Dec 06, 2021 12:41 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Kujitolea na Ustawi wa Kiuchumi na Kijamii

Kusaidia na kutoa huduma kwa wanadamu wenzako ni miongoni mwa sifa na vigezo vyenye thamani kubwa vya maisha ya binadamu.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa kawaida mwanadamu hawezi kukidhi matakwa na mahitaji yake yote peke yake katika jamii, na hapana shaka kwamba ni ushirikiano, muawana na kujitolea ndivyo vinavyokuwa na taathira kubwa zaidi katika uwanja huo. Ushirikiano na muawana huo unaweza kufanyika kwa kujitolea na kutenda wema. Watu wa jamii husika wanaweza kuwa na taathira kubwa sana katika kupunguza matatizo mengi ya jamii hiyo kwa kushiriki katika kazi za kujitolea na kutoa huduma bila ya malipo kwa wanadamu wenzao wenye haja. 

Kazi ya kujitolea ni ile inayofanyika kwa uhuru na irada kamili ya kutaka kutenda kheri na hisani, na huakisi hamu ya mtu husika ya kuonesha mshikamano wake na wanadamu wengine. Mtu anayejitolea ni yule anayependa na kutaka kushiriki au kutoa huduma bila ya kulazimishwa, kuamrishwa na bila ya kutarajia malipo ya kifedha na kidunia. Katika upande mwingine watu wanaofaidika na huduma hizi za kujitolea hujihisi kuwa hawako peke yao na kwamba wanathaminiwa na kujaliwa na jamii katika mazingira yote. 

Katika dunia ya sasa kuna haja kubwa ya kubuniwa mbinu na njia mpya za kutatua matatizo mbalimbali ya kijamii na kukidhi mahitaji ya wanadamu wenzetu. Miongoni mwa mbinu hizo ni kazi za kujitolea. Kwani sambamba na kuwasaidia watu wenye haja, watu wanaojitolea pia hutoa huduma na kuifadisha jamii nzima kwa ujumla. Uchunguzi umebaini kuwa, jamii yenye utajiri wa watu wenye kujitolea na kujisabilia huwa na idadi ndogo sana ya wahalifu, watu waliokimbia au kuacha masomo, mapigano ya kikabila na kikaumu na kadhalika na husifika kwa ustawi wa kiuchumi. 

Ni kutokana na umuhimu huo mkubwa wa kazi za kujitolea katika jamii ndiyo maana tarehe 5 Disemba kila mwaka ikatangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kujitolea. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 17 Disemba mwaka 1985 lilipasisha suala hilo na tangu wakati huo siku hii huadhimishwa kote duniani kuwaenzi na kuwahamasisha wanadamu wote wanaojisabilia na kujitolea kutoa huduma kwa wanadamu wenzao. Kwa mwaka huu wa 2021 maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kujitolea (IVD) yamefanyikak kwa kauilimbiu inayohimiza watu "Kujitolea sasa kwa ajili ya maisha yetu ya baadaye". Kuhimiza, kutambua na kutangaza na kampeni ya kujitolea ni sehemu muhimu ya kuunda mustakabali ulio sawa na jumuishi kwa jamii na ulimwenguni kote.

Kazi za kujitolea za Umoja wa Mataifa hufanywa na watu ambao hujiandikisha kufanya kazi kama hizo kipindi cha mwaka mzima. Jumuiya ya Wajitoleao ya Umoja wa Mataifa (United Nations Volunteers) au UNV kwa kifupi huwasaidia wanadamu kuwa na maisha bora zaidi na halisi na miongoni mwa kazi zinazofanywa na wanachama wa jumuiya hii ni pamoja na miradi ya kutoa elimu bora bora huduma afya. 

Kazi za kujitolea zina taathira kubwa sana katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa nchi mbalimbali. Kwa miaka mingi sasa ambapo kazi za aina hii zinafanyika katika maeneo tofauti ya dunia na kutoa msaada mkubwa kwa nchi na serikali. Uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Marekani katika nchi 37 unaonesha kuwa, watu karibu milioni 140 wanafanya kazi za kujitolea kwa ajili ya ustawi wa jamii wa nchi zao, na kiwango hicho kinakaribia asilimia 12 ya watu wazima katika nchi hizo. Uchunguzi huo unasema kuwa, watu wanaofanya kazi za kujitolea husaidia kiasi cha karibu dola bilioni 400 kwa uchumi wa dunia. Hii inaonesha jinsi watu, mashirika na jumuiya mbalimbali zinavyotoa mchango mkubwa katika harakati na shughuli za kijamii na maendeleo ya kiuchumi. 

