Feb 13, 2022 05:28 UTC
  • Utamaduni wa Qur'ani katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Qur'ani Tukufu ndio chanzo muhimu zaidi cha elimu na maarifa ya Uislamu, ambacho, pamoja na vyanzo vingine vya elimu ya dini, mbali na kutumiwa katika maisha ya mtu binafsi na ya kiibada, vilevile huainisha mfumo wa jamii katika masuala ya kisiasa na kijamii. 

Harakati ya kimapinduzi ya taifa la Iran dhidi ya utawala wa kimabavu wa Shah na utawala wa kifalme wa Pahlavi nayo ilianza kwa msukumo wa mafundisho hayo ya Qur'ani Tukufu yanayosisitiza kuwa: 

إِنَّ اللَّهَ لاَ یُغَیِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّى یُغَیِّرُواْ مَا بِأَنفُسِهِمْ

"Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao wenyewe yaliyomo nafsini mwao." (Raad:11)

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamejulikana kuwa ni harakati ya kurejea kwenye Qur'ani. Miongozo ya kitabu hicho kitukufu ndiyo iliyokuwa utambulisho wa kidini wa harakati hiyo. Kurejea kwenye Qur’ani kunawafanya Waislamu wajizatiti kwa mafundisho yake, kupambana na ukoloni na kupigana na dhulma, na matokeo ya mapambano hayo ni kupata izza, heshima, fahari na muhimu zaidi, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Ni kama anavyosema Mtume wetu Muhammad (saw) kwamba:

رسولُ اللّه ِ صلى الله علیه و آله : مَثَلُ القُرآنِ و مَثَلُ النّاسِ کمَثَلِ الأرْضِ و الغَیثِ ، بَینَما الأرضُ مَیّتَةٌ هامِدَةٌ إذ أرسَلَ اللّه ُ علَیها الغَیثَ فاهتَزّت ، ثُمّ یُرسِلُ الوابِلَ فتَهتَزُّ و تَربُو ، ثُمّ لا یَزالَ یُرسِلُ الأودِیَةَ حتّى تَبذُرَ وَ تَنبُتَ و یَزهُوَ نَباتُها ، و یُخرِجَ اللّه ُ ما فیها مِن زِینَتِها و مَعایِشِ النّاسِ و البَهائمِ ، و کذلکَ فِعلُ هذا القُرآنِ بالنّاسِ .

Mfano wa Qur'an na watu ni mfano wa ardhi na mvua, ambayo inapokuwa maiti na kavu ghafla Mwenyezi Mungu huteremsha mvua na ardhi inatikisika, kisha mvua kubwa inanyesha na ardhi inatikisika tena na kunawiri, kisha mito inafurika maji yanayotoka kwenye mabonde hadi mimea yake inastawi, kukua na kunawiri. Kisha Mwenyezi Mungu anatoa ardhini mapambo na chakula cha watu na wanyama; Vivyo hivyo ndivyo inavyofanya Qur'ani hii kwa watu." Vilvile Aya ya saba ya Suratu Muhammad inasema:

 یَا أَیُّهَا الَّذِینَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ یَنصُرْکُمْ وَیُثَبِّتْ أَقْدَامَکُمْ

"Enyi mlioamini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithabitisha miguu yenu."   VVV 

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini alifanya jitihada kubwa za kuwaongoza Waislamu wa Iran na duniani kuelekea kwenye ubinadamu na kuifahamu Qur'ani Tukufu, kitabu cha wahyi cha Mwenyezi Mungu. Kwa sababu kujitenga na Qur'ani Tukufu na mafundisho yake yenye kutoa uhai kunafungua njia ya upotofu wa kifikra na kivitendo katika jamii. Kwa msingi huo, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu serikali na wananchi walijielekeza sana kwenye Qur'ani Tukufu, na shughuli za Qur'ani kama vile kufanya majlisi za kiraa ya Qur'ani, mashindano ya Qur'ani, kutoa mafunzo na kutuma wasomaji wa Qur'ani kama walinganiaji wa Jamhuri ya Kiislamu katika nchi mbalimbali, kuanzisha redio ya Qur'ani, uchapishaji na usambazaji wa nakala za Qur'ani Tukufu na kufanya darasa za masomo ya Qur'ani viliongozeka kwa kiasi kikubwa. Kwa kadiri kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajifaharisha kuwa katika kipindi cha miaka zaidi ya 40 iliyopita wawakilishi wake wameshinda tuzo 180 katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ya Qur'ani.

Tafsiri ya Qur'ani Tukufu ni miongoni mwa sayansi za Kiislamu zinazoeleza na kufafanua zaidi fikra za mafundisho yanayomuokoa mwanadamu ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na kuweka wazi zaidi uzuri na siri za Aya za Mwenyezi Mungu. Hapana shaka yoyote kwamba, kwa kuwa Qur'ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu basi yanahitaji tafsiri na ufafanuzi. Kati ya vitabu vyote vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu SW, Qur'ani ndicho kitabu kilichopewa mazingatio zaidi na kufasiriwa kwa wingi zaidi na wasomi wengi. Hivyo basi miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni kuanzishwa darsa na majlisi za tafsiri ya Qur'ani katika maeneo mbalimbali ya nchi. Washiriki katika majlisi na darsa hizo, mbali na kujifunza maana na maelezo ya Aya za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu, wamekuwa wakihimizwa kufanya jitihada za kutekeleza kivitendo mafundisho ya kitabu hicho maishani mwao katika kampeni iliyopewa jina la Mtindo wa Maisha wa Qur'ani. 

