Jan 30, 2022 09:04 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuondolewa ujahili mamboleo

Neno 'ujahili' au ujinga ambalo limetumika katika Qur'ani na Hadithi na hata katika vitabu na nyaraka nyingi za kihistoria lina maana nyingi.

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwezi Februari 1979 uliibua sauti mpya duniani. Imam Khomeini (MA) ambaye aliongoza mapinduzi hayo alitoa pigo kubwa kwa ujahili mamboleo ambao ulikuwa umeshamiri na kuziathiri nguzo zote za utawala nchini Iran.

Ujahili hauna maana ya kutokuwa na elimu pekee bali ni hali ya kiroho na kimaanawi ambayo humuathiri mwanadamu na kumfanya awe mkaidi na kutotii amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu. Ujahili umekuwepo duniani kwa sura mbalimbali katika zama tofauti ambapo ujahili wa mwanzo ulionekana katika kipindi cha kabla ya kubaathiwa na kuteuliwa Mtume Mtukufu (saw). Qur'ani Tukufu inautaja ujahili huo kuwa ujahili wa kwanza na wa zamani. Katika ujahili huo, watu walikataa kumwabudu Mwenyezi Mungu mmoja na kuamua kuabudu masanamu sambamba na kuwa na misimamo mikali ya taasubi zisizo na msingi. Katika zama hizo, ujinga, utumiaji mabavu, ufisadi, ufuska na kutodhibiti matamanio ya nafsi vilimtawala mwanadamu na kumfanya asiweze kutumia akili ipaswavyo kiasi cha kumfanya apuuze maadili na utu alioumbwa nao. Ufisadi, ufuska, ukaidi, taasubi za kikabila, kiburi na ubinafsi, unyanyasaji dhidi ya majirani, dharau na ukatili dhidi ya wanawake na maovu mengine mengi yalikuwa yamefika kileleni, kiasi kwamba baba, alikuwa akimzika hai kaburini binti yake asiye na hatia na wakati huohuo kujivunia ukatili na unyama huo. Katika mazingira hayo ya kusikitisha, Mungu alimtuma Nabii wa nuru na rehema, wema na ubinadamu (saw) ili aje awaokoe wanadamu na kuwatoa katika maisha hayo ya unyama. Baada ya kuteuliwa na Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad al-Mustafa (saw) kupitia ujumbe wake wa mbinguni aliweza kubadilisha ukaidi, chuki kali na ufisadi wa watu hao wajinga na kuwasha mwanga wa wongofu katika nyoyo zao, na bila shaka alistahimili matatizo na mateso mengi katika njia hiyo.

Alibadilisha fikra na imani za kijahilia na kuweka mahala pake ucha-Mungu, ukweli, uaminifu, rehema, heshima kwa familia, wema kwa majirani, kujiepusha na kula vyakula vilivyoharamishwa na mali ya mayatima, kujiepusha na ufisadi na uasherati, na kuhimiza kumtumikia Mwenyezi Mungu. Kutokana na subira kubwa aliyokuwanayo Mtume Mtukufu (saw) na maadili yake ya hali ya juu, na licha ya mateso yote aliyopata kutoka kwa makafiri, lakini alifanikiwa kuunda jamii ya kwanza ya Kiislamu, kueneza Tauhidi na kubuni serikali ya ya kwanza ya Kiislamu  bila ya vita wala vurugu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema hivi katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani: Yeye ndiye aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hekima, ijapokuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri. (Surah Juma'ah, aya ya 2)

Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alianzisha serikali yenye ukarimu, inayoongoza kwenye njia nyoofu, yenye ubinadamu, inayohuisha utu wa mwanadamu na inayoheshimu wanawake, na ambayo ilifanikiwa kubadilisha upendo na ukatili na kuwafanya Waislamu kuwa ndugu.

Ujahili au kwa maneno mengine ujinga, hata hivyo, hauhusishwi tu na zama za Mtume (S.A.W), bali kwa ujumla, unahusiana na wakati na zama zozote ambapo jamii ya mwanadamu huvuka mipaka ya thamani za kimantiki na kukanyaga thamani za kiutu na kiroho.

***********

Karne 14 zilikuwa zimepita tangu kutokea Mapinduzi ya Kiislamu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na ujahili mamboleo ulikuwa umekita mizizi na kuenea katika kila pembe ya dunia. Pia kulikuwa na utawala wa kifalme nchini Iran. Nasaba na ukoo wa kifalme wa Pahlavi na wale waliofungamana na utawala wake walikuwa wakiishi kwenye kilele cha starehe na anasa, ilihali watu wa kawaida katika miji mingi ya Iran walikuwa wakiishi kwenye hali duni na kutokuwa na hata vifaa na suhula za msingi kabisa za kuendeshea maisha.

