Jul 08, 2022 09:30 UTC
  • Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu, 1443 Hijiria

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu. Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu, na swala na salamu zake zimshukie Muhammad al-mustafa na Aali zake watoharifu na Masahaba zake weme.

Tumashukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mwenye Hekima ambaye kwa mara nyingine tena ameufanya msimu wa Hija kuwa sehemu ya kukusanyika mataifa ya Kiislamu na kuwafungulia njia hiyo ya fadhila na rehema. Hivi sasa na kwa mara nyingine Umma wa Kiislamu unaweza kushuhudia umoja na mshikamano wao katika kioo hiki kisafi na cha kudumu milele na hivyo kupata fursa ya kujiepusha na mambo yanayowatenganisha na kuwagawanya.

Umoja wa Waislamu ni moja ya nguzo mbili za msingi za Hija, ambazo iwapo zitafungamanishwa na kudhikiri (dhikr) na umaanawi, ambayo ni nguzo nyingine ya wajibu huu wa ajabu, zinaweza kuufikisha Umma wa Kiislamu kwenye kilele cha heshima na furaha na kuufanya kuwa mfano wa wazi wa kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini. Lakini wanaafiki hawajui.

Hija ni mjumuiko wa nguzo mbili hizi za kisiasa na kimaanawi na dini tukufu ya Uislamu ni mchanganyiko mtukufu na adhimu wa siasa na umaanawi. Katika historia ya hivi karibuni, maadui wa mataifa ya Kiislamu wamefanya juhudi kubwa kwa ajili ya kudhoofisha nguzo mbili hizi zinazotoa uhai, yaani umoja na umaanawi miongoni mwa mataifa yetu. Wameudhoofisha umaanawi kwa kueneza mtindo wa maisha wa Kimagharibi, ambao ni mtupu kimaanawi kwa kutoona mbali. Wanaibua matatizo na kuvuruga umoja wa Waislamu kwa kueneza mambo yasiyo na msingi na yanayoibua hitilafu kama vile tofauti za lugha, kabila, rangi na maeneo ya kijografia.

Umma wa Kiislamu, ambao mfano wake mdogo tu sasa unaonekana katika amali tofauti za Hija, unapasa kusimama na kukabiliana na suala hili kwa nguvu zake zote. Yaani kwa upande mmoja, unapasa kuimarisha ukumbusho wa Mungu, kufanya kazi kwa ajili ya Mungu, kutafakari neno la Mungu na kutumainia ahadi za Mungu katika kila jambo, na kwa upande mwingine, kukabiliana na kushinda kila mienendo ya migawanyiko na hitilafu. Kinachoweza kusemwa kwa uhakika hii leo ni kwamba hali ya sasa duniani na katika ulimwengu wa Kiislamu ni nzuri zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa ajili ya kufanikisha juhudi hizi zenye thamani.

Hii ni kwa sababu, kwanza kabisa, leo hii wasomi na umati mkubwa wa watu katika nchi za Kiislamu umetilia maanani utajiri wao mkubwa wa kiakili na kimaanawi na umetambua umuhimu na thamani yake. Leo, uliberali na ukomunisti, ambao ni dhihirisho muhimu zaidi la ustaarabu wa Magharibi, hauna tena sura kama ile iliyokuwepo katika miaka mia moja na miaka hamsini iliyopita. Heshima iliyokuwanayo demokrasia ya pesa ya nchi za Magharibi hivi sasa inatiliwa shaka kubwa ambapo wanafikra wa Magharibi wanakiri kwamba wamechanganyikiwa kutokana na kupotoshwa kiakili na kiutendaji. Katika ulimwengu wa Uislamu, vijana, wanafikra, wasomi na wanazuoni, kwa kuona hali hii, wamepata mtazamo mpya kuhusu utajiri wao wa kielimu na pia misimamo ya kisiasa iliyo katika nchi zao, na huu ndio ule mwamko wa Kiislamu ambao tunauzungumzia daima.

Pili, kujitambua huku kwa Kiislamu kumezua jambo la ajabu na la kimiujiza katika moyo wa ulimwengu wa Kiislamu, ambapo madola yenye kiburi duniani yanakabiliwa na matatizo makubwa katika uwanja huo. Jina la jambo hilo ni "mapambano (muqawama)" na ukweli wake ni kuibuka nguvu ya imani, jihadi na kutawakali (kwa Mwenyezi Mungu). Jambo hili ndilo lile lile ambalo lilikuwepo mwanzoni mwa Uislamu na kuzungumziwa katika Aya hii tukufu inayosema: Walioambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa. Basi wakarudi na neema na fadhila za Mwenyezi Mungu. Hapana baya lililowagusa, na wakafuata yanayomridhi Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.

Medani ya Palestina ni moja ya madhihirisho ya jambo hilo la kustaajabisha ambapo imeweza kuutoa utawala wa Kizayuni katika hali ya kuhujumu hadi katika hali ya kujitetea na kutojua la kufanya na wakati huo huo kuuibulia matatizo chungu nzima yanayoukabili hivi sasa, ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi. Mifano mingine mizuri ya mapambano inaweza kuonekana wazi katika nchi za Lebanon, Iraq, Yemen na maeneo mengine.

