Jul 14, 2022 07:47 UTC
  • Imam Ali al Hadi (as), Taa ya Uongofu

Imam Hadi (as) alizaliwa tarehe 15 Dhul Hijja mwaka 212 Hijiria katika mji mtakatifu wa Madina. Alipewa lakabu ya al-Hadi kwa maana ya muongozaji. Alitekeleza vyema jukumu hilo la kuongoza jamii ya Kiislamu kwa muda wa miaka 33.

Katika zama hizo umashururi wa Imam Hadi (as) alienea kwa kasi katika maeneo yote ya karibu na mbali na kuwafanya watu waliokuwa na kiu kubwa ya kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kukimbilia kwake mjini Madina kwa lengo la kunufaika na elimu yake. Muhammad bin Shahrashub ni mmoja kati ya wanahistoria wa Kiislamu, waliofanya utafiti na kuandika kwa mapana na marefu historia ya Ahlubait wa Mtume (saw). Anaandika katika kitabu chake cha Manaqib Aal Abi Talib kuhusu maadili mema na tabia njema za Imam al Hadi (as) akisema: ''Alikuwa mtu mwenye roho mzuri na msema ukweli zaidi kati ya watu wote wa zama zake. Alipokaa kimya uso wake uling'ara kwa utukufu maalumu, na alipozungumza, maneno na shakhsia yake ilikuwa ikiwavutia watu wote.''

Imam Ali an-Naqi al-Hadi (as) ni mfano bora wa neema na rehema ya Mwenyezi Mungu ambayo amewajaalia waja wake. Alikuwa nuru na taa inayowaelekeza wanadamu kwenye njia ya ukamilifu ili wale waliopotea na kukwama njiani waweze kuongozwa na taa hiyo kwenye njia nyoofu inayowaelekeza kwa Mola wao. Sira na mwenendo wa maisha yake pia ni mfano bora kwa wanaotafuta ukamilifu.

Imam al Hadi (as) alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu mwaka 220 Hijria baada ya kuuawa shahidi baba yake, akiwa na umri wa miaka minane tu. Katika zama za uongozi wake, utawala wa Bani Abbas ilikuwa ukidhoofika taratibu na kuelekea ukingoni. Kama walivyokuwa babu zake, tabia na maadili bora ya Imam Hadi (as) viliwafanya watu waliokuwa wamechoshwa na dhulma na uonevu wa watawala dhalimu wa ukoo wa Bani Abbas wapokee kwa moyo mkunjufu tabia hizo njema, miongozo na mafundisho sahihi ya Uislamu ya Imam Hadi (as). Hali hiyo pamoja na uchamungu mkubwa wa Imam, iliwavutia sana watu, suala lililozidisha idadi ya wafuasi wa Ahlulbat (as) siku baada ya nyingine. Tabia njema za Imam (as), ambaye alishi katika kipindi cha makhalifa sita wa Bani Abbas, iliwavutia zaidi watu katika njia sahihi, yaani mafundisho halisi ya Uislamu. Watawala hao waovu walimsumbua na kumtesa sana mjukuu huyo wa Mtume katika kipindi cha uongozi wake wa Umma wa Kiislamu. Hatimaye wa mwisho wao, yaani Mu'tassim, alimpa sumu na kumuua shahidi Imam Ali al Hadi al Naqi (as). Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba licha ya watawala hao madhalimu kuwa katika kilele cha nguvu za kidhahiri humu duniani, lakini waliishi na kuaga dunia kwa madhila makubwa na hii leo historia inawakumbuka kama watawala madhalimu na makatili mkubwa. Katika upande wa pili, Imam Ali al Hadi (as) anatakwa kwa taadhima na kutukuzwa na mamilioni ya Waislamu, na miongozo na mafundisho yake yamebakia kama tochi na taa inayowamulikia wanadamu katika njia ya uongovu.  

