama kutoka Makka) na Ansar (wenyeji wa Madina) wa kusaidiana katika njia ya haki, nayo ilikuwa na umuhimu wa aina yake. Kwa hatua hiyo Mtume (saw) alijenga umoja na mshikamano wa pande zote kati ya Muhajirina na Ansar.

Wapenzi wasikilizaji, jamii iliyoundwa na Bwana Mtume SAW katika zama hizo, ilikuwa jamii ya kidugu na ambayo ilikuwa na umoja, ushirikiano na mshikamano. Mtume SAW anasema: Mfano wa Waumini katika kupendana na kurehemeana na kuhurumiana kwao ni sawa na viungo vya mwili mmoja, kiungo kimoja kikishtakia maumivu, basi mwili mzima huwa pamoja na kiungo hicho katika maumivu.

Katika sehemu nyingine ya sira ya Bwana Mtume SAW na mkakati wake wa kuhakikisha umoja unapatikana baina ya Waislamu, mbora huyo wa viumbe alitoa hotuba muhimu katika Masjidul Haraam baada ya Fat'h Makka. Mtume SAW alisema katika sehemu ya hotuba hiyo kwamba:

Mwislamu ni ndugu wa Muislamu, hamdhulumu, haachi kumsaidia, wala hamdanganyi na wala hamdharau.

 

 

Mkakati mwingine uliotumiwa na Bwana Mtume SAW ili kuhakikisha umoja wa umma wa Kiislamu unapatikana ni kupinga ukaumu, ukabila na ubaguzi. Uislamu ulipambana vikali na taasubi za kikaumu pamoja na ubaguzi, na ukaweka bayana kwamba, kigezo cha ubora wa mtu sio rangi, kabila, taifa au utajiri bali ni taqwa na uchaji Mungu. Ili kuwa kigezo na ruwaza njema, Bwana Mtume SAW alisimama na kupambana vikali na taasubi.

Siku moja sahaba wa Mtume SAW, Salman Fars aliyekuwa Muajemi alikuwa amekaa katika msikiti wa Mtume SAW. Hapo walikuweko pia masahaba wakubwa na mara katika mazungumzo yao likajitokeza suala la nasaba na asili ya mtu. Basi kila mtu akawa akitaja nasaba na asili yake na kwa namna fulani akijifakharisha kwa hilo. Ilipofika zamu ya sahaba Salman Farsi mabwana wale wakamwambia, jieleze na utaje nasaba na asili yako. Hata hivyo, badala ya kujifakharisha, Salman Farsi akasema, jina langu mimi ni Salman na ni mtoto wa mmoja wa waja wa Mwenyezi Mungu. Nilikuwa katika upotofu, Mwenyezi Mungu akaniongoa kupitia Mtume Wake Muhammad SAW, nilikuwa masikini, Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake akanifanya nisiwe mhitaji, nilikuwa mtumwa, Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume Wake akanikomboa.

 

Hii ndio nasaba na asili yangu." Haukupita muda Mtume SAW akaingia msikitini hapo na Salman Farsi akamhadithia Mtume yale yaliyojiri hapo. Mtume SAW akawageukia wale masahaba ambao wote walikuwa ni kutoka kabila la Quraishi na kusema: Enyi Maquraishi! Damu ni nini? Ukaumu ni nini? Nasaba na fakhari ya kila mtu ni dini yake. Ubinaadamu na uungwana wa mtu ni tabia yake, shakhsia yake ni kufanya kwake kazi kwa wingi.

Sisitizo la Bwana Mtume SAW la kutokuwa na msingi wowote suala la taasubi za kikaumu na kikabila ni jambo ambalo lilikuwa na taathira chanya na kubwa katika kuleta hali ya mshikamano na kukurubisha pamoja nyoyo za Waislamu hususan Waislamu wasiokuwa Waarabu na hivyo kuleta mfungamano na mshikamano baina yao.

Wapenzi wasikilizaji kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwengu kwa mnasaba wa maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa mbora wa viumbe, Muhammad bin Abdillah, Mtume wa Allah (s.a.w.w).

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags