Nov 13, 2021 16:19 UTC

Assalaamu Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hassan Askari (as), ambaye ni miongoni mwa Maimamu watoharifu katika kizazi cha Bwana Mtume Muhammad (saw). Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa kando ya redio zenu kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Alfajiri ya tarehe 8 Mfunguo Saba Rabiuthani mwaka 232 Hijria habari ya kuzaliwa mwana mbarikiwa ilienea katika mji mtakatifu wa Madina. Siku hiyo Imam Hassan Askari mwana wa Imam Ali al Hadi alikuwa amezaliwa na kunawirisha nyumba ya Ahlul Bait (as). Siku za kuzaliwa Maimamu watoharifu katika nyumba ya Mtume Muhammad (saw) huwa siku za furaha kwa waumini wote na huwa na darsa na ibra nyingi za kujifunza. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maisha yote ya watukufu hao tangu kuzaliwa kwao hadi walipoaga dunia na kuuawa shahidi yamejaa nukta nyingi za kujifunza.

Imam Hassan Askari alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 22. Kipindi cha Uimamu wake kiliendelea kwa muda wa miaka 6 na wakati wote huo alikabiliana na vikwazo, vizingiti na mashaka mengi kutoka kwa watawala wa Bani Abbas.

Akiwa bado mchanga, Imam Askari (as) aliishi na baba yake uhamishoni katika eneo la Samarra lililoko kilomita 110 kaskazani mwa Baghdad huko Iraq. Familia ya Imam iliwekwa chini ya usimamizi na uangalizi mkali wa watawala wa Kiabbasi. Imenukuliwa kuwa ilikuwa vigumu mno kwa wafuasi wa Ahlul Bait kuwasiliana na Imam Askari katika kipindi hicho kutokana na mzingiro mkubwa wa watalawa wa Kiabbasi. Kutokana na hali hiyo Imam alilazimika kuwasiliana na wafuasi wake kupitia masahaba zake kadhaa waliokuwa karibu naye.

 

Pamoja na hali hiyo Imam Hassan Askari (as) hakuacha mapambano yake dhidi ya madhalimu na watawala mafisadi na daima alifanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba, mafundisho yenye thamani ya dini tukufu ya Kiislamu yanawafikia watu walau kwa mashaka makubwa. Alianzisha mbinu maalumu za kueneza mafundisho halisi ya Uislamu kupitia njia ya kujibu maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiulizwa na wapinzani wa dini, kuweka wazi misimamo ya Uislamu kupitia njia ya kushiriki kwenye midahalo na mijada ya kielimu na kulea kizazi cha wanafunzi hodari na wenye maarifa sahihi ya Uislamu.

Imam pia alitoa kipaumbele sana kwa suala la kutoa huduma na kuwasaidia waumini na watu wenye haja.

Imam Hassan Askari anasema: Mambo mawili ni miongoni mwa sifa mbili kuu. Imani na itikadi ya Mwenyezi Mungu Mmoja na kuwanufaisha ndugu katika imani. Kwa mujibu wa hadithi hii ya Imam Askari, kuwahudumia watu kuna umuhimu mkubwa kiasi kwamba kumetajwa baada ya suala la imani ya itikadi ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Kama unavyojua mpenzi msikilizaji katika aya nyingi za Qur'ani Tukufu Mwenyezi Mungu SW ametaja "amali njema" baada ya imani na kumwamini Yeye. Kwa msimgi huo katika hadithi hii Imam Askari (as) anakutaja kuwahudumia watu kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya amali njema.   

Moja ya mambo yenye umuhimu mkubwa katika akhlaki na maadili ya Kiislamu ni kuwajali watu, kuwa na moyo wa ushirikiano, kutenda wema na kuwahudumia watu kwa njia mbalimbali hususan waumini na watu watenda mema. Tunapotazama Aya za Qur'ani Tukufu na hadithi nyingi na vilevile sira na mwenendo wa Mitume wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake tunaona kuwa, hakuna jambo linalomkurubisha zaidi mja kwa Mola Muumba baada ya kutenda amali za wajibu kama kutenda wema na kuwahudumia waja wake. Ni kwa sababu hiyohoyo ndiyo maana Manabii na mawalii wa Mwenyezi Mungu daima walikuwa wakitanguliza mbele kazi ya kuwahudumia watu na kukidhi haja zao.

 

Imam Askari (as) pia aliwaarifisha wafuasi halisi wa Ahlul Bait kuwa ni wale ambao sawa na viongozi wao wa kidini, wanashiriki barabara katika harakati ya kuwahudumia watu na ndugu zao katika dini na kuheshimu mipaka na sheria za Mwenyezi Mungu. Anawaarifisha Shia na wafuasi wa kweli wa Watu wa Nyumba tukufu ta Mtume (saw) kwa kusema: "Shia na wafuasi halisi wa Ali bin Abi Twalib (as) ni wale wanaowatanguliza ngudu zao wa kidini mbele ya nafsi zao japokuwa wao wenyewe ni wahitaji."

Anasema katika hadithi nyingine akiwabainishia wajibu wa wanazuoni na maulamaa wa kidini kwamba: Maulamaa wanaotufuata sisi Ahlul Bait ambao wanafanya jitihada za kutatua matatizo ya wafuasi wetu wataingia katika uwanja wa kufufuliwa Siku ya Kiyama wakiwa na taji la ukarimu vichwani mwao huku nuru ya taji hilo ikiwaka kila upande na kuwamulikia watu watakaokuwepo kwenye uwanja huo.

Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Abu Hashim anasimulia kwamba: Siku moja Imam Hassan Askari alisema katika hadhara ya watu kuwa: Moja ya milango ya kuingia peponi unaitwa mlango wa "maaruf" kwa maana ya mlango wa mema. Na hakuna mtu atakeingia peponi kupitia mlango huo isipokuwa wale waliotenda mema duniani na kuwasaidia wanadamu wenzao.

Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) walikuwa vigezo bora vya kuigwa baada ya babu yao na walijipamba kwa sifa aali za kibinadamu. Kwa msingi huo Imam Hassan Askari mwenyewe alikuwa kigezo cha kuigwa katika kuwasaidia na kuwahudumia watu katika jamii.

Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Muhammad bin Ali amesema: hali ya kimaisha ilituwia ngumu mimi na familia yangu kutokana na umaskini na kila tulikokwenda kuomba msaada na auni tuliambulia patupu. Baba alisema: Hebu twende kwa Imam Hassan Askari kwani watu wanasema kuwa ni mtu karimu na amekuwa mashuhuri kwa sifa hiyo. Muhammad bin Ali anaendelea kusimulia kuwa: Tulikwenda nyumbani kwa Imam na tulipokua njiani baba alisema itakua vizuri sana kwangu kama Imam atanipa dirihamu 500 ili niweze kukidhi haja zangu. Dirhami 200 nitazitumia kununua nguo zangu na ahli yangu, dirhamu nyingine 200 nitazitumia kwa ajili ya kulipa madeni na mia moja zitakazosalia nitazitumia kwa ajili ya masurufu mengine.

 

Muhammad bin Ali anaendelea kusema kuwa: Mimi pia nilitamani lau Imam angenipa dirhamu mia tatu nikakidhi mahitaji yangu. Anasema tulipofika nyumbani kwa Imam hadimu wake alitoka nje na kuita: Ali bin Ibrahim na mwanaye waingie ndani. Tuliingia ndani na kumsalimia Imam Askari ambaye alimwambia baba kwamba: kwa nini hadi sasa hujaja kututembelea?

Baba alisema: Sayidi wangu, nilikuwa nikiona haya kuja nyumbani kwao katika hali mbaya kama hii niliyonayo. Anasema: Tulipotoka nje hadimu wa Imam alimpa baba kifuko kilichokuwa na fedha na kusema: Hizi hapa dirhamu 500. Tumia dirhamu 200 kwa ajili ya kununua mavazi, dirhamu nyingine 200 lipia madeni yako na mia moja itakayosalia itumie katika mahitaji yako mengine. Hadimu wa Imam pia alitoa kifuko kingine na kunipa mimi kisha akasema: hizi ni dirhamu 300. Tumia dirhamu 100 kwa ajili ya kununulia kipandwa, mia moja kwa ajili ya kununua mavazi na mia itakayosalia itumie kwa ajili ya mahitaji yako mengine. 

Wapenzi waskilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu cha leo unaelekea ukingoni. Ni matumaini yangu kuwa mumefaidika na kipindi hiki kilichowajieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Imam Hassan Askari (as), mmoja kati ya wajukuu watoharifu wa Mtume wetu Muhammad (saw). Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri na baraka kwa Waislamu wote hususan wafuasi wa Ahlul Bait (as) kwa mnasaba huo na tunamuomba M, Mungu SW atujaalia kuwa miongoni mwa wafuasi wa kweli wa Mtume na Ahlubaiti zake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.