Dec 13, 2021 14:13 UTC
  • Zainab, Simba Jike Binti wa Simba wa Mwenyezi Mungu

Tarehe 5 Jamadil Awwal inasadifiana na siku aliyozaliwa Bibi Zainab, simba jike binti wa Simba wa Mwenyezi Mungu.

Katika siku hiyo mwaka wa tano Hijria Mwenyezi Mungu SW alimtunuku Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatima binti Muhammad (saw) mtoto wa kike ambaye walimpa jina la Zainab. Alizaliwa baada ya kuundwa dola la kwanza la Kiislamu mjini Madina ambalo lilitokana na mapinduzi makubwa ya kiroho duniani na yaliongozwa na baba yake, Mtume wa Allah, Muhammad bin Abdullah. Bibi Zainab (as) alizaliwa na kukulia katika familia ambayo ilikuwa kitovu cha historia. Babu yake mtukufu alikuwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, baba yake, Ali bin Abi Twalib, alikuwa Mwislamu wa kwanza na wasii wa Mtume (saw); na mama yake, Fatimatul Batul (as) alikuwa binti kipenzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na mbora wa wanawake wote duniani. Zainab alirithi sifa za babu, baba na mama yake watoharifu.

Katika kipindi cha miaka mitano ya serikali ya baba yake, Ali, Zainab alikulia katika nyumba ya kiongozi mkubwa zaidi wa kisiasa na kiroho katika ulimwengu wa Kiislamu, yaani Amirul Muuminin (as). Katika kipindi hicho chote alishiriki katika harakati zote muhimu za kisiasa na kijamii hususan katika medani ya elimu na malezi, hadi wakati wa tukio adhimu la Karbala.

Historia ya Uislamu imesajili majina ya wanawake wengi waliokuwa na imani na waliojitolea ambao walibadili mkondo wa historia kwa mahudhurio yao makubwa katika medani za siasa na jamii. Wanawake hawa hawakuandika majina yao katika historia bali wao wenyewe waliandika na kutengeneza historia. Hapana shaka kuwa Zainab (as) ni miongoni mwa wanawake vigezo na wanaopaswa kuigwa na wanawake na wanaume wote wanaopigania haki na uadilifu na kukabiliana na dhulma na uonevu. Zainab binti Ali (as) alikuwa mwanamke wa zama zilizopita, zama za sasa na zijazo, kwa sababu aliwakilisha haki, uadilifu, utukufu wa mwanadamu, kupigania uhuru na kupambana na dhulma; masuala ambayo hayana kipindi maalumu wala zama na mahala makhsusi. Ni kutokana na ukweli huo ndiyo maana inasemwa kuwa, watu adhimu daima huwa juu ya historia.   

Kipindi cha utotoni Zainab alikulia katika mikono iliyojaa upendo na nuru ya babu yake, Mtume wa Allah, na baba yake Imam, khalifa na wasii wa Mtume. Alikulia katika mikono maasumu na mitakatifu, na akajipamba kwa sifa zote za ukamilifu wa kiroho na kimaanawi. Alirithi elimu na maarifa ya babu yake, zuhudi na ibada ya baba yake, kujitolea na kujisabilia kwa mama kipenzi, subira na uvumulivu wa kaka yake mkubwa, Hassan na ushujaa wa kaka yake kipenzi Hussein (as).

Miongoni mwa nukta muhimu katika maisha ya Bibi Zainab (as) ni mapenzi yake makubwa kwa kaka yake Hussein (as). Mapenzi hayo yalikuwa makubwa sana kiasi kwamba, Bibi Zainab aliweka sharti la kuolewa na mumewe, Abdullah bin Jaafar kuwa ni kufuatana na kaka yake, Hussein, mahala popote atakapokwenda.     MUZIKI

