Dec 06, 2021 16:48 UTC
  • Siku ya Kufutwa Utumwa Duniani

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, aliyemuumba mwanadamu akiwa huru, hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa wa mwingine na hakuumba kiumbe chochote isipokuwa kwa ajili ya kumwabudu Yeye mwenyewe, ambaye ni Muumba na anayestahiki kuabudiwa.

Katika historia, daima kumekuwapo watu ambao waliasi amri za Mungu na kupuwauza wanadamu wengine kutokana na kupenda makuu, kiburi na kujiona bora zaidi ya wanadamu wengine. Katika ulimwengu wetu wa sasa, licha ya maendeleo yote yaliyopatikana katika ujuzi na utambuzi, bado kuna watu na tawala zinazosumbuliwa  na tabia hii ya kujiuona bora na juu ya wengine kutokana na kiburi na ziko tayari kufanya vituko na lolote kwa ajili ya kuendeleza hali hiyo. 

Moja kati ya vituko hivyo ni kile kinachoambatana na jina la Christopher Columbus kwa jina la ugunduzi wa Amerika!! Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, je, kweli inawezekana kugundua ardhi yenye mamilioni ya wanadamu wamaoishi katika ardhi hiyo?! Bila shaka hapana, na hii ndiyo hiyo tabia na hulka tunayoitaja kuwa ni ya kiburi, kujiona bora zaidi na juu ya wengine na kupenda makuu.     

Christopher Columbus

Wakati Christopher Columbus alipotia mguu katika ardhi ya Amerika ya leo, wenyeji walimkaribisha yeye na wenzake kwa ukarimu na wema, lakini jibu la wema huo halikuwa kingine ghairi ya miaka mingi ya vita, uhalifu, mauaji, na uporaji. Katika kipindi kifupi, wanajeshi wa Uingereza waliwaua kwa umati wenyeji asilia wa Amerika. Baada ya kuangamizwa kizazi cha wenyeji, ardhi kubwa na takriban isiyo na watu wa eneo hilo ilitwaliwa na wavamizi. Hata hivyo ardhi hii ingeweza kuwa na faida kwa wavamizi hao kama utajiri na rasilimali zake vingewanufaisha wanyonyaji; na jambo hili halingeweza kutimia bila ya kuwa na nguvu kazi rahisi na pengine ya bure.

Wavamizi wa Uingereza walichagua mfumo wa utumwa ili kupata nguvu kazi hii ya bure na walitumia jeshi lao la majini kupanua kwa kasi mfumo huo, kiasi kwamba katika kipindi cha karne mbili wafanyabiashara wa Uingereza walibadilika na kuwa wafanyabiashara wakubwa zaidi wa watumwa duniani. Serikali ya Uingereza ilianzisha kampuni barani Afrika ambayo iliwawinda rasmi wanadamu huru na kuwasafirisha kama watumwa katika makoloni ya nchi hiyo katika bara la Amerika. Kwa utaratibu huo, katika kipindi cha kati ya mwaka 1500 na 1800, watu huru wapatao milioni 15 walisafirishwa na kupelekwa Amerika wakiwa watumwa.

Meli makhsusi za kubeba watumwa zilikuwa jinamizi la pili la watu huru wa jana na watumwa wa leo. Katika meli hizi, watumwa walilala chini kwenye sakafu ya mbao katika eneo la chini ya chombo hicho wakiwa wamefungwa minyororo kwa pamoja. Msongamano mkubwa wa watu, uvundo na ukosefu wa maji, chakula na hata hewa ya kutosha ya kupumua vilikuwa miongoni mwa sababu za watumwa wengi kufa katika safari hiyo ambayo wakati mwingine iliendelea kwa wiki sita.

Watumwa hao walikuwa wakiuzwa sokoni mara tu baada ya kuwasili Amerika, na huo uilikuwa mwanzo wa jinamizi lao la tatu. Walikabiliana uso kwa uso na wamiliki ambao, kwa kisingizio kidogo tu, walitenda ukatili na unyama kupita kiasi, na ilikuwa kawaida sana kwa kosa dogo la mtumwa au kutoridhika kwa bwana, kugharimu maisha  ya wanadamu hao. Kila mtu alimwona bwana kama mmiliki wa maisha ya watumwa wao; na mmiliki kumuua mtumwa halikuwa kosa lililostahiki adhabu. Pale mtumwa alipokuwa akitoroka na kukamatwa, mikono yake ilikuwa ikikatwa, kisha sehemu iliyosalia ya mikono iliyojeruhiwa ilikuwa ikitumbukizwa kwenye lami iliyochemshwa kwa moto na baadaye kunyongwa. Mbinu hii ya adhabu, ambayo ilikuwa ni aina ya mateso makali, iliitwa "lynching", na ilitumiwa kwa kipindi cha miaka mia nne ya historia ya utumwa nchini Marekani kuwasulubu maelfu ya wanadamu wasio na hatia. 

