Feb 03, 2022 08:33 UTC
  • Nafasi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Katika Kujitokeza Harakati za Kiislamu Katika Eneo

Kwa ushahidi wa historia, karne ya 20 ilikuwa karne iliyoshuhudia, pamoja na mambo mengine, baadhi ya nchi na madola duniani yakishupalia na kupigania kuwa na nguvu, mamlaka na sauti kubwa zaidi ya nchi zingine.

بسم الله الرحمن الرحیم

لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَیِّنَاتِ وَأَنْزَلْنَا مَعَهُمُ الْکِتَابَ وَالْمِیزَانَ لِیَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ

 Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu

Miaka 13 tu ya umri wa karne hiyo iliyoshuhudia mikasa mingi ilikuwa imepita, pale walimwengu waliposhuhudia Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Kutaka zisitake, nchi nyingi zilijishtukia zimenasa kwenye kinamasi cha vita hivyo; ambapo kwa upande wa Ulimwengu wa Kiislamu, matokeo ya Vita vya Kwanza vya Dunia yalikuwa ni kutoweka kwa Dola Kuu la Othmaniya na kuanza ukoloni katika ardhi za mataifa ya Waislamu. Maeneo mbalimbali ya dola la Othmaniya, ambayo hadi wakati huo yalikuwa yakitaabishwa na uongozi wa kiimla wa masultani wa dola hilo, kuanzia hapo yaliandamwa na dhulma mpya. Yaligawanywa katika sura ya vinchi vidogovidogo na vilivyotenganishwa na kuhodhiwa na pande zilizopata ushindi katika vita, ikiwemo Uingereza na Ufaransa. Uingereza na Ufaransa, ambazo zilikuwa zikihofu kuja kuundwa tena utawala mmoja mkubwa wa Kiislamu, zilijidai kidhahiri kuzipa nchi hizo ndogondogo uhuru wa kujitawala wa kisiasa; lakini ukweli ni kwamba, waliwatawalisha watu ambao waliendeleza siasa zao na kulinda maslahi yao. Kwa upande wa kiuchumi na kiutamaduni, madola hayo ya kikoloni yaliendelea kuzihodhi na kuzidhibiti nchi hizo ndogondogo.

Vita vya Kwanza vya Dunia

 

Katika hali na mazingira hayo, Misri, ambayo ni nchi muhimu na yenye nafasi ya kistratejia katika eneo, ilikoloniwa na Uingereza. Ilikuwa ni katika kipindi cha miaka hiyo, wakati serikali ya Uingereza ilipotoa Tangazo la Belfour ili kuandaa mazingira kwa Mayahudi wa Kizayuni kuivamia na kuipora Palestina.

Kwa upande wa Iran, ijapokuwa wakati vilipoanza na kupanuka vita hivyo vya dunia haikuhusika navyo kwa namna yoyote ile, lakini kwa sababu ya umuhimu wake wa kistratejia, na bila shaka kutokana na udhaifu wa wafalme wake pia, iligeuzwa uwanja wa ingia toka za wanajeshi wa Urusi na Uingereza, kiasi kwamba wakati vita vilipomalizika, karibu ardhi yote ya Iran ilikuwa imevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uingereza.

Miaka 20 baadaye, dunia ilishuhudia Vita Vikuu vya pili vya Dunia, ambavyo vilichukua muda wa miaka sita; na matokeo yake yalikuwa ni Marekani na Urusi kuibuka kuwa madola mawili makuu ya dunia; na kwa mara nyingine tena, fungu la nchi za Kiislamu likaendelea kuwa ni la baa la njaa, janga la maradhi, kuporwa utajiri wao na kukoloniwa.

Maafa ya baa la njaa nchini Iran wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia

 

Baada ya madola ajinabi na ya kigeni kujiingiza katika ardhi za mataifa ya Waislamu na njama zao za kuyatawala na kuyahodhi kiutamaduni mataifa hayo, yalijitokeza ndani ya nchi hizo makundi na mavuguvugu yaliyoamua kutafuta njia ya uokozi kwa watu wao, lakini, kwa kutegemea fikra mbalimbali za kimaada kama Umaksi, Usoshalisti, Uliberali n.k. Baadhi ya makundi hayo yalisahau na kuachana kikamilifu na utambulisho wao wa Kiislamu na kuitakidi kuwa, hakuna suluhisho jengine isipokuwa kuikimbilia Magharibi na utamaduni wa Kimagharibi. Lakini baadhi ya makundi yalijaribu kutumia kwa pamoja na kwa namna ya kuweza kukubalika, Uislamu na fikra hizo za Kimagharibi. Pamoja na hayo, miongoni mwa maulamaa wa Kishia na Kisuni, walikuwepo watu ambao walipigania kurudi kwenye mafunzo asilia ya Uislamu.