Hii leo imepita miaka 1400 tangu baada ya kufariki dunia Bibi Zainab (as) lakini mwanamke huyo shujaa na mtukufu angali anatoa ilhamu na kutia roho mpya katika historia ya mwanadamu. Alikuwa kigezo bora, hatibu hodari, mwalimu mahiri na mwendelezaji wa harakati adhimu ya mapambano ya Ashura. Mahudhurio yake makubwa katika harakati ya mapambano ya Imam Hussein (as) katika medani ya Karbala ambapo kundi dogo la waumini wa kweli, wakiongozwa na Bwana wa Mashahidi, lilisimama kupambana na dhulma, uonevu na upotoshaji wa dini, ni kigezo na ruwaza njema ya kuigwa na wapigania haki kote duniani. Zainab alikuwa simba wa kike katika matukio yote ya Karbala tangu mwanzoni mwa mapambano hayo, wakati alipokuwa katikati ya maiti za mashahidi wa haki, pindi alipochukuliwa mateka na utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya (laana za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) hadi alipokuwa katika kasri la mfalme dhalimu, Yazid bin Muawiya, huko Sham.

Mwangwi wa sauti ya simba jike ya Zainab katika kasri la dhulma na giza la Yazid bado unasikika hadi hii leo. Wakati Bibi Zainab alipoingizwa katika kasri la Yazidi katika msafara wa mateka huku wajukuu wa mtume (saw) wakiwa amefungwa kamba mikononi, hadhirina walikuwa wakisubiri kuona Bibi huyo shujaa akianguka chini mbele ya mfalme katili na kuomba msamaha. Kinyume chake, Zainab alitikisa nguzo za kasri hilo lililokuwa katika kilele cha sherehe za kuuawa na kukatwa kichwa mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as), ambacho kilitangulia msafara wa mateka kikiwa kimetundikwa juu ya mshale. Alisimama kishujaa na kumlaani mtawala huyo dhalimu na kutoa hotuba kali iliyovuruga sherehe ndani kasri la Yazid mlaaniwa. Zainab alisema katika aliyoyasema: "Ewe Mola Mlezi! Chukua haki yetu kwa waliotudhulumu, na teremsha hasira na ghadhabu yako kwa mtu aliyemwaga damu yetu katika ardhi na kuwaua wafuasi wetu, Ahlulbait".

Hotuba kali ya Bibi Zainab ndani ya kasri la Yazid iliteteresha nguzo za utawala wa Banii Umayya. Akitumia lugha fasihi iliyowakumbusha watu hotuba tamu na za aina yake za baba yake, Ali bin Abi Twalib, Zainab alimdunisha mtawala Yazid kwa kusema: "Misiba adhimu imetulazimisha kuzungumza na mtu duni kama wewe. Inasikitisha kuona watu adhimu wa kundi la Mwenyezi Mungu wakiuawa kwa mikono ya shetani. Mikono yako iliyotenda jinai, imejaa damu yetu sisi Ahlulbait wa Mtume, na mdomo wako umejaa nyama zetu."

Baada ya hapo Bibi Zainab alimpasha Yazid kwamba, vitimbi vyake kamwe haviwezi kufuta jina na Uislamu na Ahlubaiti wa Mtume (saw) katika historia kwa kusema: "Fanya vitimbi kadri uwezavyo, na jitahidi mpaka mwisho lakini elewa kwamba, hutaweza kufuta utajo na jina letu. Hutaweza kuangamiza wahyi na ufunuo wetu, na kamwe hutafikia matarajio yako ya siku nyingi.... Akili yako ni finyu, kipindi cha maisha yako kinakwisha haraka, na tapo lako linatoweka na kusambaratika. Elewa kwamba itafika siku ambapo mwenye kunadi atanadi: Laana za Mwenyezi Mungu ziwashukie madhalimu."

Bibi Zainab (as) alikamilisha hutuba yake katika kasri la mtawala Yazid kwa kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa kuanza maisha ya Ahlubaiti wa Mtume (saw) kwa saada na maghufira, na kuyakamisha kwa daraja ya juu ya kuuliwa shahidi. Hivi ndivyo Bibi Zainab alivyokuwa juu ya historia. Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya simba wa kike binti wa Simba wa Mwenyezi Mungu.       >>

Tunatoa mkono wa kheri kwa Waislamu wote dunia kwa mnasaba wa kuadhinisha siku aliyozaliwa mjukuu huyu wa Mtume wetu Muhammad (saw).