Feb 01, 2022 10:29 UTC

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Mwaka 57 baada ya Hijra ya Mtume SAW ya kutoka Makkah kuelekea Madina, katika siku ya kwanza ya mwezi uliojaa fadhila wa Rajab, ulimwengu uling'ara kwa kuzaliwa nuru ya mmoja wa watu watukufu katika kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW.

Katika siku hii yenye baraka, Mtoto kutoka Nyumba ya Mtume Muhammad SAW alizaliwa na sawa na Ahlul Bayt wengine wa Mtume SAW, akawa tawi katika matawi maridadi kwenye historia ya Uislamu. Yeye ni mwana wa Imam Sajjad AS na ni maarufu kwa jina la Baqir.

 Jina la Baqir lina maana ya mtu mwenye mwenye nuru inayonawirisha. Mtukuku huyo alitajwa kuwa mtu aliyechanua na kunawirisha elimu. Alikuwa stadi katika elimu mbali mbali na alitajwa kuwa ni bahari ya elimu. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za pongezi kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Muhammad Baqir AS.

@@@@

Baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Sajjad AS, Imam Muhammad Baqir AS alichukua jukumu muhimu la uongozi wa Ummah wa Kiislamu kwa muda wa miaka 19. Kipindi hicho kiliambatana na matukio ya kisiasa na kubadlishwa utawala kutoka ukoo wa Bani Umayya kwenda kwa ukoo wa Bani Abbas.

Katika kipindi hicho, Imam Baqir AS alitumia nafasi yake kueneza ukweli kuhusu elimu na utamaduni wa Kiislamu. Imam Baqir AS alianzisha harakati ya kiutamaduni na kisayansi katika ulimwengu wa Kiislamu na matunda ya juhudi zake yalionekana katika nyakati zilizofuata.

 Imam Baqir alijitahidi sana katika masuala ya elimu na utamaduni ili aweze kukabiliana kikamilifu na imani batili na potofu katika jamii. Aidha alikusudua kueneza fikra tukufu na a'ali ya Bwana Mtume na Watu wa Nyumba yake kupitia kuanzisha chuo kikubwa cha elimu na utamaduni.

 Sheikh Tousi, mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu amewataja wanafunzi bingwa wa Imam Baqir AS kuwa ni watu 462. Vigogo na shakhsia wakubwa wa kisiasa wa zama hizo wote walifika mbele ya Imam Baqir AS kupata angalau tone moja la bahari yake pana ya elimu. Watu kama vile Jabir bin Yazid Jofi, Zohri, Abu Hanifa, Anas ibn Malik na Shafi ni kati ya wanazuoni walionufaika na hazina kubwa ya kielimu ya Imam Baqir AS.

 

Muhammad Ibn Talha Shafi'i katika kuelezea sifa za Imam Baqir anaandika: "Alikuwa mwenye kunawirisha elimu. Hotuba zake zilikuwa fupi lakini zilizojaa maana na moyo wake ulijaa mwanga. Alikuwa ni mwenye amali njema na zilizopambwa. Alikuwa na akhlaqi njema na alitumia umri wake katika kutii amri za Mwenyezi Mungu. Alikuwa amejikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na alistahiki uongozi."

 Uimamu wa Imam Mohammad Baqir AS ulianza katika kipindi ambacho, Ummah wa Kiislamu ulikuwa unakabiliwa na changamoto za kina za kiitikadi na kifiqhi baina ya makundi mbali mbali ya Kiislamu. Kuwepo Imam Baqir AS katika medani kulipelekea kuchukuliwa hatua muafaka katika kubainisha mitazamo ya Ahlul Bayt wa Mtume SAW.

 Katika kipindi cha muda mfupi, Imam aliweza kusambaratisha kwa kiasi kikubwa itikadi za makundi potofu. Katika zama za Uimamu wake na mwanawe mwenye adhama Imam Sadiq AS, hitilafu na mivutano katika utawala wa kisiasa zilifika kileleni na hali ya kisiasa na kijamii kukumbwa na ukosefu wa uthabiti. Natija yake ilikuwa ni kwamba Makhalifa walikuwa wakibadilishwa kwa kasi kiasi kwamba katika kipindi cha Uimamu wa Imam Baqir AS, makhalifa watano walitawala.

 Kwa hivyo Imam alipata fursa isiyo na kifani kwani alijiweka mbali na mashinikizo ya kisiasa ya watawala na kuwavuta karibu naye wanazuoni wakubwa pamoja na wasomi bingwa wa sayansi na hekima. Wanazuoni waliokuwa karibu na Imam waliweza kunufaika kwa njia ya moja kwa moja na mafundisho yake ya Kiislamu aliyokuwa akiyabainisha kwa lugha fasaha.