Lakabu na jina alilopewa Imam Ali an-Naqi (as), yaani "al-Hadi" linaweka wazi hakika nyingi mno. Neno 'hidaya' Katika lugha ya Kiarabu lina maana ya kuonyesha njia na kufikisha mahala panapokusudiwa, ambapo kwa kawaida huwa ni mahala pazuri na chanya. Katika utamaduni wa Quráni na maarifa ya Ahlul Beit (as), neno hili lina maana ya kina zaidi kuliko makusudio ya kidhahiri na kijiografia tu. Kuijua vyema njia, mahala pa kufikia, kuelewa umma na walio kwenye msafara, kutambua vikwazo na matatizo ya njiani, kuhamasisha wasafiri kwa ajili ya kufanya harakati, kuhamasisha moyo wa ukakamavu miongoni mwa wasafiri na kuonyesha njia na kuongoza msafara ni sehemu ya maana ya neno 'al Hadi' katika utamaduni wa Kiislamu. Imam al Hadi (as) alikuwa jua lililongára ambalo katika miaka ya 220 hadi 254 Hijiria alichukua usukuani wa kuongoza Umma mkubwa wa Kiislamu, na kwa kipindi cha karibu miaka 34 alikuwa nahodha shupavu wa meli ya Uislamu katika mawimbi makali na ya kutisha ya zama za watawala dhalimu wa Bani Abbas. 

Kama ilivyokuwa katika zama za mababu zake watukufu, kipindi cha Imam Hadi (as) kilikuwa msimu wa hekima na madini ya elimu na maarifa. Fikra nyingi za kiitikadi zilijitokeza zikiambatana na nadharia tofauti kuhusiana na misingi ya itikadi ya Kiislamu; nadharia potovu ambazo kwa hakika zilikuwa zikihatarisha na kupotosha fikra halisi za Uislamu. Kutokana na kipawa chake kikubwa cha maarifa ya Kiislamu, nuru ya hidaya na mwongozo wake, Imam Hadi (as) aliweza kufunga milango mingi ya upotovu huo, na wakati huo huo kubainisha kwa usahihi fikra halisi za Uislamu, na kubatilisha fikra zilizokuwa zikienezwa na maadui wa Uislamu. Mbali na kuhuisha mafundisho na maarifa ya Uislamu, Imam alikuwa mstari wa mbele katika kushugulikia masuala mbalimbali ya kijamii na kutatua matatizo ya watu, kwa kadiri kwamba hakuna mtu yoyote aliyetoka nyumbani kwake hali ya kuwa amekata tamaa. 

Alikuwa mwingi wa ibada na mchamungu mkubwa kwa kadiri kwamba wanazuoni wakubwa wa Kiislamu kama Ibnu Kathir, anamsifu mjukuu huuyo wa Mtume huyo kwa kusema: "Alikuwa mchamungu mwenye takwa na zuhudi kubwa."

Kuwaongoza wanadamu na kuwaelekeza kwenye mambo mema huhitajia maarifa mengi na ya hali ya juu, ambayo hujumuisha pande zote za maisha yao. Viongozi wote maasumu walikuwa na maarifa hayo. Katika mojawapo ya matamshi yake ya kuvutia, Imam Ali al Hadi (as) anasema: ''Jina Kuu la Mweyezi Mungu (Al Ismul A'dham) lina herufi 73, na Asif ibn Barkhiya (aliyekuwa wasii, rafiki wa karibu na katibu wa Nabii Sulaiman AS) alikuwa akijua herufi moja tu kati ya herufi hizo. Alitamka herufi hiyo .. na hivyo akaweza kumletea Nabii Suleiman (as) kiti cha enzi cha Malkia Bilqis katika muda mfupi sana, ulio chini ya kupepesa jicho. Herufi 72 kati ya hizo tunazo sisi Ahlulbait, na Mwenyezi Mungu amejiwekea herufi moja ambayo inahusiana na elimu ya ghaibu.''