Walitokea warekebishaji umma wengi kutoka matabaka tofauti katika nchi za Kiislamu, muhimu zaidi tunayeweza kumuashiria hapa, ni Sayyid Jamaluddin Asad Abadi. Mwanaharakati huo ambaye alisoma katika vyuo vya kidini vya Iran na Iraq, alitumia umri wake wote kufanya safari katika ardhi za mataifa ya Waislamu. Sayyid Jamaluddin alijaribu kila mara kuwazindua na kuwaelewesha Waislamu hatari ya kutawaliwa na kuhodhiwa kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa na Magharibi.

Sayyid Jamaluddin Asad Abadi

 

Alipokuwa Afghanistan alichapisha gazeti, jarida na kuandika vitabu mbalimbali vya dini na historia. Nchini India alipambana na fikra za kimaada na mielekeo ya Kiwahabi; na hatimaye alipokuwa nchini Misri alifanikiwa kuasisi chama, ambacho kilikubalika ndani ya muda mfupi na kuvutia watu wengi; jambo ambalo liliwashtua na kuwatia hofu kubwa wakoloni, mpaka hatimaye wakaamua kumfukuza Misri na kukivunja chama hicho alichounda. Sayyid Jamaluddin aliibadilisha fasihi ya kiashrafu ya Misri iliyokuwa ikitumiwa kusifu na kutukuza wafalme na kuifanya chombo cha umma; na kuitumia kwa ajili ya kutetea na kupigania haki za wanyonge na wanaodhulumiwa.

Nchini Iran, fikra za Sayyid Jamaluddin zilitumiwa na maulamaa wa Kishia na kupelekea kujiri Mapinduzi ya Katiba. Mapinduzi ambayo yaliubadilisha, hata kama ni kwa kipindi kifupi, mfumo wa kifalme kuwa ufalme wa Kikatiba. Kutokana na athari za mapinduzi hayo, kwa mara ya kwanza majlisi ya ushauri ya taifa, yaani bunge la taifa liliweza kuundwa, ijapokuwa lilikuwa zaidi ni la kimaonyesho na la kumtumikia mfalme badala ya wananchi.

Mwaka 1952, Jamal Abdulnasir aliongoza mapinduzi ya kijeshi nchini Misri na kutangaza kufutwa mfumo wa kifalme sambamba na kuanzisha mapambano dhidi ya ukoloni. Kwa muda mrefu kuanzia hapo, Jamal Abdulnasir alitambulika kama kiongozi mkubwa zaidi wa Waarabu katika eneo na aliyependwa zaidi na watu; lakini hatimaye mwamko wa Waislamu wa Misri ulikengeuka na kuacha njia ya Uislamu asilia alioukusudia Sayyid Jamaluddin, kutokana na kupata nguvu fikra za Umajimui wa Kiarabu, yaani Pan-Arabism na vilevile mielekeo ya Kisoshalisti katika mfumo wa uchumi wa nchi hiyo.

Jamal Abdulnasir

 

Tangu mwaka 1948, ulipoanza uvamizi wa Uzayuni wa kimataifa dhidi ya Palestina, Waislamu wamejaribu kwa njia na mbinu mbalimbali kuiondoa dhulma hiyo, lakini kujidunisha na kujidharau na au udhaifu wa tawala za Kiarabu vimekuwa sababu ya kutopatikana hata nchi moja ya Kiarabu ambayo imekuwa na uwezo wa kuitetea ardhi hiyo takatifu. Mwaka 1967, nchi nne za Kiarabu, ambazo ni Misri, Iraq, Jordan na Syria ziliungana kwa madhumuni ya kuutokomeza utawala haramu wa Israel; lakini ulichukua muda wa siku sita tu kabla ya nchi hizo kushindwa vibaya katika vita hivyo. Pigo hilo, mbali na kuwa sababu ya kuporomoka nafasi ya Jamal Abdulnasir ndani ya Misri, lilifuta pia matumani na kuwakatisha tamaa Waislamu wengi duniani. Hali sawa na hiyo ndiyo waliyokuwa nayo Waislamu katika nchi zingine za Kiislamu.