Shah alijiita kuwa Mwislamu katika hali ambayo alifungamana moja kwa moja na ukoloni wa Waingereza na baadaye wa Marekani na kuegemea sana utamaduni wa Magharibi. Kauli mbiu ya utawala wake ilikuwa ni kuifanya jamii ya Iran kuwa ya Kimagharibi "kutoka kichwani hadi miguuni" na wala haukuacha kufanya juhudi zozote za kuitwisha jamii ya Iran ambayo wenyeji wake wengi ni Waislamu, utamaduni wa Magharibi. Mfano wa wazi wa fikra hii ya ujahili ilikuwa ni kupiga marufuku na kuondoa vazi la stara kwa mwanamke wa Kiislamu yaani hijabu kwenye vichwa vya wanawake nchini.

Takwimu zinazohusiana na maeneo ya ufuska na uasherati, maduka ya vileo, kasino, vilabu na kumbi za densi, utumiaji wa madawa ya kulevya hasa miongoni mwa vijana na ufisadi zinaonyesha kuwa utawala wa Pahlavi ulikuwa unapinga kwa makusudi mafundisho ya dini  na Uislamu, na ulitumia fedha nyingi ili kufikia lengo hilo. Ni wazi kuwa kuzama katika ujahili na ujinga maana yake ni  kuwa na "utawala unaoeneza ufuska na ufisadi" katika jamii.

Ayatullah Khamenei anasema ifuatavyo kuhusu ufisadi uliokuwa umeenea nchini katika kipindi cha utawala wa Shah: "Ilikuwa ni propaganda iliyopangwa vizuri kwa ajili ya kuwashawishi watu wafanye uasherati, ufuska na anasa. Hata katika mitaa ya watu masikini na iliyoachwa nyuma kimaendeleo, mikakati na vituo vya ufuska na anasa vilianzishwa na kuenezwa kwa makusudi. Vituo hivyo vya ufuska vilianzishwa hasa katika mazingira ya mikusanyiko ya vijana kama vile vyuo vikuu ambako kwa kawaida hisia na matamanio ya ujanani huwa ni ya kiwango cha juu, ili kuchochea na kueneza ufisadi katika tabaka la vijana.  Wakati tabaka la vijana linapokumbwa na ufisadi na ufuska, bila shaka hakuna taifa zuri linaloweza kutokana na vijana wa ina hiyo wala mapambano hayawezi kufanyika."

Hazina ya taifa haikuwa kwa ajili ya ustawi na kuboresha maisha ya wananchi, bali ilikuwa ni kana kwamba ni akaunti binafsi ya mfalme na aliitumia kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake mengi ya kibinafsi na kiufuska. Alitumia sehemu kubwa ya fedha hizo kwa ajili ya kudhamini bajeti na matumizi ya kifedha ya vyuo na taasisi za kisayansi za Marekani na Uingereza ili kuwaridhisha mabwana zake katika nchi hizo za Magharibi. Ubadhirifu wa pesa kwa ajili ya sherehe za kifalme na ununuzi wa nyumba nyingi za kifahari huko Merikani na nchi za Ulaya ni mfano mmoja tu wa uporaji na matumizi makubwa ya mfalme na familia yake kutoka hazina ya kitaifa, wakati ambao vyuo vikuu vya umma havikutengewa hata chumba kimoja kidogo tu kwa ajili ya wanachuo kutekelezea humo ibada zao za kidini!  Mwenendo huo wa Shah kughiriki kwenye utamaduni wa Magharibi na kukidhi bila kusita matakwa ya Marekani na Israel uliwakasirisha sana watu na wanazuoni nchini. Ghafla, na katika mazingira hayo ya kusikitisha Imam Khomeini (MA) alisimama na kutangaza upinzani wake kwa mfumo wa kifalme. Imam Khomeini alikuwa aarif, mwanazuoni wa ngazi ya juu na msomi wa sheria za Kiislamu ambaye aliyapa mafundisho ya dini umuhimu mkubwa na kuamini kuwa hayakupasa kutengenishwa na siasa.