Wajibu wa kustawisha na kueneza utamaduni tajiri wa Qur'ani, kuwajuza Waislamu wa maeneo mengine ya dunia mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu na vilevile kupata tajiriba ya nchi nyingine katika masuala yanayohusiana na Qur'ani viliilazimisha Idara ya Wakfu kuendeleza mashindano ya kimataifa ya Qur'ani. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa matukio muhimu na makubwa ya kila mwaka yanayohusiana na Qur'ani duniani. Mashindano hayo yalianza mwaka 1982 na yamekuwa yakifanyika kila mwaka tangu wakati huo isipokuwa kwenye miaka miwili tu kutokana na vita vya kulazimishwa vya utawala wa Saddam Hussein uliokuwa ukishambulia kwa mabomu maeneo na miji mbalimbali ya Iran.

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani mjini Tehran

Katika upande mwingine nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama Ummul Qura na kitovu cha nchi za Waislamu, iliifanya nchi hii iingie katika medani ya kuchapisha nakana za Qur'ani tukufu kwa kutumia mbinu za kisayansi na kielimu zaidi. Kwa msingi huo ilianzishwa taasisi cha kushughulikia suala hilo na mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya uhakiki katika taaluma ya uandishi, masuala ya sanaa, kutayarisha zana na vitendea kazi vinavyohitajika, usimamizi na usahihishaji wa nakala zitakazochapishwa, uchapishaji, usambazaji na mawasiliano na taasisi nyingine za uchapishaji wa nakala za Qur'ani Tukufu ndani na nje ya nchi. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, idadi ya wachapishaji wa Qur'ani ilikuwa ndogo sana na hapakuwa na usimamizi kutaalamu wa uchapishaji wa Qur'ani Tukufu. Mwaka 1364 Hijria Shamsia (yapata miaka 36 iliyopita) Taaisi ya Ulinganiaji wa Kiislamu ilikabidhiwa kazi ya kusimamia na kuchapisha nakala za Qur'ani Tukufu. Tangu wakati huo hadi sasa zaidi ya taasisi elfu moja zinafanya kazi ya kuchapisha nakala za Qur'ani nchini Iran. Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita taasisi ya Darul Qur'an imetoa kibali cha kuchapishwa nakala karibu milioni 166 za kitabu kitakatifu cha Qur'ani nchini Iran. Iwapo tutajumuisha vibali vilivyotolewa kabla ya hapo basi idadi ya nakala za Qur'ani zilizochapishwa hapa nchini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zinafika milioni mia mbili.

Uchapishaji wa nakala za Qur'ani uliongezeka kwa kiwango kikubwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

Sharti la kuwa na jamii inayofuata mafundisho ya Qur'ani ni kuhakikisha kwamba Qur'ani imeingia na kukita mizizi katika nyoyo za watu wa jamii husika, na hapana shaka kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalihitajia sana suala hilo ili kutimiza malengo yake. Kwa msingi huo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei amesema: "Inatupasa kukiri kwamba, jamii yetu ilitenganishwa na Qur'ani kwa miaka mingi. Kwa sasa Jamhuri ya Kiislamu inafanya jitihada za kupunguza ufa huo na kufidia kubakia nyuma katika uwanja huo. Wakati wa utawala wa kidhalimu wa Shah, Qur'ani haikuwepo katika jamii ya Iran. Naam, vilishuhudiwa visomo vya kitabu cha Qur'ani hapa na pale lakini kutadabari ndani ya kitabu hicho hususan katika ngazi ya jamii kulikuwa nadra sana hapa nchini.. Tunataka kufidia mapungufu hayo na hadi sasa kumefanyika kazi kubwa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na matunda yake yanaonekana. Huu ni mwanzo tu na tupasa kuungana na kushikamana kikamilifu na Qur'ani.. Tunapaswa kuhakikisha kwamba tunatekeleza Qur'ani Tukufu katika maisha yetu. Imepokewa kwamba mmoja wa wake wa Mtume Muhammad (saw) aliulizwa kuhusu maadili ya mtukufu huyo, akajibu kwamba: Maadili na akhlaki yake ilikuwa Qur'ani.

(کان خلقه القرآن) kwa maana kwamba, Mtume (saw) alikuwa Qur'ani inayotembea juu ya ardhi. Hali hii inapaswa kushuhudiwa katika jamii yetu."

Qari wa Misri, Mohammed Abdel Wahhab el-Tantawi akisalimiana na Ayatullah Khamenei, Tehran

Naam, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalirejesha tena Qur'ani na mafundisho yake katika jamii baada ya kuwekwa kando kwa miaka mingi na kuhakikisha kwamba, kisomo na mafundisho ya kitabu hicho yanatoka katika duara la mtu binafsi na kuingia katika jamii. Qur'ani ambayo ndiyo msingi na injini ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ilizidisha maarifa ya umma huku wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu wakifanya jitihada za kufifiza harakati hiyo kubwa na adhimu ya kueneza maarifa ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu chini ya kivuli cha mafundisho hayo ya Qur'ani, imefanikiwa kukabiliana na njama hizo za mabeberu na vibaraka wao kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40. 

Tags