Hatimaye, baada ya karne nyingi za uhalifu na unyonyaji dhidi ya watu weusi, mwaka wa 1862, Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, alipitisha Sheria ya Kukomesha Utumwa. Swali linalopaswa kuulizwa hapa ni kwamba, je, tunaweza kumtambua Lincoln kuwa mwokozi wa watumwa? Je, Lincoln alifanya hivyo kurejesha haki za watu weusi?   

Abraham Lincoln

Abraham Lincoln, kama walivyokuwa Wamarekani wote weupe, hakuwa na shaka yoyote katika itikadi ya ubaguzi wa rangi. Alikuwa akisema waziwazi kwamba: "Sijawahi kuwa, na kamwe sitakuwa mtetezi wa usawa wa kijamii, kisiasa, na wa kimbari baina ya wazungu na weusi... Nasema kuna tofauti kubwa za kimaumbile baina ya mbari za wazungu na watu weusi ambazo daima zinazuia kuishi pamoja kwa msingi wa usawa wa kijamii na kisiasa; hivyo hapana budi moja kati ya mbari hizo itakuwa na nafasi ya juu na bora zaidi. Mimi pia kama walivyo wengine wote ninaunga mkono fikra ya kuwa juu na bora zaidi watu weupe."

Kwa kutilia maanani fikra kama hizi za kibaguzi ni jambo lililombali kwamba Abraham Lincoln alifanya jitihada za kuwakomboa watumwa kwa nia na malengo ya "kibinadamu". Aliandika katika barua yake mopja kwamba: "Nitalinda muungano ... Kama ningeweza kuulinda muungano bila kumwachia huru mtumwa yeyote, ningefanya hivyo, ... Kila kitu ninachofanya kuhusu utumwa na watu wenye rangi nyeusi ni kwa sababu nadhani kinaweza kusaidia kulinda muungano."

Katika hotuba yake nyingine, Linkoln anataja sababu ya mapambano yake dhidi ya utumwa kuwa ni matatizo yaliyosababishwa na mfumo huo kwa Marekani. Swali linalokuja hapa ni kwamba je, mfumo wa utumwa ulikuwa na hatari gani kwa Marekani? Kwa nini mfumo huo haukuwa na manufaa tena kwa Marekani? Ili kupata jibu la maswali haya, ni vyema kupitia historia ya Marekani katika miaka iliyotangulia kupitishwa kwa sheria hii.

Baada ya vita na Ufaransa, Uingereza haikuwa na hali nzuri ya kiuchumi na ilidai kodi zaidi ili kufidia hasara na uharibifu uliofanywa katika makoloni yake ikiwemo Marekani, lakini Wamarekani walitambua kodi na ushuru huo kuwa si halali na kwamba ni kinyume cha sheria na hawakuwa tayari kutoa ushuru. Jambo hilo liliibua cheche za vita kati ya Marekani na Uingereza, na mwaka mmoja baadaye, hatimaye Wamarekani walitangaza uhuru wao kutoka kwa Uingereza hapo mwaka 1776. Muda mfupi baadaye majimbo ya Kaskazini na Kusini ya Marekani yalijigawa katika sehemu mbili na kuingia katika makabiliano ya wenyewe kwa wenyewe.