Katika hotuba yake ya kwanza ya hadhara, Imam aliufananisha utawala wa Shah na utawala wa Bani Umayya na Yazid. Alitoa wito kwa wananchi waamke na kumshauri Shah aache utegemezi wake kwa ukoloni wa Mashariki na Magharibi na urafiki wake na utawala mbovu na wa kikatili wa Israel, na awategemee wananchi wa Iran. Hotuba ya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ilimkasirisha sana Shah ambaye tangu wakati huo alianzisha ukandamizaji na mauaji ya umati dhidi ya wanazuoni. Vijana wengi waliuawa shahidi katika mikutano ya hadhara na maandamano makubwa, lakini wananchi wa Kiislamu wa Iran walisimama kidete kwa ajili ya ushindi na kufanikisha harakati hiyo iliyofanana na ile iliyoanzishwa na Imam Hussein (as) dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Yazid. Hatimaye, kufuatia kutoroka Shah kutoka Iran, Mapinduzi ya Kiislamu yakiongozwa na Imam Khomeini (MA) yalifikia ushindi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikaanzishwa kwa kura nyingi za wananchi.

Fikra za Imamu Khomeini (MA) zilitokana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Suna za Mtume (saw) na Ahlul-Bayt wake watoharifu (as). Imam Khomeini, ambaye alikuwa na haiba na shakhsia ya kidini, alisimama mbele ya mataghuti kama walivyofanya Mitume wa Mwenyezi Mungu ili kuhuisha amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu. Alitangaza demokrasia ya kidini ulimwenguni kama kielelezo cha serikali ya Kiislamu, na kuzima utamaduni wa Magharibi na ujamaa wa Mashariki, ambazo zilikuwa nguvu kuu duniani wakati huo.

Mapinduzi ya Kiislamu yakiongozwa na Imam Khomeini na baada yake Ayatullah Khamenei, tangu mwanzo wa kuibuka kwake hadi sasa, kwa upande mmoja yamekuwa yakipambana dhidi ya madhehebu potofu na tafsiri isiyo sahihi ya Uislamu kama ile inayoenezwa na Uwahabi, Uislamu wa Kimarekani na uliberali, na kwa upande mwingine dhidi ya utamaduni wa Magharibi, na hivyo kubatilisha fikra, thamani duni na imani zao potofu ili kuweka wazi mpaka uliopo baina ya Uislamu halisi ulioletwa na Mtume na ujahili huo.

Pamoja na hayo lakini jambo la kusikitisha ni kuwa ujahili huo mamboleo ungali unauandama ulimwengu kupitia anasa, ufuska na maisha ya kimatamanio. Leo hii, nchi zinazodai kuwa na ustawi na maendeleo zenyewe ni wakoloni wanaokanyaga na kukandamiza thamani za kiutu kupitia nara za uongo eti za kueneza demokrasia, utetezi wa haki za binadamu na uhuru duniani. Palestina imekuwa mikononi mwa utawala wa Israel ambao kwa miaka mingi umekuwa ukiua watoto wachanga na Wapalestina bila huruma. Udini unachukuliwa kuwa jambo na jukumu la mtu binafsi linalozingatiwa tu katika makanisa na mahekalu na wakati huohuo kuchochewa matamanio, ufuska na kila aina ya ufisadi na upotovu unaoenezwa kwa kila mbinu ulimwenguni ili kusahaulisha amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei anasema kuhusiana na suala hilo: “Kinachokuzwa leo hii na vyombo vya siasa vya Magharibi ni ujahili mamboleo na ujinga uleule ambao Mtume (saw) alitumwa kwa ajili ya kuuondoa katika maisha ya jamii ya mwanadamu. Alama za ujinga huo zinaonekana wazi katika ulimwengu wa leo na katika ustaarabu wa kawaida na potovu wa Magharibi. Dhulma ile ile, ubaguzi uleule, kutojali utu wa binadamu na kughiriki katika masuala na matamanio ya kijinsia ni miongoni mwa alama hizo. Moja ya dalili za ujinga na ujahili wa kwanza ni wanawake kutembea uchi. Leo pia, moja ya nembo muhimu za ustaarabu wa Magharibi ni wanawake kutembea wakiwa uchi. Huu ndio ule ule ujinga wa mwanzoni, ila ni ujinga ambao katika zama hizi umeweza kuenezwa na kujizatiti katika jamii ya mwanadamu kupitia silaha ya propaganda za kisasa, ili kuficha ukweli machoni pa watu. Sisi Waislamu lazima tuelewe haya, tanapasa kuyajue haya."

Tags