Haram ya Imam Ali al Hadi (as), Iraq

Imam Hadi (AS) hakuwa mwanga ulioangaza na kuvutia nyoyo za Waislamu pekee. Bali nuru ya maarifa yake iliangaza dunia nzima na kuzivutia nyoyo za watu wote. Sifa na shakhsia yake viliwavutia wafuasi wa madhehebu na dini zote ambao waliathiriwana sifa zake njema pamoja na nafasi yake ya juu kielimu. Yazdad, tabibu wa Kikristo ni miongoni mwa watu waliovutiwa sana na elimu kubwa ya Imam Hadi (AS). Anasema: "Kama kulikuwepo mtu aliyekuwa na maarifa na elimu ya kila jambo (katika zama zake) basi mtu huyo ni Imam al Hadi peke yake. Watawala wa Bani Abbas walimpeleka Samarra ili kuwazuia watu wasimfuate, kwa sababu uwepo wake miongoni mwa watu ulihatarisha utawala wao", mwisho wa kunukuu.  

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa semi za hekima za Imam al Hadi (as). Anasema: "Yeyote anayemcha Mwenyezi Mungu, watu watamcha, anayemtii Mungu, wanadamu watamtii, na anayemtii Muumba hataogopa ghadhabu ya viumbe wake, na anayemkasirisha Muumba lazima awe na hakika kwamba atakumbwa na ghadhabu za viumbe."

مَنْ اتَّقی الله یتَّقی، وَ مَنْ اطاعَ لله یطاع، و من اطاعَ الخالق لم یبال سَخَطَ المَخْلُوقین، و مَنْ اَسْخَطَ الخالق فَلییقَنَ ان یحِلَّ به سَخَطَ المَخلوقین

Anasema katika hadithi nyingine kwamba: ''Tahadhari na mtu anayeiona duni nafsi yake, na wala hatambua thamani yake.'' مَنْ هانَتْ علیه نَفْسَهُ فلاتَأمَنْ شَرَّهُ 

Vimevile amesema: Dunia ni soko ambamo kundi moja limepata faida ndani yake, na kundi jingine linapata hasara. اَلدُّنْیا سُوقٌ رَبِحَ فیها قَوْمٌ وَ خَسِرَ آخَروُنَ

Imam al Hadi pia alikuwa akiwahimzia Waislamu kukumbuka mwisho wa maisha yao hapa duniani kutokana na taathira yake katika mienendo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Anasema: Kumbuka mwisho wa uhai wako, ukiwa umelala kitandani baina ya watu wa familia yako; na hakuna tabibu anayeweza kuzuia kifo chako, wala rafiki wa kukufaa lolote.

اذْکُرْ مَصْرَعَکَ بَیْنَ یَدَیْ أَهْلِکَ وَ لَا طَبِیبَ یَمْنَعُکَ وَ لَا حَبِیبَ یَنْفَعُکَ

Kwa hakika hii ndiyo hulka na tabia ya watu wenye busara na akili ambao daima hukumbuka mwisho na matokeo ya kazi na maisha yao kutokana na taathira zake kubwa katika mienendo na maisha yao. Babu yake Imam Ali al Hadi (as), yaani Mtume wetu Muhammad al Mustafa (saw) anasema: Enyi watu! Mwenye akili zaidi kati yenu ni yule anayekumbuka kifo zaidi." یَا أَیُّهَا النَّاسُ إِنَّ أَکْیَسَکُمْ أَکْثَرُکُمْ ذِکْراً لِلْمَوْت‌

Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri na baraka kwa Waislamu wote hususan wafuasi na wapenzi wa Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume wetu Muhammad (saw) kwa kwa mnasaba wa kuadhimisha na kukumbuka siku ya kuzaliwa mjukuu wake mwema, Imam Ali al Hadi al Naqii (sa). Tunamuomba Mwenyezi Mungu SW aturuzuku shafaa yao Siku ya Kiyama na atufufue pamoja na Mtume na Aali zake Kiramu.