Majimbo ya Kusini kwa kiasi fulani yalihesabiwa kuwa koloni la majimbo ya Kaskazini. Uchumi katika majimbo ya kusini uliegemea kwenye kilimo, huku uchumi wa majimbo ya Kaskazini ukitegemea zaidi viwanda. Baada ya Mapinduzi ya Viwanda, majimbo ya Kaskazini hayakuhitaji tena nguvu kazi ya bure na ya bei nafuu ya watumwa kutokana na kusasisha na kuimarisha viwanda vyao, ilhali majimbo ya kusini bado yalihitaji nguvu kazi rahisi na ya bure ya watumwa hao ili kudumisha uzalishaji katika mashamba makubwa ya maeneo hayo; hivyo yaliendeleza mfumo wa utumwa. Ustawi na kupanuka kwa kilimo na utumwa kuliwapa nguvu kubwa sana wamiliki wa majimbo ya Kusini, na watu wa Kaskazini walichelea uasi wa watu wa Kusini; hivyo walifanya jitihada kubwa za kuimarisha nafasi yao ya juu na kwa ajili ya kuyatawala majimbo ya Kusini. Watu wa majimbo ya Kusini waliwatumia watumwa wao weusi, ambao walikuwa wanaume wenye nguvu na maumbo makubwa, kupigana na majimbo ya Kaskazini, na walikaribia kwenye ukingo wa ushindi. Ilikuwa katika muktadha na mazingira haya ndipo Lincoln alipochukua uamuzi wa kupitisha Sheria ya Kukomesha Utumwa. Sheria hii kwa hakika ilikuwa chombo na wenzo wa vita wa Abraham Lincoln. Watumwa walikimbia kwa makundi kutoka Kusini wakielekea katika majimbo ya Kaskazini kwa matumaini ya kuwa huru, na suala hili lilipelekea kushindwa kwa watu wa Kusini mwa Marekani. 

Swali jingine linalojitokeza ni kwamba, watumwa walioachiliwa mwishoni mwa vita walikuwa na hali gani? Je, baada ya miaka mia nne ya utumwa, walipata nchi nyingine yao wenyewe isiyokuwa Marekani? Je, walikuwa na nyumba au maskani  na kazi ya kuwapa kipato katika ardhi hiyo? Je, walikuwa na chakula cha kula au kuwalisha watoto wao?

Mwisho wa utumwa huko Marekani ulikuwa mwanzo wa kutangatanga na kutokuwa na makazi, njaa na mashaka mengine mengi kwa watumwa hao. Fikra za kibaguzi za Wamarekani zilikuwa sababu ya watu weusi kutokuwa na hadhi na nafasi yoyote ya maana ya kijamii, na wazungu waliwaona kuwa hatari kwa wafanyakazi weupe na hawakuwa tayari kuwavumilia. Inawezekana vipi kutarajia kwamba, vizazi kwa vizazi ambavyo katika kipindi chote cha maisha yao viliwatumikisha na kuwauza watu weusi kama wanyama, sasa viwatambue kama majirani au wanadamu na wafanyakazi wenzao? Fikra hizi za kibaguzi zilipelekea kubuniwa sheria za kutenganisha baina ya watu weupe na watu weusi. Kulingana na sheria hizo zinazojulikana kama Sheria za Jim Crow (Jim Crow laws), jamii za watu weusi na weupe zilitenganishwa katika nyanja zote za kijamii. Wazungu hawakuwa wakitumia hata bomba zilizotumiwa na watu weusi kwa ajili ya kunywa maji, na watu weusi hawakuruhusiwa kutumia bomba na vyombo ya wazungu.   

Baada ya kupita karne nyingi ubaguzi wa rangi bado unaendelea kushuhudiwa nchini Marekani, na hadi sasa Wamarekani weusi wanateswa, kukandamizwa na kudhulumiwa. Kidhahiri inaonekana kwamba utumwa umekwisha, lakini ukweli ni kwamba watu huru weusi wa leo wanaendelea kukabiliana na matatizo mengi ya ubaguzi wa rangi. Usalama wa watu hawa unatishiwa hata na polisi na vikosi vya serikali. Hii leo, karibu miaka mia mbili imepita tangu mwanadamu atangaze mwisho wa utumwa kwenye karatasi na nyaraka rasmi, lakini katika ulimwengu wetu wa leo, sio tu watu weusi, bali wanadamu wa rangi na mbari zote, jinsia na rika tofauti wanaweza kufanywa watumwa. Kwa mujibu wa baadhi ya takwimu zinazotolewa na mashirika ya kupambana na utumwa, takriban watu milioni ishirini na nne wanaishi katika hali ya utumwa kwa sasa. Hii ina maana kwamba, utumwa haujaisha, bali umebadilishwa sura na muundo wake. Hii leo wako wanadamu, wanaume, wanawake na watoto wengi wanaolazimishwa kufanya kazi za sulubu. Wanadamu hawa wanafanyishwa kazi maisha yao yote bila kupewa ujira na malipo ya jasho lao. Baya zaidi ni kwamba, katikati mwa bara la Ulaya, kuna maduka ambako watu hutangazwa na kuuzwa kama bidhaa. Jana watumwa walikuwa wakipigwa chapa cha moto, na hii leo bei yao inaainishwa kwa kuwekewa alama za msimbo upau (barcode).