Tatu, pamoja na hayo yote, dunia hii leo inashuhudia kielelezo chenye mafanikio na cha fahari cha uwezo na mamlaka ya kisiasa ya Uislamu katika Iran ya Kiislamu. Uthabiti, kujitawala, maendeleo na heshima ya Jamhuri ya Kiislamu ni tukio kubwa, lenye maana na la kuvutia linaloweza kuvutia fikra na hisia za kila Muislamu aliye macho. Kutokuwa na uwezo na wakati mwingine vitendo vibaya vya sisi wahudumu wa mfumo huu, ambavyo vimechelewesha kupatikana baraka zote za serikali ya Kiislamu, havijaweza kamwe kuitikisa misingi imara na hatua madhubuti zinazotokana na misingi ya mfumo huu wala kusimamisha maendeleo yake ya kimaada na kimaanawi. Mwanzoni mwa orodha ya kanuni hii ya kimsingi, ni utawala wa Uislamu katika kutunga sheria na utendaji, kuegemea kura za wananchi katika masuala muhimu ya kiutawala ya nchi, uhuru kamili wa kisiasa, na kutotegemea madola ya kidhalimu umewekwa katika kilele cha uendeshaji wa nchi. Na kanuni hizi ndizo zinazoweza kuwa mahali pa maafikiano baina ya mataifa na serikali za Kiislamu na kuufanya Umma wa Kiislamu kuunganishwa na kushikamana katika mielekeo na ushirikiano wake.

Haya ni mazingira na mambo ambayo yamepelekea kupatikana fursa mwafaka zilizopo hivi sasa; kwa Uimwengu wa Kiislamu kupiga hatua kwa umoja na mshikamano. Serikali za nchi za Kiislamu, wenye vipawa wa kidini na wa kiakademia, wataalamishaji wenye fikra huru na vijana wenye kiu ya kujua ukweli ndio wanaopaswa kufikiria zaidi jinsi ya kufaidika na mazingira haya mwafaka yaliyopo.

Ni kawaida kwa madola ya kiistikbari, na zaidi Marekani, kuingiwa na wasiwasi kutokana na kujitokeza muelekeo huu katika Ulimwengu wa Kiislamu na kutumia nyenzo zao zote kwa ajili ya kukabiliana nao; ndivyo ilivyo hivi sasa. Kuanzia kwenye mtandao mkuu wa vyombo vya habari na mbinu za vita laini, uwashaji moto wa vita, uchocheaji vita vya niaba, uenezaji chokochoko na usambazaji sumu za kisiasa; mpaka utoaji vitisho, kurubuni na kutoa hongo… vyote hivyo vinatumiwa na Marekani na waistikbari wengine ili kuuondoa Ulimwengu wa Kiislamu kwenye mkondo wa njia yake ya mwamko, fanaka na saada. Utawala mtendajinai na mwovu wa Kizayuni uliopo katika eneo hili, nao pia ni moja ya nyenzo zinazotumiwa katika hujuma hizi za kila upande.

Kwa fadhila na irada ya Mwenyezi Mungu, mara nyingi hujuma na njama hizi zimekuwa zikigonga mwamba; na Magharibi ya Kiistikbari imezidi kuwa dhaifu siku baada ya siku katika eneo letu nyeti na hasasi; na kwa hivi karibuni, ulimwenguni kote. Mfadhaiko na kushindwa Marekani katika eneo pamoja na mshirika wake mtendajinai yaani utawala ghasibu, kunaweza kuonekana kwa uwazi kabisa katika medani ya matukio ya Palestina, Lebanon, Syria, Iraq, Yemen na Afghanistan.

Katika upande wa pili, Ulimwengu wa Kiislamu umejaa vijana wenye motisha na ari kubwa. Rasilimali kubwa zaidi ya kujengea mustakabali ni kuwa na matumaini na moyo wa kujiamini, mambo ambayo leo yameshamiri katika Ulimwengu wa Kiislamu, hasa katika nchi za eneo hili. Ni wajibu wetu sote kuilinda na kuiongeza rasilimali hii.

Pamoja na yote haya, tusighafilike hata chembe na hila za adui; tujiepushe na ghururi na mghafala na tuongeze juhudi zetu na tuzidi kuwa macho; na katika kila hali, kwa mazingatio na unyenyekevu, tumuombe msaada Mwenyezi Mungu Mweza na Mwenye Hekima.

Kuhudhuria katika hadhara na amali za Hija ni fursa adhimu kwa ajili ya kutawakali na kunyenyekea na vilevile kwa ajili ya kutafakari na kuchukua maamuzi.

Waombeeni dua ndugu zenu Waislamu duniani kote; na mwombeni Mwenyezi Mungu awape taufiki na ushindi. Katika dua zenu hizo, niombeeni pia na mimi ndugu yenu nipate mwongozo na msaada wa Mwenyezi Mungu.

Wassalamu Alaykum Warahmatullah

Sayyid Ali Khamenei

5 Dhilhijjah 1443