Kambi ya wakimbizi Wapalestina

 

Katika hali na mazingira hayo, ndipo minong'ono ikasambaa duniani kuhusu mapambano ya Waislamu wa Kishia nchini Iran waliokuwa wakiongozwa na mmoja wa mafaqihi wa chuo cha kidini cha Qom. Alimu na faqihi huyo mwanamapinduzi na mpigavita dhulma, ambaye aliutoa waqfu umri wake wote kwa ajili ya Uislamu na Waislamu, alikuwa ni Ruhullah al Musawi al Khomeini. Ayatullah Khomeini, ambaye tokea ujanani mwake alisoma katika vyuo vya kidini vya Qom na Najaf na katika umri wa miaka 27 akawa ameshafikia daraja ya Ijtihad, katika umri huo alikuwa arifu kwa maana halisi, yaani mtu mwenye elimu ya nafsi ya kumtambua Mwenyezi Mungu na pia mwanamapambano aliyepevuka na aliyekamilika. Sambamba na kufundisha na kuandika vitabu vya kidini na kuandaa maulamaa wa baadaye wa Ulimwengu wa Kiislamu, Ayatullah Khomeini aliendesha mapambano pia dhidi ya mfumo wa Ufalme wa Kipahlavi nchini Iran. Ufalme ambao, ulianza kuwepo kwa uungaji mkono wa Uingereza na ukaendelea kutawala Iran kwa msaada wa Marekani na Israel. Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo mkubwa, ubinafsi na kuacha kupambana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ndiko kulikowafikisha Waislamu kwenye hali hiyo ya masaibu na kuwafanya watawaliwe na kila mtu. Katika maandiko yake, Ayatullah Khomeini alibainisha nadharia inayotilia mkazo udharura wa Waislamu wote duniani kufuata "Utawala wa Faqihi"; faqihi ambaye ni alimu zaidi, shujaa na mjuzi zaidi wa hali ya zama zake; na akalieleza hilo kuwa ndio siri ya ushindi wa Waislamu. Baada ya kuaga dunia Ayatullah al-Udhma Bourujerdi, Marjaa na kiongozi wa Waislamu wa Kishia duniani katika zama hizo, Ayatullah Khomeini, alikuwa ndiye mwanazuoni aliyekubalika na kupendwa zaidi na watu nchini Iran, kutokana na harakati zake za kijamii na kisiasa.

Hotuba na misimamo yake madhubuti ya kukabiliana na hatua haramu za utawala wa Kipahlavi iliwapa watu matumaini ya mustakabali wa mafanikio. Kufuatia vita vya siku sita baina ya Waarabu na Israel, Ayatullah Khomeini (RA) alitoa fatua ya kuharamisha nchi za Kiislamu kuwa na miamala ya aina yoyote ile ya kibiashara na Israel na fatua ya kuharamisha pia utumiwaji wa bidhaa za utawala huo wa Kizayuni katika jamii za Kiislamu. Ayatullah Khomeini alitoa fatua nyingine pia iliyojuzisha Waislamu wa Kishia kutoa sadaka na Zaka zao kwa wanamapambano wa Palestina; na hiyo ikawa ni mara ya kwanza kujuzishwa Mashia kutoa Zaka zao kwa wasiokuwa Waislamu wa Kishia.

Kwa uongozi wa Imam Khomeini, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi kamili mwaka 1979, ambao ni mwaka 1357 Shamsia; na ushindi huo ukang'aa mithli ya nuru kwenye macho na nyoyo za Waislamu duniani na kuongeza maradufu matumaini yao ya kujikomboa na udikteta na ukoloni.

Imam Khomeini

 

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Waislamu wa madhehebu ya Shia katika kila pembe ya dunia walipata tena na kujivunia utambulisho wao. Hata ndugu zao wengi wa madhehebu ya Suni pia, waliokuwa wamebainikiwa na kutokuwa na faida fikra na nadharia za Kimagharibi walipata njia mpya kutoka kwenye kitovu cha Uislamu asilia iliyowakomboa na kuwatoa kwenye minyororo ya fikra na nadharia hizo. Waislamu wa Kishia nchini Lebanon, ambao walimtambua rasmi Imam Khomeini (RA) kuwa ni "Faqihi Mtawala", waliungana na kuwa kitu kimoja na wakaasisi kwa idhini yake kundi na harakati ambayo sasa inajulikana kama "Hizbullah"; harakati ambayo hii leo ni adui mkubwa na mwenye nguvu wa kupambana na utawala ghasibu wa Israel.