 Katika kipindi cha Imam Baqir AS, hujuma ya kiutamaduni iliyokuwa imeratibiwa na Bani Umayyah ililenga kuvuruga itikadi za kidini za Ummah wa Kiislamu. Aidha katika kipindi hicho jamii ya Kiislamu ilishuhudia kuibuka nadharia zisizo sahihi za kifalsafa kuhusu misingi ya itikadi.

 Ni kwa sababu hii ndio baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu wakachanganyikiwa katika jitihada zao za kuutafuta ukweli. Imam Baqir AS kwa kutegemea dalili za kimantiki na zenye kupambanua alichambua fikra hizo potofu za kifalsafa na kuweza kubainisha nukta pofotu katika nadharia hizo mpya. Mtukufu huyo aliwatia kiti moto wanafalsafa wasiokuwa wa kidini na kuweza kubainisha mitazamo ya itikadi sahihi za Kiislamu. Kutokana na mazingira hayo, sayansi za kalam au misingi ya itikadi ziliweza kuvuma katika zama za Imam Baqir AS.

 

 Imam Baqir AS alikuwa miongoni mwa watu na daima aliandamana nao. Pamoja na shani na adhama yote aliyokuwa nayo, mtukufu huyo alikuwa akiwahudumia watu wa tabaka dhaifu na waliotengwa katika jamii. Alikuwa akiketi na watu waliosahaulika kabisa, kuzungumza nao na kutatua matatizo yao. Muamala uliojaa ukarimu na unyenyekevu wa mtukufu huyo uliwapelekea watu wengi kumfuata.

 Imam Baqir AS hakumuacha bila jibu kila aliyekuja kwake kuomba msaada na aliwasisitizia wengine kuhusu umuhimu wa kuwasaidia na kuwaheshimu wahitaji. Kutokana na muamala wake mwema ulioambatana na adabu na mapenzi, Imam Baqir AS aliweza kuwavutia hata wapinzani wake. Katika historia tunasoma kuwa mtu mmoja kutoka Sham ambaye hakuafikiana kiitikadi na Imam Baqir AS alikuwa akifika katika vikao vya mtukufu huyo na kunufaika navyo.

 Mtu huyo anasema sababu ya maingiliano yake mazuri na Imam Baqir AS ni akhlaqi njema na muamala wake mzuri. Alikuwa akimwambia hivi mtukufu huyo: "Wewe unabainisha masuala kwa njia fasaha na ya wazi. Unatumia maneno mazuri katika kauli zako. Ni kwa sababu hii ndio napata furaha ya kushiriki kwenye vikao vyako."

 Pamoja na shughuli zake nyingi za kielimu na kiutamaduni, Imam Baqir AS hakughafilika na masuala ya kisiasa na alikuwa akiwakosoa sana watawala wa kiimla na madhalimu wa zama zake. Katika harakati zake za kuwazindua Waislamu kisiasa, Imam alibainisha sifa za viongozi wema ili watu waweze kuwatia kwenye mizani watawala na wafahamu udhaifu na upotofu wao.

Imam Baqir anasema: "Uongozi wa jamii unamstahikia mtu mwenye sifa tatu. Kwanza ni ucha Mungu ili takwa iweze kumkinga na mitihani ya madaraka kama vile kutumbukia katika mtego wa ufisadi. Pili awe mstahamilivu ili aweza kuzuia hasira zake. Tatu aamiliane na watu anaowatawala kama baba mkarimu na awe na tabia nzuri."

 

 Wapenzi wasikilizaji kwa mara nyingine tunatoa mkono wa pongezi, kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Baqir AS na tunaendelea kipindi cha leo kwa maneneo yafuatayo ya mtukufu huyo:

 As'wad bin Kathiri anasema: "Nilimpelekea Imam Baqir AS malalamiko yangu kuhusu mambo niliyoyahitaji na dharau wanayonifanyia ndugu zangu. Mtukufu huyo akasema: "Ni ndugu gani huyo anayekujali unapokuwa tajiri na mwenye uwezo lakini anakupuuza na kukudharau unapokuwa kwenye dhiki?" Kisha alitoa amri nipewe msaada wa dirhamu 700 ili nitatulie matatizo yangu na akaniambia, "tujulishe hali yako itakavyokuwa."

 Mbali na kubobea sana katika elimu, Imam Baqir AS alipambika pia kwa sifa bora za kimaadili na ukamilifu wa kibinadamu. Hata lakabu yake ya Baqir nayo inaashiria kubobea na kutabahari kwake mno katika elimu. Baqir ni neno la Kiarabu lenye maana ya mbukuaji na mpambanuaji wa kina wa mambo.  Muhammad bin Abdul Fattah, mmoja wa wanavyuoni wa madhehebu ya Hanafi anasema: Imam Baqir alipewa lakabu ya Baqirul Ulum kutokana na kwamba alikuwa akifukua hazina zilizokuwa zimejificha za maarifa na hekima.