Ni kweli kwamba wanadamu wamekuwa wakiwajihiana na utumwa katika kipindi chote cha historia, lakini jambo muhimu zaidi ni jinsi ya kukabiliana na uovu huo. Miaka 1400 iliyopita, wakati Uislamu ulipodhihirfi katika Bara Arabu, jamii zilikuwa na ufahamu mdogo kuhusu utumwa. Ijapokuwa jambo hili baya na ovu lilikuwa likipingana na sheria na mafundisho ya Uislamu, lakini badala ya kufuta utumwa papo na hapo na kuwaacha watumwa bila makazi, kazi, mapato na kadhalika, Uislamu uliweka sheria za kutokomeza kabisa mizizi na chanzo cha ubaguzi wa rangi, na hulka ya mabwana ya kujiona bora zaidi ya wanadanu wengine. Uislamu ulikataza na kuharamisha watu huru kufanywa watumwa, na njia pekee ya kuwafanya watumwa ilikuwa ni kumkamata kafiri katika vita dhidi ya Waislamu. Hii pia haikuwa na maana kwamba mateka wote wa vita walikuwa wakifanywa watumwa, la hasha, kwa sababu ilitokea mara nyingi kwamba Mtukufu Mtume, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake, aliwaachia huru mateka wa vita kwa udhuru mdogo au hata bila ya udhuru wowote.

Kwa upande mwingine, Uislamu ulikataza dhulma na ukatili dhidi ya watumwa na kuwapa haki zao za binadamu. Uliwapa haki ya kuoa na kuanzisha familia, na kukomesha kuuzwa kwao bila familia zao. Bwana na mmiliki yeyote hakuwa na haki ya kumtenganisha mtumwa na familia yake na kisha kumuuza. Kwa mujibu wa sheria hizo za Uislamu, ikiwa bwana au mmiliki angetenda vibaya na kumdhuru mtumwa wake, hata kwa kumvunja jino tu, mtumwa huyo angeachiwa huru na tangu hapo hukubaliwa kama mtu huru katika jamii. Mabwana hawakuwa na haki ya kuwalazimisha watumwa kufanya mambo ambayo yalikuwa nje ya uwezo wao. Nafsi na uhai wa watumwa ulikuwa na thamani sawa na uhai  wa wanadamu wengine, na hakuna bwana aliyekuwa na haki ya kumuua mtumwa wake. 

Uislamu uliwafundisha wafuasi wake kwamba, hakuna mwanadamu aliyebora kuliko mwingine, na kwamba hakuna kitu chochote kama rangi ya ngozi, familia na ukoo, mali au hata jaha na madaraka kinachopasa kuwa sababu ya mwanadamu kujivuna na kujiona bora na juu ya wanadamu wenzake, na kwamba jambo pekee litakalomfanya mtu kuwa bora kuliko wengine mbele ya Mwenyezi Mungu ni imani na uchamungu; na sifa hii anaweza kuwa nayo zaidi mtumwa kuliko bwana na mmiliki wake. 

Uislamu umethamini kazi na kustawisha ardhi, na unapendekeza kwamba mfanyakazi anapaswa kulipwa matunda ya kazi yake  kabla ya jasho kukauka kwenye paji la uso wake. Dini hiyo pia imebuni njia nyingi kwa ajili ya kuwakomboa watumwa na imeitambua kitendo hicho kuwa ni kafara ya dhambi nyingi. Kwa msingi huo pale Mwislamu alipokuwa akitenda dhambi, njia fupi ya kuepuka adhabu ya Mwenyezi Mungu ilikuwa kumwachia huru mtumwa mmoja au zaidi.

Hivyo, badala ya kupiga marufuku jambo hilo ovu na baya ambalo lilisababishwa na baadhi ya mambo, Uislamu ulianzisha vita na kupambana na sababu na vyanzo vya utumwa yaani ghururi, kupenda ukuu, kujiona bora zaidi ya wanadamu wengine kiburi, kupenda jaha na ukubwa, maslahi haramu ya kibinafsi na kadhalika. Uislamu ulipambana dhidi ya haya yote na matokeo yake ni kukomesha kivitendo mfumo wa utumwa katika jamii za Kiislamu.    

 

Tags