Huko Palestina, na kwa ilhamu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yalichipua makundi mengi ya wanajihadi, ambao japokuwa walikuwa wafuasi wa madhehebu ya Suni, lakini nyoyoni mwao walikuwa na mapenzi ya Imam Khomeini na malengo yake; na wakazifanya mbinu zake za mapambano na za wafuasi wake kuwa ndio dira yao ya kufuata. Ikiwa katika mazingira magumu ya vita vya kupambana na madola yenye nguvu duniani, Iran haikuacha kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa. Baada ya miaka minane ya vita vikali, ambavyo walipigana wakiwa mikono mitupu, Wairani, waliweza kuyashinda madola hayo yenye nguvu. Walipeperusha bendera ya kutetea uadilifu na wakaendelea kuwaunga mkono wanyonge na wanaodhulumiwa. Uungaji mkono huo uliwahamasisha Waislamu wa nchi zingine za Kiislamu kuungana na kuwa wamoja katika kukabiliana na ukoloni na udikteta. Katika miaka hiyohiyo ya awali ya ushindi wa wananchi wa Iran, Waislamu Waafghanistan wa Kishia na Kisuni waliungana pamoja na kulishinda jeshi la Shirikisho la Kisovieti la Urusi.

Wakati wachambuzi wa kisiasa wenye utegemezi kwa Magharibi wanapigia upatu dhana ya kutoweka haraka Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, huku madola makubwa ya dunia yakiendelea kila siku kuandaa mipango na njama mpya za kuuangusha mfumo wake, mapinduzi hayo yanayoongozwa na Faqihi mweledi na shujaa, huku yakiungwa mkono na wananchi, yangali yanasonga mbele ili kufikia malengo yake matukufu.

Lakini si yenyewe tu yanayosonga mbele, bali kwa kutangaza fikra za kutetea uadilifu na kuutangaza Uislamu kama dini ya kijamii na kisiasa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameonyesha na yanaendelea kuwaonyesha Waislamu wengine kwa uwazi kabisa njia ya kufikia ukombozi wa kujivua na dhulma na udikteta.Utaalamishaji huo umepelekea muongo wa kwanza wa karne ya 21 kushuhudia vuguvugu la mwamko wa Kiislamu katika nchi nyingi za Waislamu, ikiwemo Misri, Libya, Yemen, Bahrain na Tunisia. Mavuguvugu hayo ya mapinduzi yalikuwa ni ya kutaka kurejesha mifumo ya kisiasa kwenye Uislamu na kuhitimishwa uimla na udikteta wa watawala wa nchi hizo.

Imam Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

 

Naam, na hivi ndivyo Imam Khomeini (MA) alivyoyaelezea kwa usahihi kabisa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwamba yalikuwa ni mripuko wa nuru. Kwa uono wake mpana na wa mbali juu ya mustakabali na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, mzee huyo mkongwe, mweledi na mwenye hekima alitufungulia njia, ambayo tunapaswa kushikamana nayo kwa uimara hadi pumzi yetu ya mwisho na kuiendeleza kwa usahihi kabisa ili ije iwe mirathi ya watakaofuatia baada yetu. Sisi sote hatutasahau katu kwamba msingi hasa wa urithi huu ni harakati ya pamoja ya umma mzima wa Kiislamu chini ya bendera ya Utawala wa Faqihi. Harakati au vuguvugu lolote lile ambalo limeghafilika na msingi huu au limeukengeuka, limefeli na kuharibikiwa mapema na kusahaulika katika kurasa za historia. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza wapendwa wake wengi kwa ajili ya kuulinda na kuudumisha msingi huu adhimu. Hakuna shaka yoyote kuwa baada ya hapa na kuendelea, ndivyo itakavyokuwa pia na itaendelea kuwaita na kuwalingania Waislamu wote kufuata na kufungamana na njia hii ya mwongozo sahihi wa Uislamu.../