 Na kwa hakika ni kweli kabisa Imam Baqir AS alikuwa mtu mwenye maarifa na hekima ya hali ya juu. Inaelezwa kuwa, kufanya mzaha mwanaume na mwanamke ni jambo ambalo linawaweka mbali na staha na haya. Abu Basir anasimulia yafuatayo: Nilikuwa katika msikiti wa Kufa nikimfundisha Qur’ani mwanamke mmoja. Ghafla moja nikawa nimefanya naye mzaha na utani. Ukapita muda, kisha siku moja nikapata fursa ya kumtembelea Imam Muhammad Baqir AS mjini Madina. Imam akanilaumu kwa kitendo changu kile. Niliona haya na kuinamisha kichwa changu chini. Imam Baqir AS akasema: Fanya toba, na usifanye tena utani na mzaha na mwanamke ambaye si maharimu wako.

 

Vile vile kutoa nasaha na kumnasihi mtu kutokana na jambo baya au kumzindua kutokana na hatari ya upotofu iliyoko mbele yake, ni jambo jingine muhimu kiasi kwamba, Imam Muhammad Baqir AS anawataja kuwa ni wafanya hiana na usaliti watu ambao wanajizuia kuwanasihi watu wengine. Anasema: "Endapo wasomi wataficha nasaha zao, basi watakuwa ni wenye kufanya khiana."

Tab'an, baadhi ya wakati ni vigumu mtu kukubali nasaha na mwongozo na anapokosolewa hata kwa njia nzuri huwa anachukia na kukasirika. Hata hivyo kuchukia na kukasirika kwake huko inabidi mtu anayetoa nasaha avumilie kwani hatima yake ni nzuri.

 Imam Muhammad Baqir AS ambaye tunakumbusha tena kuwa ni Imam wa Tano kati ya Maimamu 12 kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume SAW amenukuliwa pia akisema: "Wafuate watu ambao wanakulilia wakikutakia kheri, na epukana na watu ambao wanakucheka na ambao wanakutakia mabaya.

 Imam Ja'afar Swadiq AS naye amenukuliwa akisema, baba yangu yaani Imam Muhammad Baqir AS alikuwa akisema: Madhali umekata shauri kufanya jambo la kheri, basi harakisha kulifanya, kwani hujui baadaye nini kitatokea.

Miongoni mwa mambo mengine yaliyopewa kipaumbele na Imam Baqir AS ni kusimama kidete kutetea haki na wakati huo huo kupambana kwa nguvu zote na dhulma.

Imam Baqir alibainisha na kufichua uovu wa watawala wa Bani Umayyah katika minasaba na fursa mbalimbali alizopata. Aliamini kwamba, viongozi na watawala wana nafasi kubwa katika imma ufanisi au kunakamika na kuharibikiwa watu katika jamii wanazoziongoza. Katika zama za Imam Baqir AS kulikuwa na migogoro ya kisiasa ya kugombaniana madaraka watawala wa Bani Umayya.

 

Migogoro hiyo ilitoa mwanya kwa Imam Baqir AS kuweza kueneza mafundisho ya Ahlul Bayt AS. Katika zama hizo, watawala wa Bani Umayyah walishughulishwa zaidi na kuimarisha tawala zao kwa kupambana na mizozo ya kisiasa iliyokuwepo baina yao. Hivyo hali hiyo kwa kiasi fulani ilitoa fursa ya kuenezwa mafundisho ya kiutamaduni na kiitikadi ya watu wa nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

 Moja ya hatari zilizokuwa zikiukabili umma wa Kiislamu wakati huo ni fikra za kupandikiza zilizoingizwa katika umma wa Mtume Muhammad SAW. Hivyo kazi kubwa ya Imam Baqir AS ilikuwa ni kupambana na fikra hizo potofu kwa hoja za kimantiki na alitumia Qur’ani, sunna za Bwana Mtume na sira za Ahlul Bayt AS kuwa nguzo na marejeo makuu ya kutatua migogoro ya kifikra na kiitikadi iliyoukumba umma wa Kiislamu. Aliwaongoza watu vizuri kwa kutumia chemchemu hizo tajiri na zenye thamani kubwa za elimu, hikma na maarifa.

 Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kukukmbuka siku ya kuzaliwa Imam Muhammad Baqir, Imam wa Tano wa Waislamu wa Kishia tukimuomba Allah azidi kuwapa nguvu Waislamu waweze kujikomboa kutoka kwenye makucha ya madhalimu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags