Feb 16, 2022 03:59 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu na Uhuishaji Kigezo cha Kufuatwa na Mwanamke Muislamu

Katika kipindi cha miaka 43 tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa, zimefanyika juhudi athirifu za kuhuisha heshima ya wanawake.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi kwa ushiriki wa wananchi wote, wake kwa waume; na wanawake kwa upande wao, walitoa mchango mkubwa, athirifu na wa kipekee. Kabla ya mapinduzi, na kutokana na hujuma za utamaduni wa Magharibi, kulikuwa na mtazamo wa kiuchu kuhusiana na wanawake; na wa kuwaona kama bidhaa tu; na sifa zote za thamani za kiutu za kiumbe huyo zilikuwa katika hali ya kuchujuka, kumomonyoka na kutoweka.

Mtazamo wa Magharibi wa kumchukulia mwanamke kama bidhaa, ambao hatimaye ulifika pia hadi Iran, ulipelekea kukanyagwa na kuharibiwa utambulisho na shakhsia ya mwanamke wa Kiirani katika enzi za tawala za kifalme hapa nchini. Masaibu hayo yalianza katika karne ya 19, ambapo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyopatikana Magharibi, fikra za kimaada zilipata nguvu na kutawala na kupelekea kujitokeza fikra iitwayo Usekulari. Usekulari, ambao uliitenganisha dini na maisha na siasa, haukuzipa umuhimu wowote fikra na matendo ya kidini.

Utamaduni na fikra ya Usekulari vilifika katika nchi na mataifa ya Waislamu kuanzia mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 kwa msaada wa mfumo wa Ubepari wa Magharibi na kuingiza katika nchi hizo fikra ya Usasa na Umamboleo. Baada ya hapo na kuendelea, Ulaya na Marekani zikawa zinatambulika kama kigezo na mfano wa kuigwa katika nchi za Waislamu; na dini ikachukuliwa kuwa ni kizuizi na mkwamishaji wa Usasa. Jambo hilo lilipelekea karibu tawala zote katika nchi za Waislamu, ukiwemo wa Kipahlavi nchini Iran kuchukua hatua ya kuzielekeza nchi kwenye Usasa na Umamboleo, hali ambayo iliathiri mno maisha ya binafsi na ya kijamii ya wanawake na mfumo mzima wa familia.

Reza Khan, mfalme wa zama hizo wa Iran, ambao kwa kweli alikuwa kibaraka wa Ukoloni alitoa amri ya kuacha kuvaa Hijabu wanawake wa Iran ili nchi iendane na mfumo wa Usasa na Umamboleo.

Uvuaji Hijabu uliofanywa na mke wa Mfalme na mabanati wake

Wanawake Wairani, ambao hadi wakati huo walikuwa wakijisitiri kikamilifu kwa vazi la staha la hijabu walipokuwa kwenye hadhara za watu, walianza kuvutwa na kuvuliwa shungi kwa nguvu, kwa mateke na virungu na askari wa utawala wa Shah na kulazimika kutembea vichwa wazi. Mfalme Reza Khan, ambaye hakuwa na elimu na ujuzi wa kutosha wa mambo, hakuweza kutambua kuwa, chimbuko la kidini, kiutamaduni, kijamii na kihistoria la Iran limetokana na misingi ya mafundisho yanayojenga na yaliyotukuka ya Uislamu; na kwamba kuwavua shungi na mitandio wanawake kutasababisha matatizo mengi na mivutano mikubwa. Hatua hiyo iliwafanya wanawake wengi Waislamu Wairani wavaao Hijabu waamue kujitenga kikamilifu na hadhara za kijamii  ili kulinda heshima na staha yao; na kuna baadhi yao ambao waliamua kwa miaka kadhaa kubakia majumbani tu!

Baada ya Reza Shah kuondolewa madarakani na vikosi vya jeshi la Uingereza, Mohammad Reza Shah, naye pia aliamua kufuata njia potofu aliyopita baba yake. Hatua mbalimbali zilichukuliwa, si na serikali na maafisa wa serikali pekee, bali hata na wanawake na wanaume waliokuwa nje ya serikali, ili kuwafanya wanawake wabadilishe mavazi yao na wabadilike pia katika kusuhubiana na kulahikiana na wanaume. Ni kama kwamba kulikuwa na sera maalumu, iliyolenga kujenga dhana kwamba, kuwa na haya na staha si jambo linalopendeza kwa wanawake; bali ni kinyume chake; yaani kujiremba kupindukia, kujionyesha mbele ya wanaume na kuwa na maingiliano nao yasiyo na mpaka ndiyo silka na mwenendo unaofaa kufuatwa na wanawake.

Shah wa Iran, ambaye alikuwa ndiye kiongozi mkuu wa nchi, yeye mwenyewe alikuwa akiwaangalia wanawake kwa jicho la kuwadunisha na kuwaona kama bidhaa tu; na alikuwa maarufu pia kwa uasherati. Waandishi wa kumbukumbu za Shah wamefichua mengi kuhusu ufuska na ufisadi wake. Mfano mmojawapo wa hayo ni maneno aliyosema Ali Shahbazi, askari wa kikosi cha gadi ya Mfalme na mkuu wa timu ya walinzi wa Shah, ambaye katika kitabu cha kumbukumbu zake, ameeleza yafuatayo kuhusu uasherati wa Shah: "Kuanzia wakati Alam alipokuwa waziri, aliunda kitengo maalumu ndani ya wizara ya masuala ya ufalme, ambapo...wahusika wake walikuwa na kazi ya kumpelekea Shah wake za watu, mabanati wenye sura jamili na au wake na mabinti za watu waliokuwa wakitaka kupewa vyeo."

Imam Khomeini (MA)

 

Imam Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameizungumzia kama ifuatavyo, hali ya dhulma na udhalilishaji iliyowafika wanawake katika zama za utawala wa Kifalme: "Mwanamke alidhulumika katika vipindi viwili; kimoja ni katika zama za ujahilia, ambapo Uislamu ulimfadhili mwanadamu kwa ujumla na hasa mwanamke kwa kumtoa kwenye hali ya kudhulumika aliyokuwa nayo. Kipindi kingine ni katika Iran yetu; mwanamke alidhulumika pia, na hiyo ni katika zama za Shah aliyepita na Shah wa sasa. Kwa kutumia kisingizio cha kutaka kumkomboa mwanamke, walimtendea mwanamke kila aina ya dhulma, walimshusha mwanamke kwenye nafasi ya heshima na utukufu aliokuwa nao, kutoka kwenye nafasi ya umaanawi aliyokuwa nayo, wakamfanya ni kitu tu; na kwa kutumia jina la uhuru, "uhuru wa wanawake" na "uhuru wa wanaume" wakaupora uhuru wa mwanamke na mwanamme na wakawafanya wanawake na vijana wetu wawe na tabia chafu..." (Sahifa ya Nuru, Juzuu ya 6)

Wanawake wa Iran wamepata mafanikio makubwa katika michezo, sambamba na kuchunga vazi la staha la Hijabu

 

Lakini vielezi na vitambulishi vinavyoainisha nafasi ya mwanamke katika jamii ya Kiislamu vinajengwa kwa kufuata mtazamo wa kitauhidi kuhusiana na ulimwengu. Katika mtazamo huo, pamoja na kuwepo uhuru wa kuchagua kazi au ajira, mume, elimu na shughuli nyinginezo kwa ajili ya wanawake, lakini kitu kinachompa utambulisho mwanamke, ni nafasi yake katika malezi ya kizazi na jamii. Kazi ya umama ina thamani kama ilivyo kazi ya Utume. Na subira kubwa na moyo wa huruma iliyokithiri aliyonayo mama katika kazi ya kulea mtoto safi na mwema, ina nafasi na hadhi sawa na subira na juhudi kubwa walizofanya Mitume kwa ajili ya kuwaongoa wanadamu.

Imam Khomeini, kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye alikuwa alimu wa kupigiwa mfano, kama ulivyo mtazamo wa dini, alikuwa na mtazamo wa kumpa heshima, wa kumthamini na wa kumjenga mwanamke. Alikuwa akiamini kuwa, mwanamke ana hadhi ya heshima, sharafu, izza na utukufu. Mwanamke ana uwezo wa kufikia daraja ya juu kabisa ya umaanawi huku akijishughulisha pia na shughuli za kitaaluma, kisiasa na kijamii. Imam Khomeini alikuwa akiitakidi kwamba, kwa mtazamo mtukufu wa Uislamu, lengo la mwanadamu, awe mwanamke au mwanamme, ni kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu; na kwa hivyo kumwabudu Mwenyezi Mungu na kudhihirisha uja kwake ni jambo linalomjenga na kumpandisha daraja mwanamke ili kufikia cheo cha kumkurubisha kwa Mola.

Katika moja ya hotuba zake muhimu sana kuhusu mwanamke, Imam Khomeini anasema: "mwanamke ni mtu, tena ni mtu mkubwa; mwanamke ni mlezi wa jamii. Watu wanakulia kwenye mikono ya mwanamke... na kutengenekewa na kuharibikiwa nchi yoyote ile kunategemea na kuwepo kwa mwanamke. Kwa malezi yake sahihi, mwanamke anamjenga mtu na kwa malezi yake sahihi anaistawisha nchi."

Akiendelea kulizungumzia hilo, Imam Khomeini anaashiria mtazamo wa Uislamu na mwenendo wa kuvutia wa Bwana Mtume Muhammad SAW kuhusiana na mwanamke na anasema: "Historia ya Uislamu ni shahidi wa jinsi Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehma na amani ya Allah ziwe juu yake na Aali zake, alivyokuwa akimpa heshima kubwa mno binti yake, mzaliwa huyo mtukufu Bibi Fatimatu-Zahra SA, ili kuonyesha kuwa mwanamke ana ukubwa maalumu katika jamii, ukubwa ambao kama si wa juu zaidi kuliko wa mwanamme, basi haupungui."

Wanawake wanakwea daraja za elimu sawa na wanaume baada ya Mapinduzi ya Kiislamu

 

Imam Khomeini alikuwa akiwaambia akina mama wajitahidi katika kuchota elimu na wasiache kufanya kila juhudi kwa ajili ya kujijenga kwa fadhila na utukufu wa kiakhlaqi na kuzitakasa nafsi zao, kwa sababu wanawake ndio chimbuko la kheri na saada kwa ajili ya jamii. Imam Khomeini alikuwa akiwataka wanawake wajihusishe na masuala ya kisiasa kama walivyo wanaume; na kama ambavyo wanaume wanajishughulisha katika nyuga za kitaaluma na kiutamaduni, nao pia wafanye hivyo; lakini katika kushiriki kwao katika nyanja zote hizo wasiache kuchunga hijabu, staha, murua na heshima yao.

Katika kipindi cha miaka 43 tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa, zimefanyika jitihada athirifu za kuhuisha na kurejesha heshima na hadhi ya wanawake. Wanawake Waislamu wa Iran, hivi sasa wameweza kupata mafanikio makubwa katika nyuga tofauti za kitaaluma na utafiti, michezo, utabibu, teknolojia, sanaa, utengezaji dawa na chanjo na katika nyanja za masuala mengine yanayohitajika nchini. Wanawake Waislamu wa Iran wameonyesha kuwa kushika dini mwanamke na kuvaa hijabu si tu hakuwi kizuizi cha kumfanya ashindwe kufikia malengo ya juu, bali kunamwandalia mazingira salama zaidi, ya thamani zaidi na ya uhakika zaidi kwa ajili ya kufikia vilele vya mafanikio.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei anasema, mtazamo wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu wanawake unatokana na mtazamo uliotukuka wa Uislamu kuhusu mwanamke; na alifafanua hilo kama ifuatavyo: "katika mantiki ya Uislamu, mwanamke ana mwongozo na kigezo kamili cha kufuata; mwanamke wa Kiislamu, maana yake ni kiumbe mwenye imani na staha; anayebeba sehemu muhimu zaidi ya malezi ya mwanadamu; ni mwenye taathira kwa jamii; anajengeka kitaaluma na kimaanawi; ni mwendeshaji wa chombo muhimu sana cha familia na ndiye sababu ya kupata utulivu jinsia ya kiume. Haya yote yanaunganika pamoja na sifa za kike kama upole, uraufu wa moyo na utayarifu wa kupokea nuru ya uongofu wa Mwenyezi Mungu. Hiki ndicho kigezo cha mwanamke wa Kiislamu. Mkabala wake, siku zote katika historia kimekuwepo kigezo cha mtazamo potofu; leo hii kigezo hicho potofu ni mwanamke wa Kimagharibi, ambaye sifa zake yeye, kinyume na zile sifa zote bora na za kipekee tulizoeleza kuhusu mwanamke wa Kiislamu, ni kuweza kumvutia, kumtamanisha na kumstarehesha mwanamme. Kwa sababu hiyo, kielelezo cha mwanamke wa Kimagharibi ni kukaa utupu. Mnaona nyinyi wenyewe, katika hafla zao, mwanamme lazima awe amejisitiri kikamilifu, lakini mwanamke awe yuko utupu zaidi kadiri iwezekenavyo".../

Tags