 Hii leo kunahisika haja kubwa zaidi ya wajitoleao katika nchi zinazostawi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, taasisi na jumuiya za kiserikali katika nchi hizo haziwezi kutekeleza isipokuwa kiwango cha chini kabisa cha miradi na huduma zao, na utekeleza bora wa kazi na huduma hizo unawezekana kwa msaada wa asasi na watu anaojisabilia na kujitolea. Pamoja na hayo inatupasa kusema kuwa, ili kazi hizi za kujitolea ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kuna ulazima wa kuwepo mipango na ratiba nzuri, uwekezaji wa kutosha, mafunzo sahihi na kadhalika. Vilevile watu wanaohudumiwa wanapaswa kuelewa vyema umuhimu wa kazi hizi za kujitolea.

Ustawi endelevu ni miongoni mwa malengo muhimu ya nchi zote duniani, na ili kuweza kupata ustawi huo nchi hizo zinahitajia zaidi watu na jumuiya zinazofanya kazi za kujitolea. Watu na asasi za aina hii zina umuhimu mkubwa sana katika kufanikisha, kuratibu, kupanga na kusimamia kazi za kujitolea. Kazi za watu na jumuiya hizi huwa msaada muhimu sana kwa sekta ya uchumi na masuala ya kijamii na hata ya kisiasa ya nchi au jamii husika. Si hayo tu, bali tunathubutu kusema kuwa, umuhimu na mchango wa watu na asasi hizi unaweza kufananishwa na umuhimu wa kazi za serikali. Hivyo inatupasa kusema kuwa, kazi hizi za kujitolea si mbadala wa kazi na shughuli za serikiali bali ni kamilisho muhimu la kazi hizo. Jumuiya na taasisi zinazofanya kazi za kujitolea hutoa huduma muhimu sana katika jamii kama ujenzi wa mahospitali na vituo vya afya, shule, vituo vya kulea mayatima na wasiojiweza, taasisi za kidini na kiutamaduni, maeneo ya michezo na burudani na kadhalika ambavyo huwa na taathira kubwa sana katika kuboresha maisha ya raia. Vilevile watu na taasisi hizo zinazofanya kazi za kujitolea huwa washirika na wasaidizi bora katika utekelezaji wa miradi ya serikali kama kupambana na umaskini, kuwezesha watu wa jamii, kutoa elimu, kukabiliana na uhalifu na matatizo ya kijamii, kupunguza ufa wa kimatabaka na kadhalika.       

 Tunakamilisha makala yetu leo kwa kutupia jicho baadhi ya taasisi za kijamii zinazofanya kazi za kujitolea nchini Iran. Hapa nchi kuna asasi na jumuiya nyingi zisizo za serikali zinazojishughulisha na kazi za kutoa huduma mbalimbali za kujitolea na kazi za kheri. Miongoni mwa taasisi hizo ni ile ya Mahak iliyoanza kazi zake mwaka 1991 kwa ajili ya kuhudumia watoto wenye maradhi ya saratani wenye umri wa chini ya miaka 16 na familia zao. Ikitumia misaada ya wahisani na wananchi na wafanyakazi wake kujitolea, taasisi hii ya Mahaka imepata mafanikio makubwa katika kutoa misaada ya kibinadamu, kutoa matibabu na kufanya utafiti. Hii leo taasisi hii inatambulika kuwa miongoni mwa vituo vikubwa vya tiba ya saratani ya watoto katika kanda ya Mashariki ya Kati. Hadi mwishoni mwa mwaka 2016 taasisi hii ya Mahaka ilikuwa imehudumia zaidi ya watoto elfu 27 wenye maradhi ya saratani na kutoa misaada kwa familia zao katika kipindi chote cha matibabu.

Taasisi ya Mahak 

Taasisi nyingine muhimu katika uwanja huu hapa nchini ni jumuiya ya misaada ya kibinadamu ya Imam Ali’s Popular Students Relief Society. Jumuiya hii isiyo ya serikali ilianza kazi mwaka 2008 kwa shabaha ya kutoa misaada kwa watoto na wanawake waliopatwa na shida na masaibu. Mwaka 2010 Jumuiya hii ilifanikiwa kupewa hadhi ya kuwa mshauri katika Baraza la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (United Nations Economic and Social Council). Lengo la jumuiya hii ya Imam Ali (as) ni kujenga dunia yenye uadilifu na amani kupitia njia ya kuwahudumia watu waliopatwa na masaibu hususan wanawake na watoto. Karibu watu elfu 40 wanapata huduma za aina mbalimbali katika vituo vya jumuiya hiyo katika maeneo mbalimbali ya Iran kama huduma za tiba ya masuala ya kinafsi, vikao vya ushauri nasaha kwa watu binafsi na makundi, kutoa elimu na mafunzo kwa watoto, kutoa elimu na stadi za ujasiriamali na kujiajiri kwa wanawake wanaosimamia familia zao, huduma za matibabu kwa familia na kadhalika.